Angahewa
Angahewa ni matabaka ya gesi za hewa yanayozingira sayari au gimba lingine la angani yakishikwa na uvutano wa gimba husika.
Angahewa ya Dunia
Angahewa inakinga uhai duniani kwa kupunguza mnururisho wa urujuanimno wa Jua, kutunza halijoto duniani kwa kuakisisha mawimbi ya mialekundu, kupunguza tofauti kati ya baridi na joto na kuwapa wanyama na mimea viwango vya oksijeni na nitrojeni wanavyohitaji.
Magimba ya angani mengine kama sayari au Jua huwa pia na aina za angahewa ingawa gesi zake ni tofauti na za duniani.
Gesi zilizopo katika angahewa ya Dunia ni hasa nitrojeni (78%) na oksijeni (21%) pamoja na viwango vidogo lakini muhimu vya arigoni (0.9%), dioksidi kabonia (0.035%), mvuke wa maji na gesi nyingine mbalimbali.
Angahewa haina mwisho kamili, ila inazidi kuwa hafifu jinsi inavyofikia juu. Asilimia 75 za masi ya hewa yake iko katika angavungu hadi kilomita 11 juu ya uso wa Dunia. Uzito wa hewa hupimwa kama kanieneo angahewa.
Halijoto na matabaka ya angahewa
Sehemu za angahewa zina baridi au joto zaidi kutegemeana na kimo. Tukipaa juu ya uso wa Dunia halijoto inazidi kuwa baridi, baadaye joto tena, kadiri jinsi tunavyopaa. Mabadiliko ya halijoto yanafuata muundo wa tabaka zinazotofautishwa na kiwango cha joto au baridi kinachopimwa.
Kwa jumla inawezekana kutofautisha matabaka 5 ambayo ni
- Angavurugu (troposphere) - inaanza kwenye uso wa Dunia na kuishia mnamo kilomita 7 (juu ya ncha za Dunia) - 15 (juu ya sehemu za tropiki) juu yake; baridi inazidi jinsi unavyopaa juu (kwa hiyo ni baridi mlimani kushinda chini); mawingu yako hapa na hii ni tabaka ambako halihewa inatokea.
- Angatando (stratosphere) - inaishia kwenyi kimo cha km 50; hapa joto linaanza kuzidi tena. Eropleni kubwa zinapita hapa kwa sababu hakuna upepo mwenye nguvu inayosumbua mwendo
- Angakati (mesosphere) - inaishia kwa kimo cha km 80 - 85; hapa baridi inazidi jinsi unavyopaa; kuna upepo mkali.
- Angajoto (thermosphere) - inaishia kwa kimo cha km 500 - 600; joto linapanda pamoja kimo; tabaka hii ni muhimu kwa mawasiliano ya redio kwa sababu inaakisisha miale ya redio ya AM.
- Angajuu (exosphere) - ni tabaka la nje inayoanza kati ya km 500 - 1000 na kuwa hafifu kadri unayopaa juu zaidi; inafikia kilomita maelfu hadi kwa kimo cha takriban 10,000 km ambako hewa haipimiki tena
Matabaka ya juu, yaani tabakajoto na tabakanje, huitwa pia angaioni kwa sababu atomu za gesi zake zinapatikana katika hali ya ioni zilizopoteza elektroni kutokana na kupigwa na miale ya Jua iliyo bado kali sana hapo nje.
Angahewa kwenye sayari
Nje ya Dunia yetu angahewa imetambuliwa pia kwenye sayari nyingine. Katika Mfumo wa Jua kuna sayari 4 za ndani zinazofanana kiasi, ni Utaridi, Zuhura, Dunia na Mirihi. Zote nne ni sayari zinazofanywa na mwamba.
- Kati ya hizi Utaridi haina angahewa, ikiaminiwa yote imepotea kutokana na kupigwa vikali na upepo wa Jua lililo karibu na sayari hii.
- Zuhura ina angahewa nzito, hasa ya dioksidi kabonia (CO2)
- Mirihi na angahewa hafifu sana ya dioksidi kabonia (CO2). Inaaminiwa kuwa imepotea asilimia kubwa ya angahewa yake. Mirihi haina uga sumaku na hivyo upepo wa Jua unapiga sayari hii moja kwa moja na kusukuma molekyuli za angahewa mbali kwenda anga-nje.
Sayari kubwa za nje kama Mshtarii na Zohari si rahisi vile kuofautisha kati ya sayari yenyewe na angahewa yake. Sayari hizi huitwa pia "jitu za gesi" kwa sababu asilimia kubwa ya sayari yote ni elementi kama hidrojeni na heli ambazo kwetu duniani zinapatikana kama gesi. Kutokana na umbali mkubwa na Jua ni baridi zaidi hadi gesi hizi kupitia katika hali mango. Vilevile hidrojeni katika kiini cha Mshtarii inaaminiwa kuwa katika hali metalia kutokana na shinikizo kubwa ya masi yake.
Kuna miezi kadhaa zinazunguka sayari za Jua ambako angahewa zimegundliwa, kwa mfano kwa mwezi Titani wa Zohali na miezi ya Europa na Ganimedi ya Mshtarii.