Anne Boleyn

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Anne Boleyn
Wake sita wa Henry VIII
(kufuatana na mwaka wa ndoa)
Katarina wa Aragon
(1509–1533)
Anne Boleyn
(1533–1536)
Jane Seymour
(1536–1537)
Catherine Howard
(1540–1542)
Catherine Parr
(1543–1547)

Anne Boleyn (1501 au 1507 - 19 Mei 1536 mjini London) alikuwa mke wa pili katika mlolongo wa wake sita wa mfalme Henry VIII wa Uingereza. Mtoto wake Elizabeth aliendelea baadaye kuwa malkia kwa jina la Elizabeth I wa Uingereza.

Henry VIII alimpenda Anne alipokuwa bado kijana mdogo. Lakini Anne alikataa kuwa hawara au mpenzi wa mfalme asipoolewa naye. Pendo lake kwa Anne lilimsababisha mfalme kutafuta talaka na mke wake wa kwanza Katarina wa Aragon. Pia alitaka kuachana naye kwa sababu hakumzalia mtoto wa kiume kama mrithi wa mfalme.

Henry alikataliwa kibali cha Papa wa Roma kwa talaka hii, akaamua kujitenga na usimamizi wa Papa, akajitangaza kuwa mkuu wa Kanisa la Uingereza na maaskofu wa kanisa hilo walimkubalia talaka.

Hapo Henry akamwoa Anne mwaka huohuo wa 1532. Mwaka 1533 walimpata mtoto wa kwanza aliyekuwa binti Elizabeth. Mfalme alisikitika kukosa tena mtoto wa kiume. hata hakushiriki katika ubatizo wa mtoto, lakini alimtambua kama mtoto rasmi na mrithi wake.

Miaka 1534 na 1536 Anne aliharibikiwa mimba. Mfalme, baada ya kuona ya kwamba hatakuwa na mtoto wa kiume kwa njia ya Anne, alianza kuangalia wanawake wengine, akaanza kutafuta njia za kuachana naye, lakini aliogopa talaka ya pili.

Hapo watu wa mazingira ya mfalme walianza kutafuta mashahidi kwa mashtaka ya uwongo ya kuwa Anne alikuwa na mapenzi na watu wengine. Mfalme aliona hii kuwa njia ya kuachana na Anne bila talaka. Kesi ya Anne ilipelekwa mbele ya mahakama akashtakiwa kuvunja ndoa, kufanya mapenzi na kaka yake na kupanga kumwua mfalme. Mashtaka yale yote hayakuweza kuthibitishwa lakini mfalme alikaa kimya na mahakama ilitoa hukumu ya mauti.

Anne Boleyn aliuawa tarehe 19 Mei 1536. Mfalme Henry VIII kwa nafasi hii alimchukua mnyongaji Jean Rombaud kutoka Ufaransa ambaye alitumia upanga baada ya shoka ya kawaida na kwa njia hii Anne aliweza kufa haraka na bila mateso.

Mfalme aliendelea kumwoa mke wake wa tatu Jane Seymour, hadi wa sita bila kupata mtoto wa kiume alivyotamani.

Mtoto Elizabeth alikuwa bado mdogo lakini alilelewa mbali na mama na baadaye mke wa sita wa mfalme aliamua kumlea.