Mtumiaji:Dee Soulza/1"
Changamoto Zinazokikabili Kiswahili
[hariri | hariri chanzo]Kiswahili ni moja ya lugha kumi maarufu zinazozungumzwa zaidi barani Afrika ambayo asili yake ni lugha za asili za makabila ya Wabantu wa Afrika ya Mashariki. Haiba hiyo ya Kiswahili imewekwa bayana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwenye uzinduzi wa Siku ya Kiswahili Duniani, Julai 7, 2023[1] Mwaka 2024, Umoja wa Afrika umekitangaza Kiswahili kuwa ni moja ya lugha zake rasmi za kiutendaji[2]. Hatua hiyo imefikiwa baada ya lugha hiyo kupiga hatua zingine kama hiyo: Kuwa miongoni mwa lugha rasmi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika[SADC] hali kadhalika Jumuiya ya Afrika Mashariki [EAC].
Wakati hadhi ya Kiswahili ikiongezeka, wadau wa lugha hiyo wamebaini changamoto mbalimbali zinazoikabili[3] Katika makala yake ya Februari 15, 2024 iitwayo Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Umoja wa Afrika: kunatoa fursa gani kwa Wazungumzaji wake? Idhaa ya Kiswahili ya BBC ilitoa kauli kuwa 'kuna haja ya tahadhari' [juu ya yale yanayokikwaza Kiswahili]. BBC ikataja changamoto kadha ambazo zinaongezea kwenye orodha ya changamoto za lugha hiyo. Kwenye makala hiyo, Mohammed Abdulrahman alisema, baadhi ya wazungumzaji wa kiswahili huondoa maneno asilia ya Kiswahili na kuweka maneno mengine yasiyokidhi kwa sababu tu za kisiasa ama utashi binafsi.
Wadau wameitaja pia changamoto ya matumizi mabaya ya maneno ya Kiswahili. Daktari Nasra Habibu wa Idara ya Mafunzo ya Lugha na Fasihi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania [OUT][4] akihojiwa na mwandishi wa habari, aligusia juu ya kubanangwa kwa Kiswahili[5]. Maneno kutamkwa vibaya na hata kubadilishiwa maana. Kuna mifano mingi ya matumizi yaso sahihi ya maneno. Neno sura kutumika mahala pa neno uso , kama 'nitaificha wapi sura yangu' badala ya nitauficha wapi uso wangu'. Watu wanasahau kuwa sura ni jinsi uso ulivyoumbika (mbaya au mzuri) na uso ndiyo sehemu ya mbele ya kichwa imebayo viungo mbalimbali. Matumizi ya maneno binti na msichana pia yanakanganywa: 'Yule binti ni mstaarabu sana'; itakuwa ni kauli sahihi kama mzungumzaji ana nafasi ya mzazi kinasaba kwa mzungumziwa. Neno sahihi ni msichana.
Ingizo la 29 la Methali za Kiswahili kwenye tovuti ya Scribd, linatupa mfano wa methali ambayo maana yake imebadilisnwa[6]. Kufa kufaana ina maana ya ' wakati wa shida jamii husaidiana ' (ndugu na jamaa kuwasaidia wafiwa) na sio ' afapo mtu kunapatikana fursa mbalimbali. Hali kadhalika, baadhi ya methali zinabadilishiwa maumbo yao ya asili; kwa mfano, ' mali bila daftari hupotea bila habari'. Baadhi ya watu husema ' mali bila daftari hupungua bila habari.'
Changamoto nyingine inayotajwa ni ile ya baadhi ya maafisa wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)[7] kunadi misamiati na mabadiliko ambayo yanaleta changamoto kwenye sifa ya lugha kujiumba yenyewe. Mfano mzuri ni pale afisa anapoutangazia umma kupitia vyombo vya habari kuwa si sahihi kusema bahati mbaya kwani bahati haiwezi kuwa mbaya. Kilichosahaulika ni kuwa kirai hicho kina maana ya kinahau na hakipaswi kufasiliwa kwa kuchambua maana za neno mojamoja yanayokiumba. ' Isivyo bahati' aliyoipendekeza, kisawe chake cha Kiingereza ni unfortunate au unlucky na si bad luck[8].
visawe vya bahati mbaya katika lugha nyinginezo za kimataifa ni: bad luck (Kiingereza), haza sayi (Kiarabu), chance ya mabe/makila mabe (Kilingala), emikisa emibi (Luganda), mal chance (Kifaransa), mala suerte (Kihispaniola) na mà sorte (Kireno).Lugha zote hizo zinasema ' bahati mbaya ' katika kirai cha maneno mawili.[9]
Athari zinazotokana na waandishi wasio na weledi wa kutosha kwenye Kiswahili, ni changamoto nyingine. Daktari Kamfipo Gideon, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliiangalia changamoto hii kwa ukaribu zaidi kwenye utafiti wake, kisha akaja na majibu kuwa kufanya usaili wa kina wakati wa kuajiri waandishi wa vyombo vya Kiswahili haitoshi. Waweke pia sera thabiti za kuwaendeleza waandishi wao kwenye taaluma ya Kiswahili[10].
Changamoto nyingine inaletwa na athari ya waandishi wasio rasmi wanaoanikiza maudhui yao kupitia mitandao ya kijamii, tovuti, blogu, na kadhalika. Maudhui ya waandishi hao hayalazimiki kupitia kwa mhariri yeyote. Kwa namna hiyo, kunakosekana fursa ya kusahihishwa na kuhakikishwa kwa ubora wa Kiswahili kilichotumika. Athari zinamfikia msomaji moja kwa moja.
Wadau wameanikiza changamoto na wadau haohao bado wana kazi ya kufanya: kupanga mikakati na kuweka mipango ya kukabiliana na changamoto hizo[11]. Mikakati itakayowekwa ikidhi kwenye kukikinga Kiswahili dhidi ya kubanangwa na hata kukipa afueni juu ya madhila yaliyokikumba.
- ↑ World Kiswahili language day". unesco.org/en. 24 May 2023. Archived from the original on 27 June 2023. Retrieved 5 April 2024.
- ↑ "Kiswahili chapitishwa kuwa Lugha ya Kazi ya Umoja wa Afrika | Embassy of Tanzania in Addis Ababa, Ethiopia". www.et.tzembassy.go.tz. Iliwekwa mnamo 2024-04-29.
- ↑ Journals
- ↑ University of Tanzania, Open (January 16, 2021). "Department of Languages and Literary Studies". out.ac.tz. Archived from the original on March 25, 2023. Retrieved April 15, 2024
- ↑ Welle, Deutsche (19 March 2024). "Kongamano la nne la idhaa za Kiswahili duniani". www.dw.com. Retrieved 5 April 2024.
- ↑ https://www.scribd.com/document/249714623/Swahili-Proverbs-2
- ↑ Tanzania, Baraza la Kiswahili (November 17, 2018). "BAKITA Home". bakita.go.tz. Archived from the original on May 11, 2021. Retrieved April 20, 2024.
- ↑ UDSM, TUKI (2006). ENGLISH - SWAHILI DICTIONARY [Dictionary] (3rd ed.). Shanghai Kangshi: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. p. 946. ISBN 9976-911-29-7.{{cite book}}: CS1 maint: date and year (link)
- ↑ Google Translate
- ↑ Journals, University of Dar Es Salaam (July 30, 2020). "English Features in Kiswahili Social Media". Utafiti Journal. 14 (1). Archived from the original on August 10, 2022. Retrieved April 16, 2024.
- ↑ Minja, Dativa (2023-03-21). "Tanzania: PM Tasks Stakeholders to Promote Kiswahili". Tanzania Daily News. Retrieved 2024-04-05 – via All Africa.