Maji kujaa na kupwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Maji kupwa)
Bandari ya Alma katika Kanada kwenye pwani la Atlantiki wakati wa maji kujaa na kupwa.
Kisiwa cha Saint Michaels Mount nchini Uingereza hufikiwa kwa miguu kwenye nchi kavu wakati wa maji kupwa

Maji kujaa na kupwa ni mabadiliko ya uwiano wa bahari unaopanda na kushuka kila siku. "Maji kujaa" ni hali ya juu na "maji kupwa" ni hali ya chini ya maji ya bahari. Tofauti kati ya hali hizi inaweza kufikia hadi mita kadhaa.

Mabadiliko ya maji kujaa na kupwa hutokea mara mbili kila siku yaani kila mahali huwa na maji kujaa mara mbili na maji kupwa mara mbili kila siku.

Kanda la kujaa na kupwa[hariri | hariri chanzo]

Kwenye pwani ambako mtelemko wa nchi si mkali kuna kanda ya eneo linalobadilika kila siku kuwa nchi kavu kwa masaa kadhaa halafu tena bahari. Karibu na Mombasa kuna kanda la pwani ambako bahari inarudi kila siku kwa upana wa kilomita mbili na wakati wa maji kupwa inawezekana kutembea kwa kilomita hizi mbili ambako baada ya masaa kadhaa bahari itarudi.

Katika nchi nyingine kanda hili linaweza kufikia hadi ya upana wa kilomita 40 kwa mfano kwenye pwani la Bahari ya Kaskazini upande wa Ujerumani na Uholanzi.

Kanda hili ni muhimu kwa ajili ya ekolojia ya bahari maana vidudu vingi ambavyo ni lishe ya samaki na ndege wanaishi na kuzaa hapa.

Visiwa vilivyoko katika kanda hili vinafikiwa kwa miguu au hata kwa gari wakati wa maji kupwa lakini kwa boti wakati wa maji kujaa.

Sababu za maji kujaa na kupwa[hariri | hariri chanzo]

Mabadiliko yanasabishwa na nguvu ya graviti ya mwezi na jua inayovuta dunia yetu. Sehemu ya dunia iliyo tazama mwezi ni karibu zaidi kwake na inaathiriwa zaidi na nguvu ya graviti. Maji ya bahari ni gimba moja kubwa la kiowevu na hivyo sehemu yake iliyoathiriwa zaidi inavutwa kuelekea mwezini. Ilhali mwezi unazunguka dunia katika muda wa takriban siku moja (halihalisi kidogo zaidi ya siku moja ya hesabu yetu) kuna kilele cha maji yanayovutwa kuelekea mwezini. Mzunguko wa mwezi ni masaa 24 na dakika 50 kwa hiyo saa ya maji kupaa na kupwa hubadilika hizi dakika 50 kila siku.

Kuna athira nyingine zinazovuta uso wa maji ya bahari pia; hii ni hasa kani nje kutokana na mzunguko wa dunia kwenye mhimili wake na graviti ya jua. Kila mwezi wakati jua iko nyuma ya mwezi kwenye mstari nyoofu nguvu za graviti hizi mbili zinaungana na kusababisha bamvua inayomaanisha maji kujaa sana yaani uso wa maji wa bahari hupanda juu zaidi kuliko kawaida.

Kimsingi mabadiliko ya graviti ya mwezi huathiri kila kitu duniani na pia magimba madogo kama mto, bwawa na maji katika bakuli. Lakini kama gimba la maji ni dogo tofauti hazionekani ingawa zinapimika kwa mitambo.


Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Kalenda za maji kujaa na kupwa[hariri | hariri chanzo]