Dunia Uwanja wa Fujo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Dunia Uwanja wa Fujo ni riwaya iliyoandikwa na Euphrase Kezilahabi mwaka wa 1975. Ni riwaya ambayo inasawili maisha ya wanadamu hususani waishio Afrika Mashariki, hasa hasa katika nchi ya Tanzania.

“Dunia Uwanja wa Fujo” inaelezea jinsi maisha yaliyopo duniani ni sawasawa na fujo, kwani kila mtu anayekuja duniani huleta fujo zake na baadaye kutoweka. Mwandishi anaelezea kwamba kila mtu anafanya fujo zake na kusababisha matatizo mbalimbali katika jamii yake kama vile mauaji, ukabila, umalaya, uchawi, ubakaji, ulevi wa kupindukia n.k. Hivyo basi mwandishi anaamini kwamba katika dunia kila mtu anakuja na fujo zake na kutoweka. Kwa mfano, mhusika Tumaini katika riwaya hii ameleta fujo zake kama vile umalaya, mauaji na mengine mengi na baadaye kutoweka.

Mbinu za kifani katika riwaya hii[hariri | hariri chanzo]

Fani za kijadi ndizo zilizosababisha riwaya izalike. "Dunia ni Uwanja wa Fujo” ni mojawapo ya riwaya zilizotokana na fani ya kijadi ambayo ni sira. Sira ni fani ya kijadi ambayo hujumuisha wasifu na tawasifu, yaani habari za maisha ya watu; kwa mfano mwandishi E. Kezilahabi katika riwaya yake hii amejaribu kumuonyesha mhusika Tumaini maisha aliyokuwa akiishi.

Mfano uk. 11, “Alibatizwa, alikuwa mtoto wa mwalimu Kapinga……”. Vile vile Tumaini alikuwa mlevi, malaya, mfano uk. 73 “mwenyewe kaingiaaaa, tajiri wetuuu”. Hivyo basi riwaya hii inasadifu kuwa ni mojawapo ya riwaya za fani za kijadi ambayo hujumuisha wasifu wa mhusika Tumaini toka mwanzo hadi mwisho wa maisha yake.

Muundo[hariri | hariri chanzo]

Muundo ni namna visa na matukio hufuatana kwa mtiririko. Hivyo tunaweza kusema pia muundo ni mfuatano wa masimulizi katika kazi ya fasihi. Katika riwaya hii mwandishi ametumia muundo wa rejea pamoja na changamano.

Katika muundo wa rejea mwandishi anaanza kwa kuonyesha maisha ya Dennis pale alipowapokea wageni akina Tumaini na pia kurejelea kwa kuonyesha maisha ya Dennis pale tangu utoto wake (uk.66).

Pia mwandishi ametumia muundo changamano au rukia ambapo visa vinakuwa vinarukiana: hii inajidhihirisha sehemu ya kwanza ambapo anatuonyesha nyumbani kwa Kasala ambaye anaishi kijijini Bugolola; kisa hakijaisha tunaona pia kisa cha Tumaini (uk.11) ambapo mwandishi anaonyesha alivyozaliwa na kubatizwa.

Mwandishi pia ameigawa kazi yake katika sehemu kuu tatu na kila sehemu ameipa namba ili kusadifu yaliyomo katika kazi yake ya riwaya.

Katika sehemu ya kwanza E. Kezilahabi amewachora wahusika kwa kuonyesha adha na matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii ya Bugolola, kwa mfano ushirikina, umalaya na ulevi: mambo hayo yote ameyaonyesha katika namba 1, 2, 3, 4, 5.

Pia katika sehemu ya pili tunamuona Tumaini akiwashawishi akina John na Anastasia kwenda nao mjini Dar es Salaam, lakini inakomea Shinyanga baada ya kukutana na dada ya Dennis, kitu kilichompelekea Tumaini na wenziwe kuanza maisha mapya mjini Shinyanga. Lakini katika maisha hayo Tumaini na John wanakuwa wenye kupenda pombe na ansa, kitu kilichopelekea kufilisika kwa Tumaini.

Sehemu ya tatu inaonyesha baada ya Tumaini kuamua kufanya kazi alivyopata mafanikio makubwa, lakini mafanikio hayo yanaingia doa baada ya serikali kuingiza mfumo wa ujamaa, kitu kilichopelekea mali zote za Tumaini. Mwisho kabisa tunamuona akichukua jukumu la kumuua mkuu wa wilaya ya Shinyanga ambaye ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa shughuli za ujamaa; kitendo hicho kinapelekea hukumu ya kifo kwa Tumaini (namba 12, 13, 14).

Msuko[hariri | hariri chanzo]

Mbunda Msokile (1992:206) anasema kuwa msuko ni mtiririko au mfuatano wa matukio yanayosimuliwa toka mwanzo mpaka mwisho. Hali hii huandamana na uchaguzi au mpangilio na ufundi wa kusimulia matukio yaliyoungwa vyema katika kazi ya sanaa ya kubuni itumiayo lugha. Lakini ufafanuzi huo si tofauti na ule unaofafanua muundo, kwani nao ni mtiririko wa matukio jinsi yanavyopangwa kiufundi kutoka mwanzo wa simulizi hadi mwisho.

Pesa za urithi alizoachiwa Tuamini pamoja na malezi mabaya kutoka kwa wazazi wake ndizo zinazokuwa usababishi wa utovu wa nidhamu wa Tumaini katika kijiji chao cha Bugolola, mambo hayo ya utovu wa nidhamu ni kama vile: kuwa mlevi, malaya, kutofanya kazi, pia kutumia ovyo mali alizoachiwa. Mfano katika uk.15 “tunamuona mama yake Tumaini akimkabithi Tumaini funguo ya kufungua sanduku la marehemu baba yake ambalo lilikuwa limebeba urithi wake.

Tumaini baada ya kupewa pesa za urithi hapa ndio tunaona mshitikizo kwani pesa za urithi zilimsababisha kuamua kuacha shule na kuanza kuzitumia pesa hizo ovyo kama vile ukahaba, umalaya, ulevi na mengineyo (uk. 16, 17).

Pia katika riwaya hii msuko unaendelea kuonekana pale ambapo Tumaini, John na Anastazia walipofika Mwanza na kufanya maamuzi ya kuelekea Dar es Salaam baada ya kuona eneo la Mwanza halitawafaa kwa kuanza maisha mapya kwani palikuwa karibu mno na kijini kwao; sababu nyingine ilikuwa akina Tumaini hawakuondoka kijijini kwa wema. Safari yao ya kuelekea Dar es Saalam inafikia kikomo pale ambapo walipofika Shinyanga na kukutana na Dennis ambaye aliwasihi wasitishe safari yao ili aambatane nao wakapajue kwake na kumpasha habari juu ya mambo yaliyokuwa yakiendelea kijijini kwao Mugele (uk. 55-72).

Hali ya kuahirisha safari ya kuelekea Shinyanga ilisababisha akina Tumaini kuanza maisha mapya mjini Shinyanga na kwa vile Tumaini alikuwa na pesa nyingi za urithi alianza maisha ya anasa; hali hiyo ilipelekea Tumaini kuishiwa kipato na kutafuta kazi ya ulinzi ambayo alisaidiwa na Dennis katika kuipata (uk.114). Lakini pindi alipoanza kazi hiyo alijikuta akichukiwa na watu mbalimbali kutokana na kazi yake ya kuchunguza watu siri zao na kuziripotisha serikalini. Kazi hiyo ilisababisha hata baadhi ya watu kumkimbia Tumaini mahali alipotia mguu wake. Mfano pindi alipofika baa wateja walikunywa haraka haraka na kukimbia hali hiyo ilisababisha wenye biashara zao kumchukia Tumaini na ikafikia hatua ya kumtafutia Tumaini wajambazi wa kumuadabisha Tumaini.

Baada ya Tumaini kutafutiwa majambazi na kuwa amehadabishwa hali hiyo inatumika kama usababishi wa Tumaini kuichukia kazi yake na kuamua kutafuta kazi nyingine ya kujiajili yeye mwenyewe, kazi yenyewe ilikuwa ni kazi ya ukulima japo alianza kama mkulima mdogo lakini baadae akajikuta akipata maendeleo makubwa katika kazi yake mfano alinunua shamba kubwa na alitumia Trekta katika shuguli zake za kilimo. Lakini ng'ombe wa maskini hazai: serikali ikapitisha mfumo wa ujamaa ambapo ilidai hakuna umiliki binafsi na mali zote ni za ni za umma hali hiyo ilisababisha kumuingiza tumaini matatani kwa hakukubaliana na hali hiyo na kupelekea kufanya tukio la mauaji ambapo alimuua mkuu wa wilaya ambaye ndiye alikuwa ni kiongozi wa ujamaa (uk. 114). Kitendo hicho kilitumika kama usababishi kwa Tumaini kuwekwa chini ulinzi wa polisi na hatimaye kuhukumiwa kunyongwa (uk. 131).

Mtindo[hariri | hariri chanzo]

Mtindo ni jinsi msanii anavyotumia ufundi, umahiri na hisia zake katika kutenda au kueleza jambo fulani. Katika riyawa hii kuna mitindo mbalimbali ambayo mwandishi ameitumia; ni kama vile:

 • Monolojia: Masimulizi kwa kiasi kikubwa mwandishi ametumia lugha ya masimulizi katika kuelezea visa/matukio, sifa na tabia za wahusika katika kuikamilisha kazi yake.
 • Barua: Mwandishi pia ametumia mtindo wa barua, m kwa mfano katika uk. 68 mwandishi ametumia mtindo wa barua tunaona Vera akimwandikia Denis barua, pia uk. 105 mwandishi ametumia mtindo huu wa barua, Tunamuona Tumaini akimuandikia Joku barua vilevile katika uk 110 “tunamuona Denis akipokea barua kutoka kwa Vera”, uk. 123 “bibi Kimalio alimuandikia barua Denis”.
 • Hotuba: Mwandishi katika kazi yake hii ya riwaya ya “Dunia ni uwanja wa fujo” ametumia mtindo wa hotuba. Kwa mfano katika uk. 115 - 117 mtindo wa hotuba umetumika na hotuba ilikuwa ya kusisitiza Azimio la Arusha ambalo lililenga hatua ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo ilitaka watu wote wamiliki mali na uchumi kwa pamoja bila kujali mwenye nacho na asiye ncho.
 • Nyimbo: Ni mtindo mmoja wapo aliotumia mwandishi aliotumia mwandishi wa riwa hii. Kwa mfano uk. 10 mwandishi ametumia wimbo ulioimbwa na mpiga zeze.
 • “Wanaume Bugolola
 • Mchana hawajambo
 • Usiku hawana tendo”

Mwandishi pia ametumia wimbo kwa mtindo wa shairi katika kazi yake hii kwa mfano katika uk. 13 tunona Tumaini akiandika shairi ambalo lilisomwa na mwalimu darasani kama ifuatavyo.

 • “Yeh,
 • Nitaoa msichana
 • Msichana mwenye shingo
 • Shingo shingo kama la mbuni..”

Mwandishi ametumia wimbo wa maungunzo, mwandishi katika mtindo wa mazungumzo ametumia nafsi zote tatu yaani nafsi ya nafsi ya kwanza, nafsi ya pili, nafsi ya tatu katika kazi yake hii, kwa mfano. - Uk. 13 tuaona nafsi ya kwanza umoja “nitaoa msichana” na - uk. 27 tunaona nafsi ya kwanza wingi. “hata sisi,” pia - Pia nafsi ya pili katika riwaya hii imetumika kwa mfano uk. 36 “…wewe kasala Pia nafsi ya tatu katika riwaya hii tunaona katika uk. 35 “….yeye alisema kwa machozi

Matumizi ya lugha[hariri | hariri chanzo]

Lugha ni muhimu katika kazi ya fasihi. Pasipo lugha hakuna riwaya. Mwandishi wa riwaya hii ametumia lugha sanifu iliyosheheni taswira, mkoto, misemo, methali, tamathali za semi, nahau, lugha za kigeni, na mbinu zingine za kisanaa kama ifuatavyo:

Lugha sanifu ni mojawapo ya lugha ambayo mwandishi ametumia toka mwanzo hadi mwisho. Lugha iliyotumika ni Kiswahili sanifu.

Pia mwandishi ametumia lugha isiyo sanifu kwa kiasi kidogo. Kwa mfano katika uk. 5, Mwandishi anasema “…. Batoto bamenisosondogorasondogola na chichwa, bengine bamenikorokorakorokora na kucha”. Uk. 30 “…. Vizuri walilia kwa sauti za kutisha, yuhuu. Huba, huba, huba. Wotha ,wotha”

Lugha ya kigeni imetumiwa na E. Kezilahabi katika riwaya yake hii. Lugha ya kigeni aliyotumia ni Kiingereza kwa mfano: - “Africans royal bar” (uk. 62). - “Snow cap” (uk. 62) - “You are too optimistic about life and you are too pessimistic” (uk. 65, 66). - “Welcome back” (uk. 88). - “Security (uk. 89 na 90).

Mchanganyo ndimi: Ni matumizi ya lugha ambayo mwandishi ametumia katika riwaya hii. Mchanganyo ndimu ni ile hali mtu kuongea kwa kutumia lugha zaidi ya mbili. - Mfano: “mimi …naturalist” (uk. 41).

Lugha za matusi: mbinu nyingine zilizotumiwa na mwandishi katika riwaya hii ni lugha za matusi kwa mfano: - “Washenzini ninyi”. (uk. 12). - “Kumbe bado washenzi” (uk. 50). - “Yule mshenzi amekwenda” (uk. 93) - “Nimemfukuza mbwa tumaini (uk. 109). - “Kwanza wewe bwege. (uk. 121). - “…. Alidakia na kusema unyokonyoko (uk. 122).

Tamathali za semi: Ni maneno yanayotumiwa yanayotumiwa na wasanii ili kutia nguvu katika kazi hiyo. Hivyo tamathali za semi zinazotumika katika riwaya hii ni pamoja na:

Tasbihiha/Mshabaha: Ni maneno ambayo hutumia kulinganisha kitu na kitu kingine kwa kutumia maneno kama vile “mithili, sawa, kama” mfano: - “Miaka ni kama kunguni” (uk. 6). - “Baba yako atakuwa mkali kama samba” (uk. 6). - “Mapenzi ni kama mpunga mototo wangu” (uk. 14). - “Lakini mimi ninaumwa ninaumwa kama panya.” (uk. 17). - “Si tutakufa kama mbwa” (uk. 19). - “Kukaa kama watakatifu” (uk. 19). - “Aliyekunyata nyumbani kwake kwa uoga kama panya aliyesikia mlio wa paka”. (uk. 130).

Sitiari: Ni tamathali za semi ambazo ulinganisha vitu vizuri kwa kutumia viunganishi au linganishi. Mfano “ni”: - “Watoto wote yatima ni watoto wangu” (uk. 15). - “Huyo ni baba yako” (uk. 12). - “Ujamaa ni mzuri” (uk. 112).

Takriri: Ni tamathali za semi ambayo neno hujirudiarudia kwa lengo la kusisitiza jambo fulani. Takriri ni matumizi ya lugha ambayo msanii ametumia katika riwaya hii, mfano wa takriri: - “Mauti, mauti”. (uk. 17). - “He! Hee! Hee!” (uk. 18) - “Kasala, kasala, ngoja nije!”(uk. 22) - “Yuhu! Yuhu!” (uk. 27) - “Haa! Haa! Haa! (uk. 42) - “Msiue, msiue!” (uk. 44)

Tashihisi: Ni tamathali za semi ambazo vitu ambavyo si viumbe hai hupewa hadhi ya kutenda kama binadamu. Mfano: - “Mwezi uliona nyota ziliona hata jua liliona.” (uk. 12) - “Tumaini alisikia sauti kama ya ndege akiimba kwa huzuni.” (uk. 19) - “kila jiwe walilokalia liliwaambia “samahani umekalia bega langu”. (uk. 32)

Tanakali sauti: Ni tamathali ya semi ambayo uigaji wa sauti za asili. Mfano Katika riwaya hii tanakari sauti alizotumia msanii ni kama ifuatavyo: “boooouuu! (uk. 130)

Tafsida: Ni tamathali za semi ambazo kwazo matumizi zake ni za adabu. Mfano: “Kazi kutembeza kengele zako kwenye mabaa.” Uk. 121. - “Tumaini alikuwa akishika mahali pabaya”. Uk. 53.

Methali: Usemi wa kisanii wa kimapokeo unaofikiriwa na jamii kuwa kweli na unaotumiwa kufumbia au kutolea mifano na huwa unabeba maana pana kuliko maneno yenyewe yanayotumiwa. Kwa mfano: - “Wema wa mtu hujulikana siku ya mazishi yake.” (Uk. 13) - “Ugonjwa haufichwi. Afichae ugonjwa ndio hufa.” (Uk. 29) - “Kweli wajinga ndio waalimu wa kuwafunza welevu. (uk. 78) - “Ukishikwa shikamana.” (Uk. 102)

Misemo: Ni mafungu ya maneno yanayotumiwa na jamii ya watu wa lugha hiyo kwa namna maalumu ili kutoa mafunzo, maadili na kuihadharisha jamii. Misemo ni maneno ambayo jamii huyatumia kutokana na uzoefu katika maisha. Kwa mfano: - “Ponda mali kifo chaja.” (Uk. 10) - “Ulimwengu hauna mwema.” (Uk. 103) - “Mapenzi yao sasa yalikuwa yamekwisha pata kovu”. (Uk. 108) - “Nilitaka uniondoe kwenye mdomo wa samba.” (Uk. 24)

Nahau: Haya ni mafungu ya maneno yenye maana maalumu ambayo haitokani na maneno ya kawaida yaliyopo kwenye maneno hayo. Nahau za lugha yoyote hutumiwa zaidi na jamii yenye asili ya lugha hiyo. Kwa mfano: - “Amezunguka mbuyu - amekula rushwa”. (uk. 25) - “Unamvika kilemba cha ukoko”. (Uk. 71) Tanakali sauti: - “Booouuu!”

Mjalizo: Katika tamathali hii sentensi huwa ni mfuatano tu wa maneno yasiyo na viungo vyovyote. Mfano: - “Wenye mashoka ! wenye mikuki na miundu! Wenye pinde na wenye mapanga walianza kulifyeka lile chaka”. (Uk. 27)

Wahusika[hariri | hariri chanzo]

Wahusika ni watu au viumbe waliokusudiwa wawakilishe tabia za watu katika kazi za fasihi. Wahusika wa fasihi ni wa aina kuu tatu,wahusika kazi ya fasihi wanaweza kuwa wahusika wakuu, wahusika wadigo, na ewahusika wajenzi. Wahusika huonyesha dhana mbili muhimu katika maisha ya watu yaani wema na mabaya pia wahusika humaanisha tabia maalumu iliyokusudiwa na jamii.

Katika riwaya ya “Dunia uwanja Fujo” wahusika wake ni mhusika mkuu, whusika wadogo, na wahusika wajenzi kama alivyoainisha Catherine Ndugo (1991) na Wangali Mwai (1991). Katika riwaya hii mwandishi ametumia wahusika wa aina tatu kwa kutumia kigezo cha Catherine na Wangeri Mwai(1991) Kama wahusika wakuu, wadogo, na wajenzi kama ifuatavyo:

Mhusika mkuu: huyu ni yule anayejitokeza kila mara katika kazi za fasihi tangu mwanzo hadi mwisho. Maudhui ya kazi ya fasihi huwa yanamzungukia na hata kutolewa na mhusika mkuu zaidi ya wahusika wengine.

Tumaini: Huyu ndiye mhusika mkuu katika riwaya hii kwani maudhui na dhamira zimejengwa juu yake. Pia tunaona wahusika wajenzi akina John, Anastazia, Dc, na mgeni kutoka Dar es saalam dhamira wanazozitenda zinamgusia mhusika mkuu ambaye ni Tumaini. Jina Tumaini ni jina ambalo amepewa na mzazi wake mzee Kapinga ambaye alikuwa mwalimu. Jina Tumaini linasadifu matumaini ya wazazi wake, pia alikuwa ni mototo pekee wa kiume katika familia ya mwalimu Kapinga pia walikuwa na matumaini pindi atakapomaliza shule ndio atakuwa msaada wao katika familia na pindi watakapokuwa wazeeka. Mambo hayo yanapatikana katika (uk.11). Inasema “… Naam Tumaini alikuwa mtoto wa watu hawa. Tumaini kama jina lenyewe lionyeshavyo alikukuwa peke yake katika tumbo la mama yake…..”

Wasifu wake: - Alikuwa ni mtoto wa Kapinga. (uk. 9) - Alikuwa malaya (uk. 8, 24) - Alikuwa mlevi (uk. 94) - Mchapa kazi (uk. 114) - Mtumia pesa vibaya (uk. 55) - Alikuwa muuaji. (uk. 128) - Alikuwa na mapenzi ya dhati kwa mkewe (uk. 128) - Alikuwa na matusi (uk. 12)

Wahusika wadogowadogo: Hawa ni wahusika ambao hawajitokezi mara kwa mara katika kazi ya fasihi ndio ambao husimamia dhamira ndogo ndogo. Katika riwaya hii ya “Dunia uwanja wa fujo” wahusika wadogo wadogo waliojitokeza ni kama ifuatavyo:

1. Kapinga. Wasifu wake: - Baba yake Tumaini. (uk. 9) - Alikuwa mwalimu. (uk. 9) - Alikuwa na malezi mabaya kwa mwanae. (uk. 12) - Alikuwa mume wa miango. (uk. 9) - Alikuwa mbinafsi. (uk. 15) - Alikuwa hapendi kushilikiana katika jamii. (uk. 12).

2. Kasala. Wasifu wake: - Ni mwanakijiji wa Bugolola. (uk. 1). - Mtoto wa Mugala. (uk. 2). - Baba yake Misana. (uk. 2). - Mume wake Mugele. (uk. 2). - Mtu mwema. (uk. 4). - Kwa kiasi fulani alikuwa mvivu. (uk. 6)

3. Mungere. Wasifu wake: - Mke wa Kasala (uk. 2). - Mama yake Misana (uk. 2). - Mwanakijiji wa Bugolola (uk. 2). - Mtu mwema na mchapa kazi. (uk. 4).

4. Misana. Wasifu wake: - Mtoto wa Kasala (uk. 2). - Alikuwa mtundu. (uk. 3). - Mtoto wa Mungere (uk. 2). - Mdogo wao akina Dennis, Leonila, Aulelia. (Uk. 5).

5. Mugala. Wasifu wake: - Mwananchi wa Bugolola. (Uk. 3) - Mchawi. (Uk. 3 na 7). - Ni mama yake Kasala. (uk. 2) - Ni mjane (uk. 4). - Mtu mwenye hasira (uk. 22) - Alikuwa na malezi mabaya kwa wajukuu zake (uk. 19).

6. Leonila. Wasifu wake: - Alikuwa dada yake Dennis na Misana. - Alikuwa mtoto wa Kasala Mungere. - Alikuwa mpenzi wa Tumaini (uk. 8 na 24).

6. Benadeta. Wasifu wake: - Mke wa pili wa Dennis (uk. 121) - Mtu mwenye chuki (uk. 120) - Alikuwa na dharau na mwenye matusi. (uk. 121)

7. Christina. Wasifu wake: - Alikuwa kahaba. (Uk.96) - Alikuwa mlevi (uk.94) - Alikuwa mlaghai (uk.95) - Hana mapenzi ya dhati (uk.96) - Alikuwa anapenda sana pesa. (Uk. 94)

8. Makoroboi. Wasifu wake: - Alikuwa jambazi (uk.96) - Alikuwa mkatili na mwenye kisasi (uk.96) - Anapenda pesa. (Uk.96)

Wahusika wajenzi[hariri | hariri chanzo]

Ni wahusika ambao maudhui yao na dhamira wanazozitenda zinamsaidia mhusika mkuu katika dhamira azitendazo. Mara nyingi wahusika wajenzi wanakazi ya kunjenga au kumsaidia mhusika mkuu katika dhamira zake. Katika riwaya hii wahusika wajenzi ni kama ifuatavyo:

1. John. Ni mhusika mjenzi kwani dhamira alizobeba na nafasi alizotumiwa na mwandishi ni kwa lengo la kumjenga mhusika mkuu tumaini. Pia tunaona John na Tumaini walikuwa na mahusiano na ushirikiano tangu wakiwa kijijini Bugolola mpaka waliposafiri kuelekea mjini Shinyanga.

Wasifu wake: -Alikuwa mlevi (uk. 62) -Alikuwa malaya (uk. 62 na 66). -Alikuwa mvivu (uk. ) -Ana mapenzi ya dhati (uk. 97)

2. Anastazia. Pia huyu ni mhusika mjenzi kwani alikubali kuambatana na Tumaini kijijini kwenda Mwanza halafu mjini Arusha. Pia uhusiano wao ulidumu na kupelekea kuoana na Tumaini.

Wasifu wake: - Alikuwa na mapenzi ya dhati. (Uk. 57, 97, & 99). - Alikuwa mke wa Tumaini. (Uk. 61) - Mtu mwenye huruma (uk. 99) - Mtu mvumilivu. (Uk. 89)

3. Dennis. Ni mmojawapo wa wahusika wajenzi kwani ndio anaemjenga mhusika Tumaini kwa kiasi kikubwa akiwa mjini Shinyanga.

Wasifu wake: - Ni mtu mwenye mapenzi ya dhati. (Uk. 59) - Alikuwa mtoto wa Kasala. (Uk. 3) - Alikuwa mtumishi wa serikalini

Maudhui[hariri | hariri chanzo]

Katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa ujumbe na msimamo.

Katika riwaya hii mwandishi amejitahidi kwa kiasi kikubwa kuonyesha maudhi mbalimbali katika kazi yake kupitia vipengele mbalimbali kama vile Dhamira, migogoro, ujumbe, falsafa, mtazamo itikadi hii yote ni kwa lengo kuu la la kuelimisha jamii kuhusu mambo mbalimbali yanayotukia katika jamii hiyo.

Dhamira ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Senkoro anataadharisha maana hii isichanganywe na maudhui kwani dhamira ni sehemu tu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.

Dhamira kuu ni wazo kuu linalojitokeza katika kazi ya fasihi, dhamira kuu katika riwaya hii ni matatizo na mikinzano ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa, sasa tuangalie ni kwa jinsi gani mwandishi ameijadili dhamira hii.

Matatizo na mikinzano ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa, Katika riwaya hii “Dunia uwanja wa fujo” kwa kiasi kikubwa riwaya hii imejikita katika dhamira hii ambapo ameonyesha matatizo na mikinzano kiuchumi na kijamii ambayo jamii ya Kitanzania iliyoandikiwa hukabiliwa nayo. Ili kuijenga dhamira hii mwandishi amewatumia wahusika kama vile Tumaini, John ,Anastazia, Kapinga, Dennis ili kuiunda dhamira yake kuu katika riwaya hii. Tukianza na Tumaini mwandishi amemuonyesha kuwa ni mhusika ambaye anapinga sera za kijamaa ya siasa ya ujamaa iliyoanzishwa na serikari nchi nzima hali hiyo inaleta ukinzani kwa tabaka lenye mali kwani hawakuwa tayari kuachia mali zao kwa umma. Hali hii inadhihilisha pale Tumaini alipoamua kupingana na hali hiyo ya kunyanganywa mali zake na kupelekea kumuua mkuu wa wilaya, ambaye alikuwa ndio kiongozi mkuu katika mkoa wa Shinyanga katika shughuli za kusimamia sera hiyo ya ujamaa. (uk. 127) Hali hiyo ni mfano tosha kudhihirisha kuwa dhamira kuu katika riwaya hii ni Matatizo na mikinzano ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa.

Dhamira ndogo ndogo. Haya ni mawazo yanayojitokeza ili kujenga dhamira kuu. Dhamira ndogondogo zinazojitokeza katika riwaya hii ni:

Mapenzi na ndoa. Mwandishi E. Kezilahabi amejadili suala la mapenzi na ndoa katika pande mbili tofauti, kwanza ameonesha mapenzi ya dhati na mapenzi ya ulaghai lakini pia ameonesha ndoa za dhati na ndoa za ulaghai. tukianza na mapenzi ya dhati, mapenzi ya dhati yanajitokeza kwa:

a) Mapenzi ya dhati kwa Tumaini na mkewe Anastazia Mwandishi ameonesha mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo Tumaini kwa mke wake, Mwandishi anathibisha hili pale anapoamua kutoroka na Anstazia na kuelekea mjini Shinyanga ambako walianza maisha mapya pia tunaona jinsi gani wawili hawa walivyojaliana hata katika kipindi cha matatizo. Mfano Anastazia alionyesha mapenzi ya kweli pale alipompelekea Tumaini chakula na kumfaliji kuwa atapona, pindi Tumaini alipopigwa na akina makoloboi. (Uk. 97)

Mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo kwa mke wake pia yanajidhihirisha pindi mke wake huyo alipokubali kuishi na Tumaini japo alikuwa ni mhuni na mlevi pia ha baada ya Tumaini kupigwa na kualibiwa sura Anastazia alindelea kuafiki kuishi na mumewe Tumini, hii ni kwa kuwa alikuwa akimpenda. Mwandishi anathibitisha hili katika uk. 64.

2. Ulevi Mwandishi E, Kezilahabi hakuwa nyuma kujadili suala la ulevi na athari zake kwa binadamu na jamii kwa ujumla, katika riwaya yake hii amemtumia muhusika Tumaini pamoja na John kuelezea dhamira hii. Tukianza na Tumaini, mwandishi anamwonesha Tumaini akianza tabia ya ulevi wa pombe kali baada ya kufiwa na wazazi wake kijijini Bugololola hata alipoamia mkoani Shinyanga aliendelea na tabia hiyo ya ulevi wa pombe, Mwandishi hakuishia hapo tu bali ameonesha na athari za tabia hiyo ya ulevi kama vile kupelekea kufilisika kwa tumaini kama mwandishi anavyothibitisha (Uk. 94 & 95).

3. Malezi kwa watoto Hii ni dhamira nyingine inayojitokeza katika riwaya hii, Mwandishi amemtumia muhusika Tumaini kuilezea dhamira hii, tunamwona Tumaini akipata malezi mabaya kutoka kwa wazazi wake kitu kilichopelekea kuyahalibu maisha ya Tumaini na kumfanya aache shule, awe mlevi, pamoja na mengine mengi.

Mfano: Siku moja Tumaini alimchoma mlezi wake jichoni. Yule kijana alimpiga Tumaini kidogo, Tumaini alikimbia kwenda kushtaki kwa mama yake. “Mama Mpishi amenipiga!” Kwa nini umempiga mtoto wangu!” Mugaya alifoka.” Hali hii inaeleza jinsi Tumaini alivyo lelewa vibaya na kudekezwa na wazazi wake (uk. 11).

Ushirikina na uchawi Ni hali ya kuamini nguvu za giza, ni jambo ambalo lina sababisha jamii nyingi kugawanyika na kukosa amani. Kwani mwandishi anadhihirisha hili anaposema:

Vizuu walilia kwa sauti ya kutisha: yuhu! yuu! huba!” (uk. 30).

“Tena alikuwa akilala ndani ya nyumba yako! Ndio maana mama yako alikuwa mchawi” (uk. 36).

Suala la ushirikina katika jamii inayotuzunguka ni janga ambalo kila siku linahatarisha maisha ya watu hususani wazee wenye macho mekundu wako hatiani kupoteza maisha yao katika baadhi ya maeneo mfano mkoa wa Shinyanga na Simiyu, hivyo dhamira hii haijapitwa na wakati.

Unafiki Hii ni dhamira pia inayojitokeza katika riwaya hii, katika kuijadili dhamira hii Mwandishi amemtumia mke wa Dennis kama mtu mnafiki kwani alijifanya anampenda mmewe kumbe alikuwa na uhusia mwamume mwingine ambaye ni John rafiki yake na Dennis. Mwandishi anadhihilisha hali hiyo akionyesha katika kitabu chake kwamba:

“Heshima yangu imekwishapotea John ukiniacha hivihivi nitaona aibu sana!” (uk. 72).

Tukigeukia katika uhalisia, tabia hii ya unafiki imeshamiri katika jamii zetu, unaweza ukawa na rafiki au ndugu ambaye akawa mnafiki kwako. Jamii inatakiwa kuondokana na tabia hii kwa haifai kabisa.

Nafasi ya mwanamke Katika riwaya hii mwanamke amechorwa katika pande mbili, amechorwa katika upande hasi lakini pia mwanamke amechorwa katika upande chanya, upande hasi mwanamke amechorwa kama kiumbe duni na dhaifu wakati katika upande chanya amechorwa kama mtu jasiri, mchapa kazi, mwenye upendo. n.k. Sasa hebu tuangalie nafasi ya mwanamke katika jamii kama alivyochorwa katika riwaya hii tukianza na upande hasi.

Katika riwaya hii mwanamke amechorwa kama kiumbe duni, dhaifu, katika nafasi mwanamke amechorwa kama:

A) Chombo cha starehe. Mwandishi amemchora mwanamke kama chombo cha starehe anayeweza kutumiwa kuwastarehesha wanaume ili mradi kufurahisha nafsi zao, hili linathibitishwa na Mwandishi katika riwaya hii akimtumia muhusika Christina kama chombo cha starehe, ambaye alionekana kujirahisishwa kwa wanaume ili mladi apate fedha. Mfano uk. 95 & 96.

“Sijaona mwanaume mwoga kama wewe! Kristina alisema.

Tumaini alilala kitandani. Kristina alizima taa” (uk. 96)

Hata katika jamii yetu inayotuzunguka wanawake kwa kujijua au kutojua wamekuwa wakifanywa kama chombo cha starehe kuwastarehesha wanaume, jamii inatakiwa kubadilika na kuondokana na dhana hii kwani mwanamke pia anastahiri heshima katika jamii.

B) Mtu asiye na maamuzi katika jamii. Mwandishi amemchora mwanamke kama mtu asiye na maamuzi katika jamii yake, kwa mfano anamtumia muhusika ambaye alikuwa nini mama yake Tumaini kushindwa kufanya maamuzi juu mali alizoziacha kama urithi wa Tumaini japo hakupenda kumuachia mtoto wao fedha nyingi(alijua zitamuangamiza mwanae) lakini alishindwa kubatilisha kutokana na maamuzi yaliyoachwa na mumewe.mfano anaonyesha;

“Ni vizuri zaidi mtoto kurithi vitu kama hivyo, licha ya hekima na kumrithisha mototo pesa ni ni kunvisha taji la uovu.” Baba yako alikataa kabisa; na kwa kuwa nilishindwa mawazo ya baba yako alipokuwa bado mzima, siwezi sasa kugeuza tamshi lake.” (uk. 15)

Hata katika jamii yetu, inawachukulia wanawake kama watu wasio na maamuzi katika familia na pindi inapotokea kufiwa na waume zao huwa wanapata shida na manyanyaso kutoka kwa ndugu wa mwanaume kama vile kufukuzwa kwenye nyumba, kunyang'anywa watoto na mali nyingine alizoshirikiana kuzichuma na mumewe. Jamii inatakiwa kumpa nafasi mwanamke na itambue kuwa ana haki sawa kama mwanamume.

C. Msaliti. Hii ni nafasi nyingine ambayo mwandishi amemchora mwanamke, kwa mfano tunaona mke wa Dennis kama mtu mnafiki kwani alijifanya anampenda mmewe kumbe alikuwa na uhusia mwamume mwingine ambaye ni John rafiki y yake na Dennis. Mwandishi anadhihilisha hali hiyo akionyesha katika kitabu chake kwamba:

“Heshima yangu imekwishapotea John ukiniacha hivihivi nitaona aibu sana!” (uk. 72).

Migogoro ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali.

Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, mogogoro ya nafsi, na migogoro ya kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi. Kwa kuanza

Mgogoro wa nafsi tunamuona Tumaini akipatwa mgogoro nafsi pindi alipofiwa na wazazi wake na baadae kug unduli kuwa walikuwa wamechuliwa ka vizuu na bibi ake na Leonila pia mgogoro nafsi wa pili ni pale ambapo leonila ankataliwa kuolewa na Tumaini anajikuta akiingia katika lindi la mgogoro nafsi. Pia Leonila anjikuta akiingia katika mgogo wa nafsi pindi pindi wazazi wake walipomwandalia mazingila ya kuolewa na tembo (uk. 15 & 39).

Mgogoro kati ya mtu na mtu Hapa tunaona mgogoro kati ya Anastazia pamoja na wazazi wake, Dennis na John, Dennis na Benadeta, Tumaini na Serikali,Kasala na mama yake.mfano. (uk. 22, 23 & 128).

-“Kumtunza mzee ni mzigo lakini inabibi uuchukue kwa fulaha” (uk. 23)

-“Baba nihurumie! Lakini Kasala aliendelea kumpiga.

Bibi wameniua kwa sababu yako!” (uk. 22).

Ujumbe/Mafunzo[hariri | hariri chanzo]

Ujumbe: mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi. Baadhi ya ujumbe unaopatikana katika riwaya hii ni pamoja na:

Kikulacho kinguoni mwako: Huu ni ujumbe ama funzo tunalolipata baada ya kusoma riwaya hii, ujumbe huu tunaupata kupitia muhusika mama Resi pindi kwani alijifanya anampenda mmewe kumbe alikuwa na uhusia mwamume mwingine ambaye ni John rafiki yake na Dennis. (uk. 72)

Majuto ni mjukuu: Ujumbe huu unajitokeza pia katika riwaya hii, mwandishi anamtumia mhusika Tumaini pale alipoendekeza starehe zilimsababisha aingie kwenye mtego wa majambazi wa kupigwa na kuhalibiwa sura yake. (uk. 98)

Elimu ni ufunguo wa maisha: Mwandishi anatupa ujumbe mwingine kuwa, ili mtu aweze kufanikiwa hana budi kushikiria na kuizingatia elimu kwani elimu ni ufunguo wa maisha, ujumbe huu katika riwaya hii unajitokeza kwa muhusika Dennis ambaye alipata kazi nzuri sababu alikuwa amekwenda shule na kupata elimu ya kutosha.

“Nyumba ya Dennis ilikuwa ni kubwa sana. Ilikuwa na vyumba saba bila kuhesabu jiko lililokuwa mumo humo ndani” (uk. 60)

Mpende akupendaye asiyekupenda achana nae, 'katika riwaya hii anaipa ujumbe jamii yake kuwa penda pale unapopendwa na si kumng'ang'ania tu mtu kwa kuwa moyo wako unataka tu kuwa naye, ujumbe huu tunaupata kupitia kwa muhusika Dennis alipogundua kuwa mke wake alikuwa na mapenzi ya uongo aliamua kuachana nae.

“Dennis alipofika nyumbani alipiga kerere nimemfukuza mbwa,Tumaini” (uk. 109)

Msimamo[hariri | hariri chanzo]

Msimamo katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Hivyo basi mwandishi anamsimamo kwamba mambo yote yanayotendeka katika ulingu huu ni sasawa na fujo tupu, kwani hata kama utajitahidi vipi kupambana na shida za ulimwengu huu matatizo yataendelea kukukabili mpaka umauti utakapokufikia.

Jina na jalada la kitabu[hariri | hariri chanzo]

Tukianza na jina la kitabu, jina ni “Dunia uwanja wa fujo” linasadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu kwani tangu mwanzo wa riwaya hii kuna matukio au fujo mbalimbali ambazo zimejitokeza fujo hizo ni kama vile umalaya, ulevi, uchawi pamoja na mengineyo mengi. Mfano suala la uchawi lidhihilika pale katika uk. 36 unasema “Tena alikuwa akilala ndani ya nyumba yako! Ndio maana mama yako alikuwa mchawi” (uk. 36).

Falsafa ya mwandishi[hariri | hariri chanzo]

Kulingana na Mbunda Msokile yeye anasema kuwa Falsafa ni wazo ambalo mtu anaamimini lina ukweli Fulani unaotawala maisha yake pamoja na maisha ya jamii. Hivyo basi katika riwaya hii anaamini kuwa katika riwaya yake ya “Dunia ni uwanja wa fujo” Kwamba maisha hayana raha wala maana isipokuwa dunia ni uwanja wa fuzo.

Kufaulu kwa mwandishi[hariri | hariri chanzo]

Mwandishi wa riwaya hii amefaulu kwa kiasi kikubwa kuibua dhamira dhamira mbalimbali katika jamii. Kwani dhamira hizo zimeonekana kuwa ni kikingamizi kikubwa cha katika maendeleo ya jamii. Mfano suala la uchawi na ushirikina , malezi mabaya, ukale na usasa. Pia mwandishi amefaulu katika suala zima la lugha kwani ametumia lugha rahisi na inayoeleweka kwa msomaji yeyote hata kama si msomi mkubwa.