Bahari ya Chumvi
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bahari ya Chumvi (Kiebrania: יָם הַמֶּלַח yam ha-melaḥ "bahari ya chumvi"; Kar.: ألبَحْر ألمَيّت al-bahrᵘ l-mayyit, "bahari ya mauti") ni ziwa lililoko kati ya Israel, Palestina na Yordani. Eneo lake ni takriban 600 km². Mwambao wa ziwa ni mahali pa chini kabisa kwenye nchi kavu ya dunia uko mita 400 chini ya uwiano wa bahari.
Ziwa liko ndani ya bonde la mto Yordani ambalo ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki. Maji yake yamepokea chumvi nyingi na kiasi cha chumvi ni mara tisa kulinganisha na chumvi katika maji ya bahari. Kiasi kikubwa cha chumvi kimezuia kuwepo kwa samaki ndani yake; uhai wa pekee ni aina za bakteria na algae.
Kiasi kikubwa cha chumvi kimesababisha densiti ya maji yake kuwa juu; hivyo mwanadamu huelea katika maji haya tu bila jitihada yoyote. Watalii hupenda kufika hapa wakiogelea na kujipakia matope ya ziwa yanayosemekana kuwa nia tabia za kuponya magonjwa ya ngozi.
Israel na Yordani zimeanzisha viwanda vinavyosafisha aina mbalimbali za chumvi kwa matumizi ya kibiashara.
Kwa jumla kiasi cha maji ziwani kimerudi nyuma kwa sababu mto Yordani ambayo ni mto wa pekee unaoingia humo umehamishwa kwa shughuli za umwagiliaji.