Charles Messier
Charles Messier (tamkaː sharl mesyee; 26 Juni 1730 – 12 Aprili 1817) alikuwa mwanaastronomia kutoka nchini Ufaransa anayekumbukwa kwa kutunga orodha ya magimba ya angani iliyojulikana kwa jina la "Orodha ya Messier". Namba za orodha yake zinatumiwa hadi leo kwa kutaja magimba ya angani mbalimbali, kwa mfano “M31” ambayo ni Galaksi ya Andromeda.
Maisha
Alizaliwa katika jimbo la Lorraine, Ufaransa. Alianza kuvutiwa na habari za astronomia baada ya kuona nyotamkia kubwa ya mwaka 1744 na kupatwa kwa jua mnamo tarehe 25 Julai 1748.
Kazi yake ya kwanza kuanzia mwaka 1754 ilikuwa ajira kama karani wa Joseph Nicolas Delisle aliyekuwa mwanastronomia mkuu wa jeshi la maji la Ufaransa. Kazi ya Messier ilikuwa pamoja na kuchora ramani. Deslisle alitambua uwezo wake alimfundisha pia misingi ya astronomia. Hasa alimfundisha kuandika kila kitu alichotazama angani pamoja na maelezo yakinifu.
Mwaka 1757 aliagizwa na Delisle kutafuta Kometi ya Halley iliyotabiriwa kurudi mwaka ule; aliitambua tu kwenye Januari 1759 kwa sababu utabiri ulikuwa na makosa. Mwaka 1761 alitazama mpito wa Zuhura mbele ya jua na mwaka 1764 alifaulu kukuta nyotamkia ya kwanza isiyojulikana bado.
Tangu 1764 Messier alitafuta hasa nyotamkia angani. Kwa jumla alizitambua 13:[1]
- C/1760 B1 (Messier)
- C/1763 S1 (Messier)
- C/1764 A1 (Messier)
- C/1766 E1 (Messier)
- C/1769 P1 (Messier)
- D/1770 L1 (Lexell)
- C/1771 G1 (Messier)
- C/1773 T1 (Messier)
- C/1780 U2 (Messier)
- C/1788 W1 (Messier)
- C/1793 S2 (Messier)
- C/1798 G1 (Messier)
- C/1785 A1 (Messier-Mechain)
Pamoja na nyotamkia hizi alikuta pia kiasi cha magimba mengine kama vile nebula, fungunyota au galaksi.
Tangu mwaka 1771 alianza kuzipeleka kwenye umma kwa njia ya orodha yake alimoorodhesha magimba 110 zinazotajwa hadi leo kwa namba kama “Messier-1” (au M1) na kadhalika[2].
Tazama pia
Marejeo
- ↑ "Maik Meyer. Catalog of comet discoveries". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2008-07-16. Iliwekwa mnamo 2017-04-24.
- ↑ History of the Messier Catalogue, tovuti ya http://www.messier.seds.org/ "The Messier catalogue", iliangaliwa Machi 2019
Viungo vya Nje
- Amateur Photos of Charles Messier Objects Archived 28 Julai 2012 at the Wayback Machine.
- Messier Marathon Archived 2 Septemba 2011 at the Wayback Machine. Tries to find as many Messier objects as possible in one night.
- New General Catalog and Index Catalog revisions
- Clickable table of Messier objects Archived 20 Oktoba 2014 at the Wayback Machine.