Nenda kwa yaliyomo

Majarra

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Galaksi)
Majarra ya Mara yenye na. M 31 na majarra mbili ndogo za kando M 32 na M 110

Majarra (pia galaksi, kutoka Kiingereza galaxy) ni kundi la nyota nyingi, vumbi la angani, na maada ya giza zinazoshikamana pamoja katika anga-nje kutokana na mvutano wao. Nyota hupatikana angani katika makundi kama mawingu makubwa sana.

Kuna majarra nyingi sana ulimwenguni. Kwa wastani kila majarra imekadiriwa kuwa na nyota kama bilioni 100 lakini kuna majarra kubwa na ndogo.

Majarra yetu, ikiwemo Mfumo wa Jua letu, imekadiriwa kuwa na nyota zaidi ya bilioni 300 (3·1011). Sehemu ya nyota hizi zinaonekana kama kanda la kung'aa kwenye anga la usiku linalojulikana kwa rangi yake kama Njia Nyeupe. Umbo lake linafanana na kisahani kikiwa na kipenyo cha miakanuru 100,000 na kikiwa na unene wa miakanuru 3,000.

Kwenye kitovu cha majarra, mvutano ni mkubwa sana kiasi cha kwamba majarra nyingi huaminiwa kuwa na shimo jeusi kituvoni[1].

Majarra zilizo karibu angani zinaitwa Mawingu ya Magellan ambayo ni majarra mbili ndogo zilizopo kwenye umbali wa miakanuru 170,000 na 200,000. Majarra kubwa ya jirani ni Mara na ina umbali wa miakanuru milioni 2.5.

Idadi kamili ya majarra zote angani haijulikani. Kuna makadirio ya kwamba idadi ya majarra zinazoweza kuangaliwa kwa vyombo vinavyopatikana ni mabilioni. Hadi sasa sehemu ndogo tu imehesabiwa lakini mara kwa mara majarra mpya zinatambuliwa kwa njia ya darubini au vyombo vya angani.

Majarra zinazojulikana zimepewa namba katika orodha ya kimataifa na wataalamu wa anga.

Majarra kati yao hujumuika pia zikiathiriana kwa njia ya graviti yao na kuzunguka kitovu cha graviti cha pamoja. Majarra hadi 50 zinazoshikamana katika kipenyo cha miakanuru milioni 10 huitwa kundi la majarra (ing. galaxy group). Kuna pia majarra mamia hadi maelfu kadhaa zinazoshikamana na hii huitwa fundo la majarra (ing. galaxy cluster) linaweza kuwa na kipenyo cha miakanuru milioni 10 - 20.

Asili ya neno

[hariri | hariri chanzo]

Neno majarra lilijulikana tangu karne nyingi kati ya mabaharia waswahili.[2] Lina asili ya kiarabu, na kwanza lilihusu Njia Nyeupe tu. Baada ya kugunduliwa kuwa Njia Nyeupe ni mojawapo ya majarra nyingi, maneno majarra na galaksi yalianza kumaanisha majarra yoyote. Neno galaksi ni jipya zaidi, kutoka Kilatini (kwa njia ya Kiingereza), yenye maana ya “njia ya maziwa".[3]

  1. Astronomers Get Closest Look Yet At Milky Way's Mysterious Core, tovuti ya National Radio Astronomy Observatory, Marekani, iliangaliwa Machi 2019
  2. Kuhusu asili ya neno: Jan Knappert, The Swahili names of stars, planets and constellations; makala katika jarida la The Indian Ocean Review, Perth, Australia September 1993, uk. 6
  3. Maziwa (mfano maziwa ya ng'ombe) kwa Kigiriki huitwa "γάλα gala" na hapo asili ya jina "galaksi".