Joatham Mporogoma Mwijage Kamala

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Joatham Mporogoma Mwijage Kamala (16 Mei 1946 - 18 Juni 1998) alikuwa mwanasiasa, kiongozi na mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Alikuwa na kipawa asilia cha uongozi na utashi mzuri kiasi cha kumgusa Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere haswa kwa imani yake kubwa juu ya misingi ya ujamaa. Amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi nchini.

Mpenzi mkubwa wa kusoma vitabu, haswa vitabu vya siasa, uongozi na uchumi. Joatham hukumbukwa kwa utashi wake mkubwa kwenye masuala ya siasa na wengi humuita mwanasiasa aliyebobea ambaye hakupata kuwa maarufu ndani na nje ya mipaka ya nchi yake.

Joatham alizaliwa katika kijiji cha Bwemera/Bwoki, kata ya Bugandika, wilaya ya Missenyi (Bukoba Vijijini kwa wakati huo) mkoani Kagera.

Alianza elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Bugandika kutoka darasa la kwanza mpaka la nne, aliendelea na darasa la tano mpaka la nane katika shule ya msingi Kigarama. Baada ya elimu ya shule ya msingi, alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Kahororo ambapo alisoma kutoka kidato cha kwanza mpaka cha nne. Baada ya hapo alijiunga na elimu ya juu ya sekondari katika shule ya sekondari ya Ihungo, Kagera ambapo alihitimu kidato cha sita.

Baada ya elimu ya sekondari, alifanikiwa kuendelea na elimu ya chuo kikuu, katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam na kupata Shahada ya Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma, huko alijengeka kisiasa na kushiriki kwenye harakati mbalimbali pamoja na wanasiasa wengine kama Pius Ng'wandu, Adam Marwa, Yoweri Museveni, Jenerali Ulimwengu, Sebastian Kinyondo na wengine wengi.

Joatham alifariki tarehe 18 Juni 1998 kwa tatizo la kansa ya shavu. Ameacha mjane Florence Kamala na watoto Emmanuel na Peter Kamala.

Viungo vya nnje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Joatham Mporogoma Mwijage Kamala kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.