Nenda kwa yaliyomo

Singeli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Msaga Sumu akitumbuiza.

Singeli (vilevile: Sengeli) ni aina ya muziki maarufu sana katika maeneo yanayokaliwa na Waswahili au watu wa Pwani nchini Tanzania. Singeli huchukuliwa kama "mchiriku" au "mnanda" wa kisasa. Muziki huo ni muunganiko wa miziki ya Taarab, Bongo Flava, mchiriku na Vanga (mdundiko) la Kizaramo ndilo limezaa muziki huu.

Muziki huo hupigwa sana katika shughuli za harusi au maulidi - hasa hukesha maarufu kama "vigodoro". Mwanzilishi wa mtindo huo ni Msaga Sumu.

Tafiti za hivi karibuni zinaonesha ya kwamba muziki wa singeli unakua na kuenea kwa kasi kubwa sana hasa jijini Dar es Salaam ambapo wasanii wengi wanaoimba muziki huo wanapatikana.

Muziki huo ulianza miaka ya 2010 huku ukionekana kama ni muziki wa kuiga hivyo kuufanya ukue kwa tabu kwa kipindi hicho, umekamata hatamu katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam na sehemu nyingine nchini Tanzania.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 66.8 ya Watanzania wanaufahamu muziki huo na wanausikiliza kwa njia tofauti ikiwepo redio, kuweka katika simu, flash na kupiga katika sherehe mbalimbali zinazofanyika katika jamii ya Watanzania.

Singeli ilianza kwa kuwa na wasanii wachache lakini aliyekuwa anasikika sana alikuwa Msaga Sumu aliyetamba na nyimbo zake kama ‘Naipenda Simba’ na nyingine nyingi ambazo zilitamba na zinaendelea kutamba mpaka sasa katika sherehe mbalimbali nchini.

Tangu uwepo wa Msaga Sumu katika muziki huo, sasa wameibuka wasanii wengine wengi ambao wanafanya vizuri kiasi cha kuufanya muziki wa Bongo Flava kuwa hatarini katika vigodoro au sherehe mbalimbali.

Muziki huo ambao hauna ulazima wa msanii kuingia studio na kurekodi mara nyingi wasanii hao hutumia beats za nyimbo nyingine kisha wanafanya mixing zao kisha wanatumia katika nyimbo zao.

Aidha, katika sherehe, kama kumtoa mtoto (vibeseni), ndoa na sikukuu za kidini muziki huo ndio unapigwa kwa asilimia 95 ukilinganisha na muziki mwingine kama nyimbo za Injili, dansi na bongo fleva. Hivyo basi miaka ijayo muziki wa singeli utakuwa juu zaidi ya muziki wa aina nyingine nchini Tanzania kwani hata redio na vyombo vya habari vingine vimeupokea vizuri muziki huo mfano mzuri ni radio EFM.[1] Baadaye vikaanza vyombo vingine kuupiga muziki huo, japo kuna baadhi ya jamii inauona kama ni muziki wa kihuni sababu ya maneno yanayotumika.

Pia ndani ya muziki wa singeli kuna pande mbili yaani:

  • singeli ladha ambayo huimbwa sana kwa hisia pia na taratibu sana
  • singeli michano, maarufu kama singeli bakora, ambayo huimbwa kwa kuwarusha watu na kwa mwendo kasi au kwa haraka haraka.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. "Singeli katika blogu ya Hivi-Sasa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2018-06-14. Iliwekwa mnamo 2016-07-21.
Makala hii kuhusu mambo ya muziki bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Singeli kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.