Nabii Eliya
Eliya (kwa Kiebrania אליהו, Eliyahu, maana yake "YHWH ndiye Mungu wangu";[1] kwa Kiarabu إلياس, Ilyās), alikuwa nabii katika Ufalme wa Kaskazini (Samaria) wakati wa mfalme Ahabu (karne ya 9 KK).
Habari za nabii huyo maarufu sana katika Biblia, na labda katika Qurani pia, zinapatikana hasa katika vitabu vya Wafalme.
Wakati mfalme Ahabu alipotawala Kaskazini (869-850 hivi KK) Israeli alimuasi kabisa YHWH ili kumuabudu Baali, kufuatana na sanamu mbili zilizotengenezwa na mfalme Yeroboamu I zikiwa na sura ileile ya Baali (fahali wa dhahabu). Mezani pa malkia Yezebeli walikuwa wanalishwa manabii wa uongo 850.
Hapo Mungu akamtuma Eliya wa Tishbi (1Fal 17-18) ambaye kwanza alizuia mvua isinyeshe nchini miaka mitatu na nusu, halafu akashindana na manabii hao juu ya mlima Karmeli. Kwa kuteremsha moto toka mbinguni juu ya sadaka yake YHWH alithibitisha kuwa ndiye Mungu pekee. Baada ya Eliya kuwachinja wote aliruhusu mvua inyeshe tena. Ndiyo sababu anasifika kwa nguvu ya sala yake (Yak 5:17-18).
Hasa ni kwamba, akisali juu ya mlima Sinai kama Musa mwanzoni mwa agano la Israeli na Mungu, alijaliwa kutokewa na Mungu katika sauti ndogo ya upepo mtulivu (1Fal 19:1-18). Hata katika Yesu kugeuka sura mlimani akatokea pamoja na Musa ili wamshuhudie kama wawakilishi wa Torati na Manabii (Mk 9:2-13).
Kwa jinsi alivyofanya kazi kwa ari, na kwa kupalizwa juu ya gari la moto (2Fal 2:1-18) akalinganishwa na moto (YbS 48:1-11) akatabiriwa atarudi kabla ya siku ya Bwana (Mal 3:23-24).
Ndiyo sababu Injili zinamtaja mara nyingi.
Kazi yake iliyeendelezwa hasa na nabii Elisha, ambaye anasifika pia kwa miujiza yake (YbS 48:12-16) na pamoja na mwalimu wake amechukuliwa na Yesu Kristo kama mfano wa unabii wake utakaowaokoa mataifa baada ya Israeli kumkataa (Lk 4:24-27).
Kadiri ya Injili ya Luka, malaika Gabrieli alitabiri kuwa Yohane Mbatizaji atakayezaliwa atarithi karama ya Eliya na kutekeleza unabii wa Kitabu cha Malaki juu yake.
[hariri] Tanbihi
- ↑ New Bible Dictionary. 1982 (second edition). Tyndale Press, Wheaton, IL, USA. ISBN 0-8423-4667-8, p. 319