Nenda kwa yaliyomo

Mnyoo kichwa-miiba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Acanthocephala)
Mnyoo kichwa-miiba
Mnyoo kichwa-miiba (Telosentis exiguus)
Mnyoo kichwa-miiba (Telosentis exiguus)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Nusuhimaya: Eumetazoa
Faila ya juu: Platyzoa
Faila: Acanthocephala
Kölreuter, 1771
Ngazi za chini

Ngeli 4:

Minyoo kichwa-miiba (kutoka kwa Kiing. spiny-headed worm) ni minyoo vidusia wa faila Acanthocephala. Kichwa chao ni kama mkonga unaoweza kubenuliwa na kuwa na miiba mingi ambayo hutumika kwa kupenya ukuta wa utumbo wa kidusiwa na kuzuia kutolewa. Minyoo hao wana angalau vidusiwa wawili, pengine watatu au zaidi. Kwa kawaida kidusiwa ya mwisho ni vertebrata, kama mamalia au ndege. Vidusiwa wengine, wanaoitwa wa katikati, ni arithropodi kwa kawaida, gegereka mara nyingi sana.

Ukubwa wa minyoo hawa hutofautiana sana: wengine wana urefu wa milimita chache na wengine sentimita kadhaa, huku Gigantorhynchus gigas akiwa kutoka sm 10 hadi 65. Sifa ya kushangaza inayoshirikiwa na lava na wapevu ni saizi kubwa ya seli nyingi, k.m. seli za neva na seli zinazounda kikombe cha uterasi. Hali ya kuwa poliploidi ni kawaida na hadi 343n imerekodiwa katika baadhi ya spishi.

Minyoo kichwa-miiba hukosa mdomo na mfumo wa mmeng'enyo wa chakula. Hii ni sifa wanayoshiriki na tegu (Cestoda), ingawa makundi hayo mawili hayana uhusiano wa karibu. Hatua za wapevu huishi ndani ya matumbo ya vidusiwa wao na kufyonza virutubisho vilivyomeng'enywa na kidusiwa, moja kwa moja kupitia ngozi yao. Wanakosa mfumo wa kutoa kinyesi, ingawa baadhi ya spishi zimeonyeshwa kuwa na seli za mwali (protonephridia).