Kaini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kaini na Abeli, mchoro wa karne ya 15 kutoka kitabu cha Ujerumani Speculum Humanae Salvationis.

Kaini kadiri ya Biblia ni jina la binadamu wa kwanza kuzaliwa na kuua.

Katika kitabu cha Mwanzo[hariri | hariri chanzo]

Kadiri ya kitabu cha Mwanzo (Biblia) katika Agano la Kale wana wawili wa kwanza wa Adamu na Hawa, majina yao Kaini na Habili, walitunza imani yao kwa Mungu wakamtolea sadaka.

Habili aliitoa katika wanyama bora wa kundi lake, akiwa na hali ya unyenyekevu na imani, naye Mungu akampokea.

Tabia ya Kaini ilikuwa ya kiburi, bila ya kumcha Mungu, kwa hiyo Mungu alimkataa (4:1-5; taz. Ebr 11:4; 1 Yoh 3:12).

Tabia na maisha ya watoaji wa sadaka ina maana kuliko vitu wanavyovitoa, kwa hiyo Mungu alimwambia Kaini kuwa, akitaka Mungu ampokee, angepaswa kushinda dhambi iliyokuwa ikitaka kumwangamiza. Dhambi hiyo ilikuwa kama mnyama wa mwitu ajikunjaye na kuotea mlangoni, ili aweze kumshambulia mtu akitoka nje (4:6-7).

Kaini hakushinda dhambi yake, na katika hasira ya wivu alimwua Habili. Tendo lake la kutwaa uzima wa ndugu yake lilidai kisasi kwa Mungu aliyetoa uhai ule. Kwa hiyo Mungu alimfukuza Kaini aende mbali na mahali walipoishi watu wengine.

Ingawa Kaini alidumu katika hali ya kutotubu, Mungu katika huruma yake kubwa alimlinda asiuawe kwa kisasi (4:8-16).

Maendeleo ya dhambi baada yake[hariri | hariri chanzo]

Baadaye historia ya wokovu inaonyesha kulikuwa na maendeleo ya ufugaji wa kondoo na ng'ombe, pia kulikuwa na maendeleo ya ufundi na utamaduni, lakini kwa upande wa maadili watu walizidi kuwa waovu.

Lameki, licha ya kumwua kijana kwa ajili ya kumwumiza kidogo, alitunga wimbo uliotukuza ukatili wake. Kaini alikuwa afadhali kidogo. Alitafuta na alipata kinga fulani ya Mungu, asije akauawa kwa kisasi, lakini Lameki hakujali jambo lo lote, akatisha sana, mtu asije akathubutu kumdhuru (4:19-24).

Baada ya mambo hayo, wazao wa Kaini hawaonekani tena katika habari za Biblia. Kuanzia hapo masimulizi yanaendelea na habari za wazao wa mwana mwingine wa Adamu, Sethi, kwa sababu walikuwa wale walioendelea kumwabudu Mungu (25-26).

Adamu na Hawa walizaa watoto wengi, wa kiume na wa kike (taz. 5:4), kwa sababu sehemu ya wajibu wao ilikuwa kusaidia kujaza dunia (taz. 1:28). Katika muda wa miaka mingi makabila mbali mbali ya watu yalipatikana, na watu wale walifanya makao yao mahali tofauti.

Lakini Biblia inashughulika na historia inayoendelea na sehemu ndogo tu ya wanadamu wote, yaani wale waliotokana na watoto wa Shemu, ambao Waebrania walikuwa wametokana nao.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Marejeo mengine[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu: