Konyeza

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Konyeza
Konyeza madoa (Mastigias papua)
Konyeza madoa (Mastigias papua)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Nusuhimaya: Eumetazoa
Faila: Cnidaria (Wanyama-upupu)
Nusufaila: Medusozoa (Konyeza)
Ngazi za chini

Ngeli 4:

Konyeza ni wanyama wa bahari au wa maji baridi. Wanaainishwa katika nusufaila Medusozoa wa faila Cnidaria (wanyama-upupu). Wana minyiri mirefu au mifupi yenye seli zinazochoma ngozi na zinazoweza kupooza au hata kuua mawinda madogo. Hutumika kwa kukamata samaki wadogo na wanyama wengine wa bahari.

Kwa kawaida konyeza ni wanyama wa bahari ambao huogelea vihuru. Mwili wao ni kama kuba lenye umbo la bakuli na chini yake kuna minyiri inayojiburura nyuma. Konyeza kama hao huitwa medusa pia kwa Kiingereza, ingawa wachache wametiwa nanga kwa kikonyo kwenye sakafu ya bahari badala ya kuwa sabili. Kuba linaweza kudundadunda ili kujisukuma na kuogelea kwa ufanisi. Konyeza wana mzunguko tata wa maisha. Medusa kwa kawaida ni awamu ya kijinsia, ambayo hutoa lava wa planula wanaotawanyika sana na kuingia katika awamu ya chechevule (isiyo na jinsia) ambayo inakaa mahali pamoja mpaka kufikia ukomavu wa kijinsia.

Konyeza hupatikana duniani kote, kutoka maji ya juu hadi kwenye kina kirefu cha bahari. Scyphozoa ("konyeza sahihi") hutokea baharini tu, lakini baadhi ya Hydrozoa wenye muonekano kama hao huishi katika maji baridi. Konyeza wakubwa, wenye rangirangi mara nyingi, wapo kwa kawaida katika maeneo ya pwani duniani kote. Medusa za spishi nyingi hukua haraka na hukomaa ndani ya miezi michache kisha hufa mara tu baada ya kuzaliana. Kinyume chake, awamu ya chechevule, iliyoshikamana na sakafu ya bahari, inaweza kuishi muda mrefu zaidi. Konyeza wamekuwepo kwa angalau miaka milioni 500, na labda miaka milioni 700 au zaidi, ambayo inawafanya kuwa kikundi cha wanyama wa ogani nyingi cha zamani zaidi.

Ngeli[hariri | hariri chanzo]

  • Cubozoa (konyeza-sanduku): Wana kuba lenye umbo la sanduku lililoviringa na velario (kiwambo kinachotumika katika kuogelea) iliyoambatanishwa ndani ya kando ya kuba na inayowasaidia kuogelea haraka zaidi. Konyeza-sanduku wamehusishwa labda karibu zaidi na konyeza wa Scyphozoa kuliko mojawapo ya ngeli hizo na Hydrozoa.
  • Hydrozoa (konyeza wadogo): Medusa yao ina ulinganifu wa nusukipenyo nne kama Scyphozoa. Takriban spishi zote zina velario. Hazina mikono ya kinywa. Zinajulikana kwa kukosekana kwa seli kwenye mesoglea. Hydrozoa huonyesha utofauti mkubwa wa mtindo wa maisha. Spishi nyingine hutunza umbo la chechevule kwa maisha yao yote na haziumbi medusa kabisa (kama Hydra ambaye kwa hivyo hazingatiwi kama konyeza) na chache zina awamu ya medusa tu na hazina awamu ya chechevule.
  • Scyphozoa (konyeza sahihi): Wana ulinganifu wa nusukipenyo nne. Takriban wote wana minyiri karibu na ukingo wa nje wa kuba, lililo na umbo la bakuli, na minyiri mirefu (minne kwa kawaida) kuzunguka mdomo katikati ya chini ya kuba.
  • Staurozoa (konyeza-kikonyo): Sifa yao ni aina ya medusa ambayo kwa ujumla imefungwa kwenye sakafu na inaelekezwa juu chini yenye kikonyo kinachoibuka kutoka kwa kilele cha kuba, ambacho kinaambatana na sakafu. Angalau baadhi ya Staurozoa wana awamu ya chechevule ambayo hufuatana na awamu ya medusa ya mzunguko wa maisha.

Picha[hariri | hariri chanzo]