Wikipedia:Makala ya wiki/Malaria

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Dlili za Malaria

Malaria ni ugonjwa wa kuambukiza ambao unaambukizwa na mbu wa jenasi Anopheles na kusababishwa na kidubini aina ya protisti Plasmodium. Mara nyingi ugonjwa huo huitwa "homa" tu, ingawa homa ni dalili yake mojawapo tu, pia kuna magonjwa mengi yanayosababisha homa. Malaria inatokea katika maeneo ya kitropiki na yanayokaribia tropiki ikiwa ni pamoja na sehemu za Amerika, Asia na Afrika. Mwaka 2015 duniani kulikuwa na maambukizi milioni 214 ya malaria, na watu 438,000 walikufa, wengi wao (90%) wakiwa barani Afrika, hasa watoto wachanga katika mataifa ya kusini kwa jangwa la Sahara. Malaria ni mojawapo ya magonjwa yaliyoenea sana na ni tatizo kuu la afya ya umma. Kwa kawaida huhusishwa na umaskini, lakini pia ni sababu ya umaskini na kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya uchumi. Kawaida, watu hupata ugonjwa wa malaria kwa kung'atwa na mbu wa kike wa jamii ya Anopheles aliyeambukizwa. Mbu aina ya Anopheles pekee ndio wanaoweza kusambaza malaria, na ni lazima wawe wameambukizwa kupitia damu waliyofyonza kutoka kwa mtu aliyeambukizwa. Maambukizi ya malaria yanaweza kupunguzwa kwa kuzuia kung'atwa na mbu kutumia vyandarua, dawa za kuzuia wadudu, au hatua za kudhibiti maenezi ya mbu kama vile kunyunyizia dawa za kuua wadudu ndani ya nyumba na kupiga mifereji kuondoa maji yaliyosimama ambapo mbu hutaga mayai yao. ►Soma zaidi