Anga
Anga (mara nyingi pia: mbingu) ni uwazi ule tunaoona juu yetu tukiinua kichwa juu nje ya jengo. Ni uwazi mkubwa; tukisimama kwenye tambarare au juu ya mlima kwenye mchana bila mawingu inaonekana kama nusutufe yenye rangi ya buluu. Ile buluu inaongezeka tukitazama juu zaidi kulingana na sehemu karibu na upeo. Wakati wa usiku anga ni nyeusi lakini inajaa nuru za nyota.
Kwa lugha nyingine anga ni eneo la angahewa au upeo unaojaa hewa juu ya uso wa ardhi. Sehemu hii inajaa molekuli za gesi za angahewa hasa nitrojeni na oksijeni; ni molekuli hizi zinazoakisisha nuru ya jua na kusababisha rangi ya buluu ya anga wakati wa mchana. Bila hewa anga ingekuwa nyeusi muda wote jinsi ilivyo mwezini (linganisha picha).
Wakati wa mchana tunaona jua angani lisipofunikwa na mawingu. Wakati wa usiku tunaona nyota na mwezi zinazoonekana pia asubuhi na jioni ambako nuru ya jua haina nguvu bado au tena. Mengine yanayoonekana angani ni mawingu, upinde wa mvua, ndege au eropleni.
Anga la Nje [hariri]
Anga halina mwisho. Pale tunapojadili sehemu kubwa iliyoko nje ya angahewa tunaweza kuita anga la nje na hii ni upeo wa mwezi, sayari, jua na nyota. Sayansi ya astronomia inaifanyia utafiti. Anga la nje ni karibu hali ya ombwe yaani tupu pasipo magimba ya angani au vumbi. Lakini inajaa mnururisho wa aina mbalimbali na kani kama graviti.
Anga na mbingu [hariri]
Katika lugha ya kila siku maneno "anga" na "mbingu" mara nyingi yanatumiwa kwa maana moja: "Mawingu yanatembea angani - mawingu yanatembea mbinguni". Lakini mbingu huwa na maana ya ziada yaani ya kidini kwa kutaja pia upeo wa Mungu au hali inayopita maarifa ya duniani: "hapa ninajisikia kama mbinguni" ni tofauti sana na "hapa najisikia angani". Katika wikipedia hii tunatumia neno "mbingu" zaidi kwa maana ya kidini.
Viungo vya nje [hariri]
| Makala bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |