Nenda kwa yaliyomo

Ramadan (mwezi)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sehemu ya mfululizo wa makala juu ya

Uislamu

Imani na ibada zake

Umoja wa Mungu
Manabii
Misahafu
Malaika
Uteule
Kiyama
Nguzo za Kiislamu
ShahadaSwalaSaumu
HijaZaka

Waislamu muhimu

Muhammad

Abu BakrAli
Ukoo wa Muhammad
Maswahaba wa Muhammad
Mitume na Manabii katika Uislamu

Maandiko na Sheria

Qur'anSunnahHadithi
Wasifu wa Muhammad
Sharia
Elimu ya Sheria za KiislamuKalam

Historia ya Uislamu

Historia
SunniShi'aKharijiyaRashidunUkhalifaMaimamu

Tamaduni za Kiislamu

ShuleMadrasa
TauhidiFalsafaMaadili
Sayansi
SanaaUjenziMiji
KalendaSikukuu
Wanawake
ViongoziSiasa
Uchumi
UmmaItikadi mpyaSufii

Tazama pia

Uislamu na dini nyingine
Hofu ya Uislamu

.

Ramadan au ramadhani, (kwa Kiarabu: رمضان) ni mwezi wa tisa katika Kalenda ya Kiislamu na mwezi wa kufunga katika Uislamu kuadhimisha ufunuo wa kwanza wa Qur'an kutona na mafundisho ya Mtume Muhammad. Mwezi huo huwa na siku 29 au 30 kutegemeana na kuonekana kwa mwezi.

Kufunga ni moja ya Nguzo tano za Uislamu. Mwislamu mzima, mwenye afya nzuri, anatakiwa kushiriki katika swaumu ambayo ni ibada ya kufunga chakula na kinywaji mchana kutwa, pamoja na kujizuia kufanya mapenzi toka alfajiri hadi magharibi.

Matendo hayo ya toba yanaendana na kuswali sana na kusoma Quran kwa wingi.

Kwa wagonjwa, wanaosafiri, wazee, wajawazito, wanaonyonyesha na wanawake wenye hedhi sio lazima kufunga.

Mwisho wa Ramadhani ni sikukuu ya Idul Fitri (عيد الفطر - ʿīdu ʾl-fiṭr) ambayo ni sherehe ya furaha na kupongezana. Waislamu hutoa zakat (zakatul-fitri زكاة الفطر) na kuswali, baadaye hukutana kwenye karamu.

Neno Ramadhani linatokana na mizizi ya Kiarabu ramiḍa au ar-ramaḍ, ambayo inamaanisha joto kali au ukavu.[1]

Asili: Qurani kuhusu Ramadan

Ramadan inatajwa katika Quran kwenye sura 2 aya 185 inayosema:

Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni wongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hesabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuokoeni ili mpate kushukuru.

Kufuatana na mapokeo ya Kiislamu Muhammad alianza kupokea ufunuo wa aya za Qurani katika kipindi cha Ramadhani. Kutokana na historia hii Waislamu huangalia Ramadhani kama mwezi mtakatifu katika kalenda ya Kiislamu.

Kuna wataalamu wanaoona ya kwamba kutokea kwa utaratibu wa kufunga mwezi mzima uliathiriwa na desturi ya kufunga katika Kanisa la Syria. Kufuatana na Bukhari, Waarabu asilia na Wayahudi wa Uarabuni kabla ya kuja kwa Uislamu walifunga kwa siku chache tu, kwa mfano siku ya Ashura [2] [3] [4]

Kusoma Qurani

“Mwezi wa Ramadhani ambayo imeteremshwa ndani yake Qur-an hali ya kuwa ni uongofu kwa watu …………" Kwa kuwa katika mwezi huu ndio Qurani iliteremshwa kwa Mtume, inatakiwa kwa Muislam kufanya bidii kuisoma angalau juzuu moja kwa siku ili aweze kumaliza msahafu ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Ramadhan.

Kuharakisha kufungua

Miongoni mwa sunna tukufu zinazotakiwa kwa mfungaji katika mwezi huu kuzikimbilia, ni kuharakisha kufungua baada tu ya kuzama jua, kwani Mtume amesema katika hadithi iliopokewa na Tirmidhy, Ibnu Khuzayma na Ibnu Habban: “Hakika nimpendaye zaidi miongoni mwa waja wangu ni anayefanya haraka katika wao kufungua saumu.”

