Martin Luther King, Jr.

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Martin Luther King, Jr.

Dr Martin Luther King, Junior (Atlanta, Georgia, 15 Januari 1929Memphis, Tennessee, 4 Aprili 1968) alikuwa Mkristo mwenye asili ya Afrika, mchungaji wa Kibaptisti na mwanaharakati mashuhuri kutoka nchi ya Marekani aliyepigania haki za binadamu, hasa Wanegro, wakati nchi hiyo ilipokuwa bado na sheria za ubaguzi wa rangi.

Baadhi ya madhehebu ya Marekani, hasa Waanglikana na Walutheri, yanamheshimu kama mtakatifu mfiadini.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe yake ya kuzaliwa au ya kuuawa.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Martin alizaliwa mjini Atlanta, Georgia, Marekani. Alikuwa mtoto wa mzee Martin Luther King Sr. ambaye pia alikuwa mchungaji na kiongozi wa kupigania haki za binadamu. Baba yake alimwita Martin Luther ili amheshimu huyu mtaalamu Mjerumani wa karne ya 16.

Aliwaongoza Waamerika Weusi kupinga ubaguzi wa rangi uliokuwepo katika sehemu za USA mpaka miaka ya 1960. Katika mapambano hayo alifuata mapokeo ya Mt. Agostino katika Kanisa. Alieleza ya kuwa kila mtu amepewa na Mungu heshima yake, hivyo sheria za nchi na serikali zinazovunja heshima hiyo si za haki. "Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu" (Mdo. 5:29).

Aliwaita watu kupinga ubaguzi hata dhidi ya serikali na polisi lakini bila kutumia mabavu. Watu waliongozwa na M. L. King waliandamana mahali pengi wakanyamaza wakipigwa na kukamatwa. Wakaingia katika hoteli, shule na vyombo vya usafiri vilivyotengwa kisheria kwa watu weupe, wakasubiri mpaka polisi ilipoitwa na kuwakamata. Wakapokea adhabu na mapigo.

Baada ya miaka kadhaa mapambano kwa silaha hizo za amani yalishinda. Mahakama kuu ya Marekani na serikali kuu zilitangaza ya kuwa ubaguzi wa rangi katika mikoa mbalimbali hauruhusiwi kuendelea.

Mwaka 1964 alipokea Tuzo ya Nobel ya Amani kwa sababu ya kutetea haki bila ya kutumia mabavu.

Hata hivyo aliuawa kwa kupigwa risasi na mteteaji wa ubaguzi wa rangi mwaka 1968.

Baada ya hapo ujumbe wake ulizidi kukubalika na sheria mbalimbali zilibadilishwa.

Anahesabika kama mmoja wa watu wakubwa wa Mungu katika historia ya Kanisa.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.