Kisaga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kisaga
Kisaga madoa-manne au wa kunde Callosobruchus maculatus
Kisaga madoa-manne au wa kunde Callosobruchus maculatus
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Faila: Arthropoda
Nusufaila: Hexapoda
Ngeli: Insecta
Ngeli ya chini: Pterygota
Oda: Coleoptera
Nusuoda: Polyphaga
Familia ya juu: Chrysomeloidea
Familia: Chrysomelidae
Nusufamilia: Bruchinae
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Makabila 6:

Visaga ni mbawakawa wa nusufamilia Bruchinae katika familia Chrysomelidae. Wadudu hao hujilisha kwa mbegu za spishi za Fabaceae (k.m. maharagwe) na za familia nyingine kadhaa. Hupitia takriban maisha yao yote katika mbegu moja. Familia hii inapatikana duniani kote na ina spishi zaidi ya 4000. Tabia zao zinafanana na zile za vidungadunga (Curculionidae) na kwa hivyo moja ya majina yao kwa Kiingereza ni bean weevils.

Kwa ujumla visaga ni wagumu wenye umbo la duaradufu na vichwa vyao vidogo vimeinamishwa chini. Urefu wao unaanzia mm 1 kufikia mm 22 kwa spishi fulani za kitropiki. Rangi kawaida ni nyeusi na/au kahawia na mara nyingi wana ruwaza ya madoa. Ingawa mandibuli zao zinaweza kurefuka, hawana pua ndefu iliyo sifa ya vidungadunga wa kweli. Mabawa ya mbele ni fupi na hayafikii kabisa ncha ya fumbatio.

Wapevu hutaga mayai juu ya mbegu, kisha mabuu hutafuna tundu la kuingilia mbegu. Wanapokuwa tayari kuwa mabundo, kwa kawaida mabuu hukatia mpevu shimo la kutoka, kisha kurudi kwenye chumba chao cha kujilisha. Visaga wapevu huwa na tabia ya kujifanya kama wamekufa na kuanguka kutoka kwa mmea wakisumbuliwa.

Vidusiwa huwa mimea ya jamii ya kunde (Fabaceae), lakini kuna spishi pia zinazopatikana katika Convolvulaceae, Arecaceae na Malvaceae, na spishi kadhaa huchukuliwa kuwa wasumbufu, k.m. kisaga wa kunde na kisaga wa karanga.

Spishi nyingi ni asili ya Afrika ya Mashariki, k.m. zile zinazoshambulia mbegu za migunga, lakini nyingine zimewasilishwa, kama kisaga wa azuki na kisaga wa njegere.

Picha[hariri | hariri chanzo]