Kandidiasisi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Candidiasis
Mwainisho na taarifa za nje
SpecialtyInfectious diseases, dermatology Edit this on Wikidata
ICD-10B37.
ICD-9112
DiseasesDB1929
MedlinePlus001511
eMedicinemed/264 emerg/76 ped/312 derm/67
MeSHD002177

Kandidiasisi ni maambukizi ya kuvu yanayotokana na aina yoyote ya Kandida (aina ya chachu).[1]

Maambukizi hayo yanapoathiri kinywa, kwa kawaida huitwa uotokuvu (au Kandidiasisi ya kinywa).[1] Ishara na dalili zinajumuisha madoa meupe kwenye ulimi au sehemu nyingine za kinywa na koo.[2] Dalili nyingine zinaweza kujumuisha maumivu na matatizo wakati wa kumeza.[2]

Maambukizi hayo yanapoathiri uke kwa kawaida huitwa maambukizi ya chachu.[1] Ishara na dalili zinajumuisha kujikuna kwenye uke, mwasho na wakati mwingine mchozo mweupe "unaofanana na jibini" kutoka ukeni.[3] Kwa nadra uume unaweza kuathirika na kusababisha kujikuna.[2]

Kwa nadra sana maambukizi hayo yanaweza kuwa vamizi na kuenea kwenye mwili wote na kusababisha homa pamoja na dalili kulingana na sehemu za mwili zilizoathiriwa.[4]

Kisababishi[hariri | hariri chanzo]

Zaidi ya aina 20 za Kandida zinaweza kusababisha maambukizi huku Candida albicans ikitokea mara nyingi zaidi.[1] Maambukizi ya kinywa hutokea mara nyingi zaidi kwa watoto wenye umri wa chini ya mwezi mmoja, wazee na walio na mfumo dhaifu wa kingamaradhi. Hali zinazosababisha mifumo dhaifu ya mwili zinajumuisha UKIMWI, upandikizaji wa ogani, kisukari na matumizi ya kotikosteroidi.Hatari nyingine zinajumuisha meno bandia na kutumia antibiotiki.[5]

Maambukizi ya uke hutokea mara nyingi katika ujauzito, kwa wenye mfumo dhaifu wa kingamwili na kufuatia matumizi ya antibiotiki.[6]

Hatari ya ueneaji mkubwa wa ugonjwa huu unajumuisha kuwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi, kufuatia upasuaji, watoto wenye uzito mdogo wa kuzaliwa na wenye mifumo dhaifu ya kingamwili.[7]

Kinga na tiba[hariri | hariri chanzo]

Juhudi za kuzuia maambukizi ya mdomoni zinajumuisha matumizi ya chlorhexidine ya kusafisha kinywa kwa wale wenye utendakazi dhaifu wa kingamwili na kuosha mdomo baada ya matumizi ya steroidi za kupumua.[8] Katika wanawake wanaoambukizwa mara kwa mara ukeni, probiotiki zinaweza kuwa bora.[6] Kwa maambukizi ya kinywa, matibabu ya kutumia clotrimazole au nystatin ya kupaka kwa kawaida huwa mwafaka. Fluconazole, itraconazole, au amphotericin B ya kumeza au inayodungwa mishipani inaweza kutumika ikiwa dawa hizo hazitibu maambukizi.[8] Baadhi ya dawa za kuvu za eneo maalumu zinaweza kutumika kutibu maambukizi ya ukeni ikijumuisha clotrimazole.[9] Kwa watu wenye maambukizi yaliyoenea sana, amphotericin B ya kudungwa mishipani hutumika mara nyingi kwa wiki kadhaa.[10] Kwa makundi fulani vya wtau wenye hatari ya juu zaidi, dawa za kuvu zinaweza kutumika kama kinga.[7]

Epidemiolojia[hariri | hariri chanzo]

Maambukizi ya kinywa hutokea katika takriban asilimia 6 ya watoto wa chini ya umri wa mwezi mmoja. Takriban asilimia 20 ya wanaofanyiwa kemotherapi ya saratani na asilimia 20 ya wale wenye UKIMWI pia hupata ugonjwa huo.[11] Takriban robo-tatu ya wanawake hupata angalau maambukizi ya chachu wakati fulani katika maisha yao.[12] Ueneaji sana wa ugonjwa huu hautokei mara nyingi isipokuwa kwa watu wenye vipengele vya hatari.[13] Magonjwa haya pia hujulikana kama maambukizi ya kuvu, moniliaisisi, na oidiomycosis.[14]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 1. 1.0 1.1 1.2 1.3 Candidiasis (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 2. 2.0 2.1 2.2 Symptoms of Oral Candidiasis (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 3. Symptoms of Genital / Vulvovaginal Candidiasis (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 4. Symptoms of Invasive Candidiasis (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 5. Risk & Prevention (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 6. 6.0 6.1 People at Risk for Genital / Vulvovaginal Candidiasis (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 7. 7.0 7.1 People at Risk for Invasive Candidiasis (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 8. 8.0 8.1 Treatment & Outcomes of Oral Candidiasis (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 9. Treatment & Outcomes of Genital / Vulvovaginal Candidiasis (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 10. Treatment & Outcomes of Invasive Candidiasis (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 11. Oral Candidiasis Statistics (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 12. Genital / vulvovaginal candidiasis (VVC) (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 13. Invasive Candidiasis Statistics (February 13, 2014). Iliwekwa mnamo 28 December 2014.
 14. James, William D.; Berger, Timothy G.; et al. (2006). Andrews' Diseases of the Skin: clinical Dermatology. Saunders Elsevier, 308–311. ISBN 0-7216-2921-0.