Futa Djalon

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Sehemu za juu za Futa Djalon

Fouta Djalon (pia: Futa Jalon, Futa Djallon) ni eneo la milima nchini Guinea (Afrika ya Magharibi). Huitwa pia "Guinea ya Kati" (Kifaransa Moyenne Guinée, zone du Fouta Djalon). Makao makuu ya eneo ni mji wa Labé.

Sehemu kubwa ya nyanda hizi za juu ni nchi ya manyasi na misitu penye vilima vinavyofuatana kwa kimo cha wastani cha mita 900 UB. Sehemu ya juu ni mlima Joura mwenye kimo cha mita 1,515m (4,970ft). Mmomonyoko wa maji umekata mabonde marefu katika mwamba wa juu.

Fouta Djalon hupokea mvua nyingi na hivyi mito mitatu mikbwa ya Afrika ya Magharibi ina chnazo hapa ni Mto Niger, Mto Gambia na mto Senegal. Kwa hiyo huitwa tangi ya maji kwa sehemu hii ya Afrika.

Wakazi asilia ni wakulima Wafulbe; lahaja yao ya Futa Djalon huhesabiwa kama lugha ya kitaifa ya Guinea.

Tangu karne ya 18 milima hii ilikuwa kitovu cha ufalme au usultani wa Kiislamu. Waislamu walianzisha vita ya jihadi dhidi ya wafuasi wa dini asilia wakaanzisha dola la kidini. Mtawala aliitwa "Almami" (kutoka Kiarabu Al Imami). Almami wa mwisho, Bubakar Biro, alishindwa na Wafaransa mnamo 1896 kwenye mapigano ya Poredaka nchi ikawa shemu ya koloni ya Kifaransa.