Nenda kwa yaliyomo

Elon Musk

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Musk mnamo mwaka 2015

Elon Reeve Musk (* Pretoria, Afrika Kusini, 28 Juni 1971) ni mhandisi na mjasiriamali anayeishi Marekani.

Amekuwa maarufu kama mwanzilishi wa huduma ya Paypal na mkuu wa kampuni ya magari ya umeme Tesla na kampuni ya roketi za anga SpaceX. Anamiliki pia makampuni mengine ya kiteknolojia.

Ana uraia wa Afrika Kusini, Kanada na Marekani[1].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Baba yake Errol ni mzawa wa Afrika Kusini aliyefanya kazi ya mhandisi, mama yake Maye alikuwa mhamiaji katika Afrika Kusini kutoka Kanada[2]. Elon ana kaka na dada mdogo. Alimaliza A-level zake kwenye Pretoria Boys High School.

Alianza kutumia kompyuta akiwa mtoto wa miaka kumi; alipokuwa na miaka 14 alitunga mchezo wa kompyuta aliyoweza kuuza kwa jarida moja[3].

Baada ya kumaliza shule ya sekondari Elon Musk alihamia Kanada kwa sababu alitaka kuepukana na huduma ya kijeshi katika Jeshi la Afrika ya Kusini (wakati ule bado chini ya siasa ya apartheid).

Alianza masomo ya juu kwenye Queen’s University akaendelea pale Marekani kwenye Chuo Kikuu cha Pennsylvania alipopokea shahada ya awali katika uchumi na fizikia. Mwaka 1995 alipokewa kwenye Chuo Kikuu cha Stanford, Kalifornia kwa kozi ya uzamivu kwenye fani ya fizikia.

Ujasiriamali[hariri | hariri chanzo]

Musk alianzisha makampuni mbalimbali akisema lengo lake ni hasa kuhakikisha uhai wa binadamu uweze kudumu katika miaka inayokuja. Kati ya makampuni yaliyokuwa maarufu hasa kuna yafuatayo.

Zip2[hariri | hariri chanzo]

Baada ya siku chache katika Stanford Musk aliamua kuachana na masomo na kuunda kampuni ya Zip2 iliyoorodhesha makampuni na maduka katika intaneti pamoja na nafasi yao kwenye ramani ya miji.[4].

Paypal[hariri | hariri chanzo]

Zip2 iliuzwa kwa kampuni kubwa ya Compaq kwenye mwaka 1999 na Musk alipata milioni za dollar 22 alizotumia kuunda biashara mpya iliyokuwa benki ya intaneti. Baada ya muda mfupi benki hii iliendelea kuwa huduma ya Paypal inayowezesha wateja kufanya malipo kupitia intaneti. Haraka sana Paypal iliendelea kuwa njia ya malipo inayotumiwa zaidi kwenye viwanja vya malipo dijitali kama eBay. Musk hakukubaliana na viongozi wengine kuhusu maendeleo ya kampuni akaondolewa katika nafasi ya mkurugenzi mkuu mwisho wa mwaka 2000 lakini aliendelea kushika asilimia 11 za hisa. Mwaka 2002 Paypal ilinunuliwa na eBay kwa dollar bilioni 2.1 ilhali Musk alipokea sehemu yake ya dollar milioni 165.

SpaceX[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kuondolewa katika ukurugenzi wa eBay Musk aliona maana ya kuboresha usafiri wa anga-nje. Mwaka 2001 alitunga mpango wa kuanzisha kituo cha "Mars Oasis" kwenye sayari ya Mirihi[5] akajaribu kununua roketi kubwa nchini Urusi. Alipoona bei zilikuwa juu mno alianza kutafakari uwezekano wa kuunda roketi mwenyewe akikadiria ya kwamba roketi zilizotengenezwa na taasisi za kiserikali kama NASA zilikuwa ghali mno.

Baada ya kupokea mapato kutokana na hisa za Paypal aliwekeza pesa yake katika kampuni mpya ya "Space Exploration Technologies" (teknolojia za utafiti wa anga-nje), kifupi SpaceX. Kampuni hii ililenga kutengeneza roketi zinazoweza kupeleka mizigo kama satelaiti na baadaye pia watu kwenye anga-nje. Musk aliamua kuunda roketi inayoweza kutumiwa mara kadhaa badala za roketi zilizofaa kwa safari moja pekee jinsi ilivyokuwa kawaida.

SpaceX ilifaulu mwaka 2008 mara ya kwanza kufikia anga-nje kwa roketi ya Falcon 1 ikiendelea kubeba satelaiti katika obiti ya nje. Gharama ni takriban theluthi 1 tu ya roketi za kawaida kwa sababu sehemu kubwa ya roketi inaweza kurudi duniani na kutumiwa tena.[6]. Roketi nyingine ni Falcon 9 na Heavy Falcon, kuna pia chombo cha angani cha SpaceX Dragon inayopeleka mizigo kutoka duniani kwenda Kituo cha Anga cha Kimataifa. Mwaka 2019 aina mpya ya Dragon itasafirisha pia wanaanga kwenda Kituo cha Anga cha Kimataifa.

Tesla[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 2004 Musk aliamua kuwekeza dollar milioni 6.5 katika kampuni changa ya Tesla Motors iliyolenga kutengeneza magari ya umeme akawa mwenyekiti wa bodi ya Tesla.

Katika miaka iliyofuata Musk aliendelea kuwekeza tena na tena jumla ya dollar milioni juu ya 20 katika Tesla. Tangu 2008 amekuwa mkurugenzi mkuu.

Tesla imeanza kutengeneza na kuuza magari ya umeme yanayopatikana kwa kiasi cha dollar 35,000.

SolarCity[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 2004 Musk alihamasisha binamu zake Lyndon Rive na Peter Rive kuanzisha SolarCity ambayo ni kampuni ya teknolojia ya umemejua. Inatengeza paneli za umemejua pamoja na vifaa vya kudhibiti chaji na kuziweka kwenye majengo ya watu na makampuni. SolarCity imenunuliwa na Tesla.

Familia[hariri | hariri chanzo]

Musk alioa mara mbili lakini ndoa zake ziliishia na talaka. Ana wana watano kutoka ndoa yake ya kwanza waliozaliwa mwaka 2004 na 2006.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. AliMughal (2019-06-18). "Elon Musk Biography, Age, Height, Wife, Family & More". BioExposed (kwa American English). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2019-07-01. Iliwekwa mnamo 2019-07-20.
  2. Elon Musk Archived 9 Machi 2019 at the Wayback Machine., tovuti ya saentrepreneurs.co.za, iliangaliwa Machi 2019
  3. Elon Musk (Tesla, SpaceX): génie ou prédateur de la Silicon Valley?, tovuti ya Nouvel Observateur ya 22-12-2015]
  4. Entrepreneur of the Year, 2007: Elon Musk Archived 29 Septemba 2020 at the Wayback Machine., tovuti ya inc.com ya mwaka 2007, iliangaliwa Machi 2019
  5. MarsNow 1.9 Profile: Elon Musk, Life to Mars Foundation Archived 2020-09-22 at Archive.today, blogu ya spaceref.com ya Septemba 2001, iliangaliwa Machi 2019
  6. Ashlee Vance: Elon Musk’s Space Dream Almost Killed Tesla. tovuti ya Bloomberg.com ya 14 Mei 2015, iliangaliwa Machi 2019
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Elon Musk kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.