Waraka wa kwanza wa Klementi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Waraka wa kwanza wa Klementi ni andiko lililoandikwa na askofu wa Roma (Italia) Klementi wa Roma mnamo mwaka 96 BK kwa kanisa la Kikristo mjini Korintho (Ugiriki).

Ni kati ya maandiko ya kwanza ya kikristo nje ya Biblia (Agano Jipya) yaliyohifadhiwa na kujulikana hadi leo.

Waraka wa kwanza wa Klementi kati ya maandiko ya kale ya kikristo[hariri | hariri chanzo]

Jina rasmi la andiko hili ni "Klementi kwa Wakorintho" (kwa Kigiriki Κλήμεντος πρὸς Κορινθίους, Klēmentos pros Korinthius).

Iliandikwa kwa lugha ya Kigiriki, iliyokuwa inatumiwa na Wakristo wengi wa wakati ule hata mjini Roma.

Pamoja na maandiko mengine kama vile Didake, Waraka wa Barnaba na nyaraka saba za Ignas wa Antiokia iko katika ya maandiko ya kale kabisa ya Ukristo wa kwanza yaliyohifadhiwa nje ya Agano Jipya.

Wataalamu wengi wengi wanahisi ya kwamba iliandikwa kabla ya mwaka 100 BK kwa hiyo miaka michache baada ya vitabu vya mwisho vya Agano Jipya au hata wakati uleule.

Waraka huu mrefu uliendelea kusomwa katika makanisa ya mashariki hadi karne ya 8, ukihesabiwa pengine kati ya vitabu vyenye uvuvio vya Biblia.

Umri wa waraka[hariri | hariri chanzo]

Ndani ya waraka kuna vidokezo kadhaa kuhusu wakati wa kuandikwa kwake hata kama hakuna tarehe kamili - lakini hii ilikuwa kawaida kwa maandiko mengi ya nyakati zile.

Waraka inataja "misiba ambayo imetufikia ghafla na mara kwa mara" na hii inachukuliwa na wataalamu kama marejeo kwa mateso ya Wakristo chini ya Kaisari Domitiano wa Roma mnamo 96-98 BK. Pia kanisa la Roma linaitwa "la kale" na barua inasema ya kwamba wazee waliosimikwa na mitume wa Yesu waliaga dunia tayari.

Sababu ya waraka[hariri | hariri chanzo]

Sababu ya kuandika waraka ilikuwa fitina ndani ya kanisa la Korintho iliyosababisha kuondolewa kwa viongozi kadhaa madarakani. Klementi alipinga fitina hii akitetea viongozi wa awali. Aliwakumbusha Wakorintho kuhusu barua waliowahi kupokea kutoka kwa Mtume Paulo.

Waraka huu ni muhimu kwa sababu inawezesha kupata picha ya hali ya ndani ya jumuia za kwanza za kikristo wakati wake. Kwa mfano waraka inataja vyeo vya "Wazee, maaskofu na mashemasi" ndani ya kanisa la Korintho.

Kanisa Katoliki linaona waraka huu kuwa ushahidi wa mamlaka ya Papa, kwa kuwa humo tunaona Klementi I kuingilia kati kwa nguvu matatizo ya kanisa la mbali, wakati mtume Yohane alipokuwa bado hai na jirani zaidi na Korintho.

Tafsiri ya Kiswahili[hariri | hariri chanzo]

Didakè yaani Mafundisho ya Mitume Kumi na Wawili na Waraka wa Mt. Klementi kwa Wakorinto, tafsiri ya B. Santopadre n.k. – ed. E.M.I. – Bologna 1990 – ISBN 88-307-0321-4

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]