Pius Msekwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pius Msekwa (wa kwanza kulia), 1961.

Pius Msekwa (amezaliwa 9 Juni 1935) ni mwanasiasa kutoka Tanzania. Kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005 alikuwa spika wa Bunge la Tanzania.

Elimu[hariri | hariri chanzo]

Pius Msekwa alipata Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1973-1974, pia Shahada ya Sanaa katika Historia kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, kati ya mwaka 1955-1960 na Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Nyadhifa alizowahi kuwa[hariri | hariri chanzo]

Amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola (CPA) kati ya mwaka 1999-2002, pia Mjumbe wa Kamati ya Kurekebisha Sekta ya Sheria kati ya mwaka 1993-1994 na Mjumbe wa Tume ya Rais ya Kuangalia Mfumo wa Vyama vya Siasa nchini kati ya mwaka 1991-1992.

Nyadhifa nyingine ambazo amewahi kuzishikilia, ni Uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi katika Mamlaka ya Maendeleo ya Mitaji kati ya mwaka 1985-2000 na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi katika Chuo cha Uongozi wa Wanyamapori barani Afrika kati ya mwaka 1985-2000.

Vilevile aliwahi kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu kati ya mwaka 1984-1989, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi katika Chuo cha Ushirika Moshi kati ya mwaka 1984, Mjumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria mwaka 1983 na Mjumbe wa Kamati ya Rais ya Kupunguza Matumizi ya Serikali kati ya mwaka 1982-1983.

Uongozi katika elimu[hariri | hariri chanzo]

Msekwa aliwahi kuwa Profesa wa Heshima katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1976, Mwenyekiti wa Tume ya Kupitia Mfumo wa Sheria nchini Tanzania, iliyojulikana kama "Tume ya Msekwa" kati ya mwaka 1975-1977 na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1970-1977.

Msekwa pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani nchini (NECTA) kati ya mwaka 1968-1970, Mjumbe na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini kati ya mwaka 1962-1980.

Mengineyo katika serikali[hariri | hariri chanzo]

Msekwa aliwahi pia kuwa Karani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 1962-1970, Karani Msaidizi wa Bunge kati ya mwaka 1960-1962 na Spika wa Bunge kati ya mwaka 2000-2005.

Vilevile Mbunge (wa kuchaguliwa) Jimbo la Ukerewe kati ya mwaka 1995-2000, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 1991-1994.

Pia Mbunge (wa kuchaguliwa)-Jimbo la Ukerewe kati ya mwaka 1990-1995, Mkuu wa mikoa ya Tabora na Kilimanjaro kati ya mwaka 1981-1984 na Ofisa wa Bunge kati ya mwaka 1981-1984.

Pia aliwahi kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kati ya mwaka 1977-1980 na Katibu Mkuu Mtendaji wa chama tawala cha Tanganyika Africa National Union (TANU) kati ya mwaka 1967-1970.

Kwa sasa Msekwa ni Katibu wa baraza la Viongozi wastaafu wa CCM, Baraza ambalo Mwenyekiti wake mi Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]