Taswira katika fasihi
Taswira katika fasihi ni maneno ambayo hujenga hali au picha fulani kwenye akili ya hadhira.
Taswira hutokana na matumizi ya lugha anayotumia msanii wa kazi ya fasihi. Matumizi hayo ni kama vile, methali, nahau na tamathali mbalimbali za semi. Wasanii wa fasihi hutumia taswira kama njia mojawapo ya kuficha kile kinachozungumzwa kwa hadhira, yaani hadhira itahitaji kutumia akili ili kuweza kubaini nini msanii huyo amekisema. Lengo kuu la msanii kufanya hivyo ni kuficha maneno ambayo yanaweza kuwa matusi kwa hadhira au kuepusha mgogoro na tabaka analolijadili, hasa akiwa analisema kwa ubaya. Na wakati mwingine taswira hutumika ili kupamba kazi hiyo.
Kwa mfano Said Mohamed katika kitabu Kivuli Kinaishi, jina la kitabu hicho ni taswira tosha inayoonesha jinsi uongozi mbaya unavyoendelea katika nchi za Afrika. Mwandishi amemtumia mhusika Bi Kilembwe kama kiongozi anayeendesha nchi yake kwa kutumia mabavu bila kusikiliza anaowaongoza. Waandishi wengine kama Mohammed Seif Khatib wa kitabu Wasakatonge ametumia taswira mbalimbali katika kazi yake ili kufikisha ujumbe wake kwa hadhira. Taswira hizo ni kama vile, Jiwe si mchi, Wasakatonge na kadhalika.
Aina za taswira
Taswira zinaweza kugawanyika katika aina mbalimbali. Aina hizo ni:
(i) Taswira hisi
Hii ni taswira ambayo huhusika na hisi ya ndani. Taswira hii huweza kumfanya msomaji au msikilizaji awe na wasiwasi, aone woga, apandwe na hasira au asikie kinyaa. Taswira hii huwa na nguvu kubwa ya kuganda akilini.
Kwa mfano: Akaniambia, “siwezi kula chakula hicho rojorojo mfano wa kohozi lenye sumu”.
Angazia taswira hizi: taswira muonjo na taswira mguso.
(ii) Taswira ya mawazo / kufikirika
Ni taswira inayotokana na mawazo. Mawazo hayo ni yale yanayohusu mambo yasiyoweza kuthibitika. Mambo hayo ni kama vile:
- Kifo
- Njaa
- Uchungu
- Raha na kadhalika.
Kwa mfano: Kifo! Kifo! Umetufanya nini sasa, mpaka unaamua kutuchukulia ndugu yetu?
(iii) Taswira zionekanazo
Hii ni taswira ambayo hujengwa kwa kutumia vielezo tunavyovijua au vile vinavofahamika katika maisha ya kila siku.
Kwa mfano: “Haikupita dakika mijusi miwili ilipita mbele yetu. Midomo yao ilikuwa myekundu, ghafla walikutana na nyoka aliyeonekana mnene tumboni. Hapana shaka alikuwa amekula mnyama”.
Makala hii kuhusu mambo ya fasihi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Taswira katika fasihi kama historia yake, uenezi au maendeleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |