Uzi wa kioo
Uzi wa kioo (kwa Kiingereza: glass fiber, optical fiber) ni uzi mwembamba wa kioo au plastiki ambao unaweza kupitisha nuru kutoka upande mmoja hadi mwingine.
Nyuzi za kioo hutumiwa hasa katika mawasiliano ya simu, lakini hutumiwa pia kwa kuangaza majengo, vifaa vya upimaji, na kamera maalumu za kuangalilia ndani ya nafasi ndogo. Katika tiba huhitajika kuangalia hali ya ndani ya mwili bila upasuaji, kama vile ndani ya mishipa ya damu au ndani ya utumbo.
Kebo ya nyuzi za kioo
[hariri | hariri chanzo]Uzi wa kioo ni ugwe mwembamba na mrefu wa kioo kitupu (SiO2) ambacho ni kiini. Unafungwa katika koti la mata tofauti inayosababisha akisisho kamili la ndani. Hivyo nuru inabaki ndani ya kiini hadi mwisho wa uzi.
Ikiwa koti la ndani linakwaruzwa, linaweza kuvunjika. Hivyo kuna matabaka ya hifadhi nje ya koti hilo yanayolilinda. Yote yanafungwa tena katika koti la nje linalofanya kebo yote imara.
Matumizi
[hariri | hariri chanzo]Matumizi makuu ya nyuzi za kioo ni katika mawasiliano ya simu (telecommunication). Ishara za habari zinapitishwa ndani ya nyuzi hizo, kimsingi sawa na ishara za umeme katika nyaya za shaba. Lakini nyuzi za kioo zinaruhusu kiasi kikubwa zaidi cha ishara kupitishwa (gigabaiti hadi terabaiti kwa sekunde), tena kwa umbali mkubwa zaidi bila amplifaya. Tangu kuanzishwa katika miaka ya 1970, teknolojia ya nyuzi za kioo imeleta mapinduzi katika mawasiliano.