Elgon (mlima)
.
Mlima Elgon ni volkano iliyolala mpakani mwa nchi za Uganda na Kenya [1] kwa upande wa Kenya upo sehemu ya kaskazini mwa Kisumu na magharibi mwa Kitale. Kasoko yake ina kipenyo cha kilomita nane.
Elgon ni mlima wa pili kwa urefu nchini Kenya baada ya Mlima Kenya. Kwa upande wa Uganda ni mlima mrefu mashariki mwa nchi lakini safu milima ya Ruwenzori ni mirefu kuliko mlima Elgon.
Majina
Jina la mlima limetokana na Waelgonyi walioishi upande wa kusini wa mlima. Wakati mwingine hujulikana kama Wasabaot, ambao wanaishi upande wa kusini wa mlima.
Ulijulikana pia kama "Ol Doinyo Ilgoon" (Mlima wa Matiti) kwa Wamaasai na kama "Masaba" upande wa Uganda.
Vilele
Mlima Elgon unajumuisha vilele vikuu vitano:
- Wagagai (mita 4,321), kikiwa nchini Uganda.
- Sudek (mita 4,302 au futi 14,140) nchini Kenya
- Koitobos (mita 4,222 au futi 13,248),kilele chenye madini aina ya basalt (Kenya)
- Mubiyi (mita 4,211 au futi 13,816)
- Masaba (mita 4,161 au 1futi 3,650)
Vipengele vya Mlima Elgon
Ndiyo volkano kongwe na kubwa zaidi iliyo peke yake katika Afrika Mashariki, ikifunika eneo la takribani kilomita mraba 3500.
Vipengele vingine vya kuvutia ni:
- Volkano aina ya kaldera - Elgon ni mojawapo ya volkano aina ya kaldera iliyo kubwa na imara duniani.
- Visima vya maji moto kando ya Mto Suam
- Endebess Bluff (mita 2563 au futi 8408)
- Mapango ya Ngwarisha, Makingeny, Chepnyalil na Kitum. Pango la Kitum lina upana wa mita 60 na hupenyeza mita 200 ndani ya mlima. Hutembelewa sana na tembo ambao hulamba chumvi inayotokana na wao kugonga kuta zake na pembe zao. Pango hilo lilitambulika sana kwa virusi vya Marburg baada ya watu wawili waliotembelea pango hili (mmoja mwaka wa 1980 na mwingine mwaka wa 1987) kuambukizwa ugonjwa huo na kufa.
Mchanga wa mlima huu ni maram mekundu. Mlima huo ni eneo la vyanzo vya mito kadhaa kama vile Mto Suam unaokuwa Mto Turkwel katika maeneo ya chini na humwaga katika Ziwa Turkana, Mto Nzoia na Lwakhakha ambayo hutiririka hadi Ziwa Viktoria. Mji wa Kitale uko chini ya mlima huu. Eneo lililo karibu na mlima huu limelindwa na mbuga mbili za Kitaifa: Mbuga ya Kitaifa ya Mlima Elgon, moja kila upande wa mpaka wa kimataifa.
Baadhi ya mimea adimu hupatikana kwenye mlima huu, ikiwa ni pamoja na Ardisiandra wettsteinii, Carduus afromontanus, Echinops hoehnelii, Ranunculus keniensis na Romulea keniensis.
Mnamo mwaka wa 1896, C.W. Hobley alikuwa Mzungu wa kwanza kuzunguka mlima huu. Kmunke na Stigler ndio wa kwanza kupanda hadi juu ya vilele vya Wagagai na Koitobos katika mwaka wa 1911 na kurekodiwa. F. Jackson, E. Gedge, na J. Martin ndio wa kwanza kupanda hadi juu ya kilele cha Sudek katika mwaka wa 1890 na kurekodiwa. Kilele kikuu ni rahisi kupanda na hakihitaji vifaa vyovyote vya kupanda milima.
Tazama pia
- Hifadhi ya Taifa ya Mlima Elgon
- Orodha ya milima ya Kenya
- Orodha ya milima ya Uganda
- Orodha ya milima ya Afrika
- Orodha ya milima
- Orodha ya volkeno nchini Kenya
Tanbihi
- ↑ "Uganda Wildlife Authority". www.uwa.or.ug. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2007-12-24. Iliwekwa mnamo 2008-03-16.
Marejeo
- Scott, Penny (1998). From Conflict to Collaboration: People and Forests at Mount Elgon, Uganda. IUCN. ISBN 2-8317-0385-9.
Viungo vya nje
- Mapango ya Mlima Elgon Ilihifadhiwa 28 Januari 2010 kwenye Wayback Machine.
- Mbuga ya Kitaifa ya Mlima Elgon Ilihifadhiwa 28 Agosti 2008 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu maeneo ya Kenya bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Elgon (mlima) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |