Kunguni-bahari

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kunguni-bahari
Kunguni-bahari (Halobates sp.)
Kunguni-bahari (Halobates sp.)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye mwili wa pingili na miguu ya kuunga wasio na ugwe wa mgongo kama wadudu, nge, buibui)
Nusufaila: Hexapoda (Arithropodi wenye miguu sita)
(bila tabaka): Dicondylia (Wadudu walio na mandibula zenye condyle mbili)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Nusungeli: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda ya juu: Paraneoptera
Oda: Hemiptera
Haeckel, 1896
Nusuoda: Heteroptera
Oda ya chini: Gerromorpha
Familia ya juu: Gerroidea
Ngazi za chini

Familia 3 na nusufamilia 4 zina kunguni-bahari:

Kunguni-bahari ni wadudu wa jenasi mbalimbali za familia Gerridae, Hermatobatidae na Veliidae katika oda ya chini Gerromorpha ya oda Hemiptera na nusungeli Pterygota (wenye mabawa) ambao hutembea juu ya maji ya bahari na kujilisha kwa wadudu walioanguka majini au planktoni wanyama karibu na uso wa maji. Jenasi hizo ni Asclepios na Halobates (Halobatinae), Stenobates (Trepobatinae), Hermatobates (Hermatobatidae), Halovelia, Haloveloides, Ocheovelia na Xenobates (Haloveliinae) na Trochopus (Rhagoveliinae).

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Kunguni-bahari ni wadudu wadogo wenye mwili wa urefu wa hadi mm 6.5 na upana wa mm 3, na upana wa miguu hadi angalau mm 15, ingawa miguu ya spishi za Hermatobatidae na Veliidae ni mifupi zaidi. Wanakosa mabawa, wana vipapasio virefu, miguu mifupi ya mbele inayotumika kukamata mawindo (na, kwa madume, kwa kushikilia jike wakati wa kupandana), miguu mirefu ya kati inayotumika kwa kujisogea na miguu mifupi zaidi ya nyuma inayotumika kwa kujiendesha. Spishi za Veliidae zina "mabega" mapana (sehemu ya mbele ya pronoto) na fumbatio yao ni ndefu kulingana na spishi nyingine. Spishi za Hermatobatidae zina pronoto fupi sana na mesonoto na metanoto zimeungana.

Tunutu hufanana na toleo ndogo za mpevu. Jinsia ni sawa kiasi, isipokuwa kwamba madume ni wembamba kuliko majike na sehemu ya nyuma ya mwili imebadilishwa kuwa viungo vya uzazi, na majike wakiwa na mayai wanaweza kuwa na tumbo nono.

Msambao na makazi[hariri | hariri chanzo]

Kunguni-bahari hupatikana katika makazi ya bahari za tropiki na nusutropiki duniani kote. Kwa kawaida wanapendelea nyuzijoto ya 24- 28° C, wako nadra chini ya 20° C na huripotiwa mara chache tu katika maji ya chini ya 15° C. Spishi nyingi hukaa karibu na pwaa na mara nyingi huzuiliwa kwa funguvisiwa moja, huku nyingine zinaenea zaidi. Hutokea hasa karibu na mikoko au mimea ingine ya bahari.

Spishi tano za Halobates hukaa mbali na pwaa: H. micans, H. germanus, H. sericeus, H. splendens na H. sobrinus, ambazo nne za mwisho zinapatikana katika Bahari ya Hindi na/au Bahari ya Pasifiki. H. micans ina msambao unaozunguka dunia na kutokea mbali na pwaa katika bahari za nyuzijoto ya juu duniani kote kati ya karibu na 40° kaskazini mpaka 40° kusini na ndiyo pekee inayopatikana katika Bahari ya Atlantiki pamoja na Bahari ya Karibi.

Kwa ujumla kunguni-bahari hutokea hapa na hapo tu, lakini wanapopatikana wanaweza kuwa wengi sana. Wakati wa kaguzi za kisayansi ambapo vyandarua vinavutwa kwa kasi kwenye uso wa maji, hukamatwa kwa zaidi ya 60% ya mivuto (chini kwa mivuto inayoenda polepole, labda kwa sababu ya uwezo wao wa kuiepuka). Utafiti unaonyesha kuwa misongamano ya maeneo inaweza kuwa juu kama mdudu 1 kwa 19 kwa spishi za bahari wazi na wadudu 120 kwa m² katika makundi ya kuzaa ya spishi karibu na pwaa.

Hermatobatidae hutokea kwenye miamba ya matumbawe. Wakati wa maji kupwa hutembea juu ya uso wa maji na wakati wa maji kujaa hubaki chini ya maji ndani ya nyufa.

Spishi za Afrika ya Mashariki[hariri | hariri chanzo]

  • Gerridae: Halobatinae
    • Halobates alluaudi
    • Halobates flaviventris
    • Halobates germanus
    • Halobates hayanus
    • Halobates micans
    • Halobates poseidon
  • Hermatobatidae
    • Hermatobates djiboutensis
  • Veliidae: Haloveliinae
    • Halovelia amphibia
    • Halovelia poissoni
    • Halovelia seychellensis