Nenda kwa yaliyomo

Msambara

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Kata ya Msambara
Nchi Tanzania
Mkoa Kigoma
Wilaya Kasulu Mjini
Idadi ya wakazi
 - Wakazi kwa ujumla 23,610

Msambara ni kata ya Wilaya ya Kasulu Mjini katika Mkoa wa Kigoma, Tanzania, yenye msimbo wa posta 47307.

Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi wa kata walihesabiwa kuwa 23,610 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 22,391 waishio humo.[2]

Eneo la Msambara

[hariri | hariri chanzo]

Kata ya Msambara inaundwa na vijiji viwili vya Msambara na Kabanga. Kata hii iko kaskazini Mashariki mwa mji wa Kasulu ambao ndiyo makao makuu ya wilaya ya Kasulu. Barabara kuu ya kutoka Kigoma kupitia Kasulu kwenda mikoa ya Mwanza, Kagera na Shinyanga kupitia Kahama inapita umbali wa km 4 kutoka Msambara.

Vijiji vya kata hii vilianzishwa wakati wa operesheni kijiji ya mwaka 1973.

Vijiji hivi vinazungukwa na milima upande wa Magharibi mlima Mgunga na Kaskazini Mashariki kuna mlima Chanza.

Vijiji hivi viko katika bonde la mito mitatu, kwa majina ni:

1. mto Ruchugi unaopita kuanzia kaskazini mashariki mwa kijiji cha Msambara, kupitia mashariki mwa kijiji hiki na kuelekea kusini mwa kijiji hiki na kupeleka maji yake katika mto Malagarasi ambapo makutano ya mto Ruchugi na Malagarasi yako Uvinza karibu na kiwanda cha chumvi;

2. Mto Kashenyi unapita kati ya vijiji hivi viwili lakini ukiegemea sana upande wa Kabanga na unapeleka maji yake katika mto Ruchugi;

3. mto Kabanga ambao unaanzia Heru Juu upande wa kijiji cha Mganza na unapita kuanzia Kaskazini Magharibi ya kijiji cha Kabanga kuelekea Mashariki ya kijiji hiki. Mto huu unapeleka maji yake katika mto Kashenyi na hatimaye mto Ruchugi.

Vijiji vinavyopakana na kata hii ni Buhoro, Mwanga na Shunga upande wa Kaskazini, Kanazi na Mubondo upande wa Mashariki, mji wa Kasulu, kijiji cha Kidyama na Ruhita upande wa Kusini na Mganza na Karunga upande wa Magharibi.

Hali ya hewa na kilimo

[hariri | hariri chanzo]

Uoto wa asili wa eneo hili ni wa kitropiki, ambao una majani marefu, misitu ya miombo na mvua za wastani kwa mwaka. Majira ya mvua katika eneo hili ni kuanzia mwezi Oktoba hadi mwezi Aprili. Aidha hali ya hewa ya kata hii ni vipindi vya joto kuanzia mwezi wa Julai katikati hadi mwezi Januari; kuanzia mwezi Februari hadi Juni/Julai katikati kunakuwa na baridi. Kwa kawaida joto huanzia nyuzi 15 sentigredi wakati wa baridi hadi nyuzi 34 wakati wa joto.

Wakazi wa kata hii hujishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula kama vile mahindi, maharage, kunde, mbaazi, mhogo, viazi vitamu na viazi mviringo, magimbi n.k. Shughuli hizi hufanyika katika mabonde ya mito Ruchugi, Kashenyi, Nyakai, na mto Kabanga kwa njia ya umwagiliaji wakati wa kiangazi; hali kilimo cha kutegemea mvua hufanyika katika maeneo yaliyo katika mabonde ya mito mahali ambapo mito haipiti wakati wa mafuriko na katika maeneo yaliyo katika miinuko ya milima.

Pia wenyeji wa kata hii hufuga wanyama kama ng'ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe kwa kiasi kidogo, mbwa, paka, kuku, bata, na sungura.

Kata hii ina misheni mbili, moja ya Kanisa Katoliki iliyoko Kabanga na nyingine ya Wapentekoste iliyoko Msambara; misheni hizi zilianzisha makanisa ya madhehebu hayo, shule za msingi na zahanati.

Kwa upande wa misheni ya Kabanga ilianzisha karakana ya ufundi mitambo (mechanics), useremala na stadi nyingine mbalimbali za kazi. Kwa upande wa misheni ya Msambara, iliyoanzishwa mwaka 1933 chini ya wamisionari wa Sweden, chuo cha mafunzo ya stadi za kazi kilianzishwa miaka ya 1980. Pia kuna chuo cha wauguzi katika hospitali ya misheni hiyo.

Hata hivyo katika miaka ya mwisho ya 1980 na miaka ya mwanzoni ya 1990 madhehebu mengine zaidi yameingia katika kata hii: Assemblies of God, Anglikana, Baptisti, Wasabato na Evangelical Assemblies of God; hivyo kuwapa wakazi wa kata hii uwanja mkubwa wa kuchagua wapi wakafanyie ibada zao.

Kata hii ilianza na shule mbili za msingi (shule ya msingi Msambara na shule msingi Kabanga). Kwa upande wa Kabanga misheni hii ya Wakatoliki ilianzisha shule ya msingi ya watoto wenye ulemavu, wakati huo watoto wasioona (vipofu) waliandikishwa na kusoma hapo ambapo wengine wameweza kufaulu mitihani yao na kuingia shule za sekondari kama vile Mzumbe Secondary, Mpwapwa n.k.

Huduma nyingine zinazopatikana kwenye kata hii ni pamoja na chuo cha ualimu Kabanga, shule ya sekondari MKA ambayo ni ya kata ya Msambara.

Viongozi

[hariri | hariri chanzo]

Viongozi waliowahi kuongoza kijiji cha Msambara ni Samweli Nyamwali (wakati wa kuanzishwa kijiji hadi 1977), Amos Mutwe (1977 - 1982), Saidi Nsindagi Nkanyagu 1983 - 1987 na 1993 - 1997, Yakobo Ntarumanga 1987 -1992 na Yona Mayila 1997 - 2002, Saidi Nsindagi 2002 - 2007.

Kata za Wilaya ya Kasulu Mjini - Mkoa wa Kigoma - Tanzania

Heru Juu | Kasulu Mjini | Kigondo | Kimobwa | Kumsenga | Kumnyika | Msambara | Muganza | Muhunga | Murubona | Murufiti | Murusi | Mwilamvya | Nyansha | Nyumbigwa | Ruhita


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Kigoma bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Msambara kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.