Nyaraka (Biblia)
Nyaraka ni mtindo wa uandishi ulio maarufu hasa kutokana na zile zilizomo katika Biblia ya Kikristo.
Katika Agano Jipya
[hariri | hariri chanzo]Kati ya vitabu 27 vya Agano Jipya, 21 vina mtindo wa barua au nyaraka. Hiyo ni tofauti kabisa na Agano la Kale, ambamo vitabu kadhaa vinazileta, lakini si kitabu kizima hata kimoja.
Paulo ndiye aliyetumia zaidi mtindo huo ili afikie na ujumbe na mamlaka yake pale asipoweza kufikia kimwili.
Barua 14 zinahusishwa na yeye kwa namna moja au nyingine, wakati nyingine 7 zinahusishwa na Yakobo, Petro, Yohane na Yuda. Hii haina maana kwamba ziliandikwa zilivyo na Mitume hao.
Kwanza, tokea awali watu waliweza kuandika barua kwa mkono wao, au kwa kumuongoza karani aandike maneno yao wenyewe, au kwa kumpa maelekezo ya jumla kuhusu namna ya kuandika kama si kumuachia aandike anavyoona inafaa.
Zaidi ya hayo, wakati wa Mitume ilikuwa kawaida kuandika kwa kutumia jina la marehemu fulani maarufu kama kwa kumwezesha aendelee kutoa ujumbe aliokuwa anautoa maishani. Pengine aliyeandika hivyo alikuwa na uhusiano wa pekee na marehemu huyo kama mwanafunzi au mwandamizi wake.
Pengine maandishi hayo hayakuwa tu barua fupi za kuwasiliana kuhusu shida fulani, bali hati au insha ndefu kuhusu mada fulani: ndizo zinazostahili kuitwa nyaraka.
Ingawa tofauti kati ya barua na waraka inaeleweka kinadharia, pengine ni vigumu kugawa vitabu hivyo vya Agano Jipya katika makundi mawili: kwa hakika Eb ni waraka na 3Yoh ni barua, lakini nyingine ziko katikati.
Barua saba zisizohusishwa na Paulo zinaitwa Katoliki, maana zimekubaliwa na Kanisa lote, ingawa maana asili ya neno hilo ilikuwa kwamba ni kwa ajili ya watu wote, jambo ambalo si kweli.
Katika Biblia barua hazikupangwa kufuatana na tarehe za kuandikwa, bali zinatangulia zile za Paulo, na kati ya hizo zinatangulia zile kwa makanisa 7, zinafuata zile kwa watu binafsi 3 na mwisho waraka kwa Waebrania ambao haumtaji Paulo. Ndani ya makundi hayo, zinatangulia zile ndefu zaidi hadi zile fupi.
Sisi, tukitaka kuelewa zaidi ujumbe na maendeleo yake, ni afadhali tuzisome kwa mpangilio wa tarehe kadiri tunavyoweza kuikadiria.
2Pet, ambayo inafikiriwa kuwa ya mwisho kuandikwa, inashuhudia kwamba tayari barua za Paulo zilikuwa zimekusanywa na kuheshimiwa kama Maandiko Matakatifu.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Catholic Encyclopedia: Epistles