Kusali usiku

Kadiri ya dini hiyo Mwislamu anatakiwa kuyatumia masiku ya mwezi huu mtukufu katika kumuabudu Allah kwa kusali na kufanya ibada nyingine, kwani ni mwezi wa pekee ambao ndani yake kunapatikana usiku wa cheo (Laylatul Qadr) ambao ibada ya usiku huo inalingana na ibada ya miezi elfu moja, na kwa hekima yake Allah hakutubainishia kuwa ni usiku wa tarehe ngapi. Na hii ni moja miongoni mwa fadhila za kuswali katika masiku ya mwezi huu. Vilevile mwenye kusimama kwa ibada katika masiku haya husamehewa makosa yake yote yaliyotangulia, kama alivyosema Bwana Mtume: “Mwenye kusimama usiku wa Ramadhani kwa kufanya ibada hali ya kuwa na imani na kutaraji thawabu anasamehewa yoteyaliotangulia miongoni mwa makosa yake.” (Bukhari na Muslim).

Kula daku

Kula daku vilevile ni miongoni mwa sunna tukufu zinazodharauliwa na wengi kati ya Waislam, kumbe fadhila zake ni kubwa kupita kiasi, miongoni mwa hizo ni kurehemewa na Allah na kutakiwa msamaha na malaika watukufu kama alivyosema Mtume katika hadithi: “Hakika Allah na Malaika wake wanawarehemu wenye kula daku.” (Twabrani, Ibnu Habban).

Vile vile Mtume amesisitiza katika hadithi kwa kusema kuwa: “Hakika daku ni baraka amekupeni Allah, hivyo basi musiiache”. (Annasai)

Kukaa Itikaaf

Inatakiwa kwa muislam kuujaalia mwezi huu na kuutumia katika kuchuma na kuvuna aina tofauti ya mema ikiwemo Itikaaf, kwani ni miongoni mwa ibada bora sana zinazomkurubisha mja kwa Mola wake, hasa awapo katika mwezi huu wa Ramadhani, kwani baadhi ya wanavyuoni wamesema kuwa haisihi ibada hii ya itikaaf pasi na funga. Na yatoshe malipo makubwa yaliyotajwa katika hadithi; Mtume amesema: “Mwenye kukaa itikaaf siku kumi katika mwezi wa Ramadhani, basi ni kama aliyehiji na akafanya umra mara mbili mbili." (Bayhaq)

Kutoa sadaka

Miongoni mwa ibada tukufu alizokuwa akizifanya Mtume ni kutoa sadaka na alilipa umuhimu sana jambo hili hadi wakati wa kuondoka kwake ulimwenguni alipokuwa katika sakaratul mauti kila alipopata fahamu ilikuwa akimuuliza Bibi Aisha iwapo ashazitoa sadaka zile dirhamu nne zilizokuwa nyumbani? Kadhalika kutoa huku kwake kulikuwa kukiongezeka katika Ramadhani.

Kumtaja Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)

Katika mwezi wa Ramadhani kadhalika inatakiwa kwa Muislam kuwa mengi ya maneno yake yawe katika kumtaja Allah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwani ni jambo ambalo linasaidia katika kuusafisha moyo wake na kuiboresha funga yake. Allah ameamrisha tumtaje kwa wingi katika aya nyingi za Qurani, na hii ndiyo ibada pekee aliyosema Allah kuwa ifanywe kwa wingi, na miongoni mwa aya hizo; “Enyi Mlioamini mtajeni Allah kwa wingi na mumtakase yeye asubuhi na jioni.” (Al- Ahzaab 41 na 42)

Kadhalika Mtume alifundisha aina tofauti za kumtaja Allah ili tusichoke na jambo hili kwani mwanadamu ni mwepesi wa kuchoka na jambo moja tu. Vilevile akaonyesha tofauti kubwa iliyopo kati ya anayemtaja Allah na asiyefanya hivyo katika hadithi aliposema; “Mfano wa anayemtaja Allah na asiyemtaja ni mfano wa mtu aliyehai na aliyekufa.” (Bukhari).

Marejeo

  1. "Ramadan | Fasting, Traditions, & Facts | Britannica". www.britannica.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2023-02-26.
  2. Bukhari-Ibn-Ismail, AbdAllah-Muhammad. "Sahih Bukhari - Book 031 (The Book of Fasting), Hadith 222.". hadithcollection.com. Retrieved 19 July 2012.
  3. Bukhari-Ibn-Ismail, AbdAllah-Muhammad. "Sahih Bukhari - Book 031 (The Book of Fasting), Hadith 223.". hadithcollection.com. Retrieved 19 July 2012.
  4. Bukhari-Ibn-Ismail, AbdAllah-Muhammad. "Sahih Bukhari - Book 031 (The Book of Fasting), Hadith 220.". hadithcollection.com. Retrieved 19 July 2012.
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.