Nenda kwa yaliyomo

Kituo cha Angani cha Kimataifa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
ISS mnamo mwaka 2010

Kituo cha Angani cha Kimataifa (kwa Kiingereza International Space Station, ISS) ni satelaiti inayozunguka Dunia katika kwenye umbali wa takriban kilomita 400 juu ya uso wa ardhi. ISS ilianzishwa kutokana na mapatano baina ya mamlaka za usafiri wa angani za NASA (Marekani), Roskosmos (Urusi), ESA (Umoja wa Ulaya), Japani na Kanada.

Ujenzi wa kituo

[hariri | hariri chanzo]

Kilianza kujengwa kwa kuunganisha sehemu zilizobebwa angani kwa roketi tangu Novemba 1998. Sehemu ya kwanza ilikuwa kitengo cha Kirusi chenye injini na nafasi ya kutunz\ na wanaanga. Sehemu zilizofuata na kuunganishwa na kiini hiki zilibebwa kwa feri ya anga Space Shuttle ya Marekani na roketi za Kirusi. Tangu mwisho wa mradi wa Space Shuttle safari zote zinategemea roketi za Kirusi.

Tangu mwaka 2011 ukubwa wake ni mnamo mita 110 x 100 x 30. Kinazunguka Dunia kila baada ya dakika 92. Kuna mpango wa kuongeza kitengo cha Kirusi cha maabara katika mwaka 2019.

Tangu mwaka 2000 kinakaliwa na timu za wanaanga 2-3 wanaokaa kwa zamu za miezi kadhaa hadi kubadilishwa na kundi jipya. Mwanaanga mmoja huteuliwa kukaa kwa muda zaidi. Timu ya kwanza ya wanaanga (Warusi 2 na Mwamerika 1) ilifika mwaka 2000.

Kimsingi umbo la ISS ni mcheduara kama bomba refu lililounganishwa kutokana na vipande mbalimbali. Nje ya bomba refu kuna mikono mikubwa inayobeba paneli za sola zinazozalisha umeme unaohitajika kwa kazi ya vifaa na mashine za kituo. Mikono mingine inabeba rejeta zinazohitajika kupoza joto linalopokewa na upande wa kituo kinachoangazwa na Jua.

Nyongeza nyingine nje ya silinda kuu ni antena na vyumba vya maabara vilivyoongezwa kando.

Mipango ya kuondoa kituo kwenye anga

[hariri | hariri chanzo]

Kwa sasa imepangwa kutumia kituo hadi mwaka 2024. Imepangwa kuangusha kituo duniani kwa kulenga maeneo ya kusini ya Bahari ya Pasifiki. Kuna uwezekano kutumia vyombo vya anga vinavyosukuma kituo kuelekea panapotakiwa.

Shughuli kwenye ISS

[hariri | hariri chanzo]

Kusudi kuu la kituo ni kuwa na maabara katika anga-nje. Katika mazingira yasiyo na graviti kuna nafasi ya kufanya majaribio mengi katika fani za biolojia, fizikia, kemia, tiba na astronomia. Kituo hiki kinabeba vifaa vinavyopima mnururisho wa mialimwengu (ing. cosmic rays) au mabadiliko ya nuru ya Jua.

Kuitazama kutoka duniani

[hariri | hariri chanzo]

Kutoka duniani ISS inaonekana kama nukta ya mwanga inayotembea polepole angani ikiangazwa na Jua na kuakisi nuru yake. Inaweza kuonekana katika masaa baada ya machweo na kabla ya kuchomoza kwa jua.[1] ISS inachukua kama dakika 10 kupita kutoka upeo mmoja kwenda mwingine, na inaonekana tu sehemu ya wakati huo kwa sababu ya kuingia ndani au nje ya kivuli cha Dunia. Kwa sababu ya ukubwa wa uso wake, ISS ndiyo satelaiti inayong'aa zaidi angani ikilingana na mwangaza unaoonekana wa −4, sawa na Zuhura. Wakati mwingine mwangaza wake unaweza kuwa mkali zaidi, hadi kufikia mara 8 au 16 mwangaza wa Zuhura. [2] [3]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
  • Reference Guide to the International Space Station (PDF) (tol. la Utilization). NASA. Septemba 2015. NP-2015-05-022-JSC.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Reference Guide to the International Space Station (PDF) (tol. la Assembly Complete). NASA. Novemba 2010. ISBN 978-0-16-086517-6. NP-2010-09-682-HQ.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
Makala hii kuhusu mambo ya teknolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hiyo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

  1. Price, Pat (2005). The Backyard Stargazer: An Absolute Beginner's Guide to Skywatching With and Without a Telescope. Gloucester, MA: Quarry Books. uk. 140. ISBN 978-1-59253-148-6.
  2. "Artificial Satellites > (Iridium) Flares". Calsky.com. Iliwekwa mnamo 1 Mei 2012.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. "How to Spot the International Space Station (and other satellites)". Hayden Planetarium. Iliwekwa mnamo 12 Julai 2011.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)