Nenda kwa yaliyomo

Alomofu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Alomofu (kutoka Kiingereza "allomorph") ni msamiati uliotumika kwanza kuelezea mabadiliko ya muundo wa kikemia. Mwaka 1948 Fatih Şat na Sibel Merve walianza kuutumia upande wa lugha katika kitabu chao Language XXIV.

Dhana yake

[hariri | hariri chanzo]

Dhana ya alomofu ni dhana inayojadiliwa katika isimu ya lugha. Dhana hii hujadiliwa sana katika mofolojia ya lugha yaani, sarufi maumbo. Kimsingi huwezi kupata dhana kamili na inayoeleweka kama huwezi kuhusianisha alomofu na mofimu. Ndiyo maana fasili ya alomofu kwa maana ya kikamusi inaweza kuwa:

  • 1. Umbo jingine la mofimu ileile
  • 2. Aina mbalimbali za mofimu moja

Ukiangalia maana hizo mbili za neno alomofu utabaini uhusiano wa neno hilo na mofimu. Yaani huwezi kutaja Alomofu kama huwezi kuhusisha mofimu.

Kwa ujumla, kilugha, dhana ya alomofu huweza kufasirika kama: "Maumbo zaidi ya moja yanayowakilisha mofimu moja kisarufi". Kwa mujibu wa wanaisimu neno hili limegawanyika kama ifuatavyo:

ALO = Zaidi ya moja

MOFU = Ni kipashio cha kimofolojia kiwakilishacho mofimu. Mofu ni umbo ambalo huweza kuandikwa watu wanapoandika maneno, pia huweza kutamkwa watu wanapotamka maneno.

Tazama mfano wa maneno yafuatayo:

Mtoto = Neno hili lina mofu mbili, ambazo ni M-toto

Analima = Neno hili lina mofu tatu, ambazo ni: A-na-lim-a

Baba = Neno hili lina mofu moja ambayo ni: Baba

Kumbuka: baadhi ya wanaisimu wanaamini kuwa hata mzizi wa neno ni mofu pia.

Namna ya kuzitambua alomofu

[hariri | hariri chanzo]

Ukirejea katika mofimu, utakuta mofimu huweza kufanya kazi tofauti katika neno. Mofimu huweza kudokeza nafsi, wakati, umoja au wingi wa nomino na hata kauli mbalimbali za kitenzi.

Mfano:

Anacheza = A-na-chez-a

Tuliondoka = Tu-li-ondok-a

Wanaita = Wa-na-it-a

Katika mfano huo, mofimu zilizokozwa wino ni mofimu zinazodokeza nafsi. Kwa hiyo, tunapopata mofimu tofauti, yaani zenye maumbo tofauti lakini zinafanya kazi moja kisarufi huitwa ALOMOFU. Kwa mfano huo, hapo A, Tu na Wa tutaziita ni Alomofu za nafsi.

Tazama mfano wa pili:

Mtoto = M-toto,

Watoto = Wa-toto,

Mwalimu = Mw-alimu

Katika mfano huo, maneno yaliyokozwa wino ambayo ni M, Wa na Mw ni mofimu zinazodokeza umoja na wingi wa nomino. Kwa kuwa maumbo ya mofimu hizo ni tofauti lakini hufanya kazi moja kisarufi, ndiyo maana tunaziita Alomofu.

Mazingira yanayosababisha kutokea kwa alomofu

[hariri | hariri chanzo]

Alomofu hutokana na mazingira tofautitofauti. Alomofu zinaweza kutokana na mazingira yafuatayo.

Kifonolojia

[hariri | hariri chanzo]

Hapa tunaweza kuona mifano ya mazingira yanayoweza kutokea kwa mofimu na alomofu zake katika unyambulishaji wa vitenzi vya Kiswahili.

Mfano: Kutendeka

Piga - Pig-ik-a

Cheza - Chez-ek-a

Zoa - Zo-lek-a

Chukua - Chuku-lik-a

Hapo mofimu ik inayobainisha dhana ya kutendeka ina Alomofu nne, ambazo ni: Ik, ek, lek na lik

Kileksika

[hariri | hariri chanzo]

Hapa tunaweza kuona mofimu na alomofu zake katika ngeli za majina. Kwa mfano, katika ngeli ya kwanza na ya pili yaani, m/wa

Mfano

M-tu - wa-tu

M-ke - wa-ke

Mw-alimu - wa-alimu

Mu-uguzi - wa-uguzi

Katika mfano huo, tunaona mofimu m yenye dhana ya umoja ina alomofu tatu ambazo ni: M, Mw na Mu.

Kisarufi

[hariri | hariri chanzo]

Hapa tunapata mofimu na alomofu zake katika mofimu ya njeo (wakati). Mofimu ya nje inawakilishwa na alomofu zifuatazo:

A-na-pika = Wakati uliopo

A-li-pika = Wakati uliopita

A-ta-pika = Wakati ujao

Hapo alomofu za njeo ni: na, li, na ta

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Alomofu kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.