Nenda kwa yaliyomo

A

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Alfabeti ya Kilatini
Aa Bb Cc Dd
Ee Ff Gg Hh Ii Jj
Kk Ll Mm Nn Oo Pp
Qq Rr Ss Tt Uu Vv
Ww Xx Yy Zz
(Kwa matumizi ya Kiswahili)
ch dh gh kh
mb mv nd ng ng' nj
ny nz sh th
Herufi A kwa mwandishi mbalimbali

A ni herufi ya kwanza katika alfabeti ya Kilatini ambayo ni pia mwandiko wa Kiswahili cha kisasa. Asili yake ni Alfa ya Kigiriki.

Maana za A

  • katika muziki A ni noti.
  • Katika tiba A ni aina ya damu.
  • Kwa magari A ni alama ya gari kutoka Austria.
  • Kati ya vipimo a ni alama ya Ar yaani eneo la mita kumi mara kumi
  • Katika fizikia A ni alama ya ampea.
  • Katika shule za nchi mbalimbali A ni daraja la juu i(la kufaulu) linalowezekana
  • kwa maana ya kiashirio A ni alama ya chanzo

Historia

Kichwa ch ng'ombe
(Alama ya kale iliyokuwa silabi)
"Alef" ya Wafinisia
(neno lao kwa ng'ombe)
Kigiriki
Alfa
Kilatini
A
Proto-semitic ox head Phoenician aleph Greek alpha Roman A

Asili ya herufi A ni miandiko iliyotangulia alfabeti ya Kilatini. Waroma walipokea mwandiko kutoka alfabeti ya Kigiriki kupitia alfabeti za Kiitalia za awali kama Kietruski. Wagiriki walipokea kutoka Wafinisia.

Kama herufi nyingine za alfabeti ya Kigiriki alfa imetoka katika alfabeti ya Wafinisia iliyokuwa alfabeti ya kwanza ya dunia. Wafinisia waliendeleza mwandiko wa kikabari wa kale uliokuwa mwandiko wa silabi na kuifanya alfabeti ya herufi moja-moja.

Faida ya alfabeti ni ya kwamba inahitaji alama chache kulingana na mwandiko wa silabi mwenye alama kwa kila silabi ya lugha fulani au mwandiko picha unaohitaji maelfu ya alama za picha.

Alef ya Wafinisia

Wafinisia walichukua alama ya ng'ombe wakairahisisha na kuiita kwa neno lao "alef" lenye maana ya "ng'ombe" lakini walisoma tu "'" yaani kituo kimya jinsi ilivyo hadi sasa katika alef ya Kiebrania. Hivyo walifanya picha kuwa herufi. Herufi ilinama jinsi kichwa cha ng'ombe kinavyoonekana kikitazamiwa kutoka kando.

Alfa ya Wagiriki

Wagiriki walipokea alfabeti kutoka Wafinisia na pia jina la herufi hii. Hawakuwa na matumizi kwa ile sauti kimya ya Wafinisia lakini walihitaji herufi za vokali ambazo hazikuandikwa katika Kifinisia jinsi ilivyo hadi sasa katika Kiebrania na pia mara nyingi katika Kiarabu.

Kwa hiyo walitumia alama kwa sauti ya A wakabadilisha kidogo jina kuwa "alfa" badala ya "alef". Lakini katika lugha yao hawakuelewa tena maana asilia iliyokuwa "ng'ombe". Kwao ilikuwa alama ya sauti tu.

Mwanzoni waliandika herufi kwa umbo la kulala kama Wafinisia lakini katika karne za baadaye herufi iligeuzwa na kuandikwa mwishowe jinsi tunavyozoea leo.