Nenda kwa yaliyomo

Mdudu-gamba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mdudu-gamba
Mdudu-gamba mwororo kijani (Coccus viridis)
Mdudu-gamba mwororo kijani (Coccus viridis)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye mwili wa pingili na miguu ya kuunga wasio na ugwe wa mgongo kama wadudu, nge, buibui)
Nusufaila: Hexapoda (Arithropodi wenye miguu sita)
(bila tabaka): Dicondylia (Wadudu walio na mandibula zenye condyle mbili)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Linnaeus, 1758
Nusungeli: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Lang, 1888
Oda ya juu: Paraneoptera
Oda: Hemiptera
Haeckel, 1896
Nusuoda: Sternorrhyncha
Familia ya juu: Coccoidea
Handlirsch, 1903
Ngazi za chini

Familia 39:

Wadudu-gamba au wadudu magamba ni wadudu wadogo wa familia ya juu Coccoidea katika oda Hemiptera ya nusungeli Pterygota (wenye mabawa). Spishi nyingi ni sumbufu, hususa kama wadudu wakiwa tele juu ya mimea, kwa sababu wanafyonza utomvu, kama vidukari na nzi weupe. Lakini hawasambazi virusi kwa sababu hawaendi kutoka mmea mmoja kuelekea mmea mwingine, kama nzi weupe. Hata shida ya kuvu inayokua kwa mana siyo kubwa kuliko shida za vidukari na nzi weupe. Spishi kadhaa hutumika kwa udhibiti wa kibiolojia ili kuua mimea misumbufu, hususa mimea iliyowasili (au kuwasilishwa) kutoka bara jingine. Wadudu-gamba wenyewe huuawa na wadudu wengine, kama wadudu-kibibi, wadudu mabawa-vena, nyigu wa kidusia n.k. Pia kuna kuvu viuawadudu (entomopathogenic fungi) inayoambukiza wadudu hawa, kama Beauveria bassiana, Lecanicillium lecanii na Aschersonia marginata.

Wadudu-gamba ni wadogo. Kwa kawaida kiwiliwili chao kina urefu wa mm 1-5, lakini spishi za familia kadhaa ni kubwa zaidi, hata mpaka mm 35. Majike huchoza kifuniko cha nta ambacho kinaweza kikubwa kuliko mdudu mwenyewe. Kifuniko hiki kinafanana mara nyingi na gamba la samaki au reptilia (asili ya jina lao), lakini nta inaweza kutoka kama nyuzi nyeupe nyembamba, kama kwa Pseudococcidae (vidukari-sufu). Majike hawana mabawa na wale wa spishi nyingi hawana miguu. Kinyume na hawa madume ya spishi zote wana miguu, na pengine mabawa pia, kwa sababu wanaihitaji ili kutafuta majike. Kwa kweli majike huhifadhi umbo wa lava ambayo huitwa neotenia (neoteny). Kama madume wakiwa na mabawa yale ya nyuma yamepungua, mara nyingi mpaka alama tu.

Wakitoka mayai lava wana miguu. Wanatembea kidogo ili kufika mahali pazuri pa kufyonza. Kwa spishi kadhaa upepo hubeba lava kuelekea mmea mwingine. Mara nyingi sisimizi wanawapeleka lava kwenye mahali pazuri, k.m. chipukizi kipya. Katika spishi nyingi mara ya kwanza ambapo lava anaambua anapoteza miguu, isipokuwa madume.

Spishi zilizochaguliwa[hariri | hariri chanzo]

Picha[hariri | hariri chanzo]