Patrick Balisidya

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Patrick Balisidya
Patrick Balisidya enzi za uhai wake akiwa kazini.
Patrick Balisidya enzi za uhai wake akiwa kazini.
Maelezo ya awali
Jina la kuzaliwa Patrick Pama Balisidya
Amezaliwa (1946-04-18)Aprili 18, 1946
Mvumi, Dodoma, Tanzania
Asili yake Mvumi, Dodoma, Tanzania
Amekufa Agosti 7, 2004 (umri 58)
Dar es Salaam, Tanzania
Aina ya muziki Muziki wa dansi
Ame/Wameshirikiana na Shaw Hassan
Orchestre Safari Sound
Afro70

Patrick Pama Balisidya (18 Aprili 1946 - 7 Agosti 2004) alikuwa mwanamuziki maarufu katika miondoko ya muziki wa dansi kutoka nchini Tanzania.

Historia yake na muziki[hariri | hariri chanzo]

Patrick Pama Balisidya alizaliwa Mvumi Dodoma tarehe 18 Aprili 1946. Kabila lake alikuwa Mgogo , kabila ambalo lina wanamuziki wengi maarufu kutokana na muziki kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kabila hilo. Mama yake alikuwa anapiga kinanda kanisani na hivyo basi kutokana na asili ya kabila lake na pia kutokana na mama yake, hakika huyu angeweza kujisifu kuwa muziki uko katika damu yake.

Vilevile Balisidya alikuwa kiongozi wa Bendi ya shuleni kwake Dodoma Secondary School. Ambapo kutoka hapo alijiunga na Chuo cha Ufundi , na baada ya kumaliza mafunzo alifanya kazi hiyo kwa muda na 1967 akawa tayari anapiga muziki Dar Es Salaam Jazz Band. Kufikia mwaka 1970 Patrick alikuwa ameanzisha kikosi chake mwenyewe Afro70, kikiwa na mtindo wake Afrosa. Alikuwa mbunifu katika muziki wake, na kwa muda mrefu alikwepa sana kuingia katika wimbi la kufuata mapigo ya Kikongo kitu ambacho hata wakati huo bendi nyingi zilikifanya, japokuwa kukutana na Franco wakati alipofanya moja ya ziara zake nchini humu kulimfanya abadili mtindo kwa kipindi kifupi na katika nyimbo moja wapo aliiga kabisa solo la Franco alilolipiga kwenye wimbo wake Georgette. Afro70 iliwakilisha wanamuziki wa Tanzania katika maonyesho ya mtu mweusi Lagos, Nigeria (FESTAC Festival 1977).

Vyombo alivyotumia katika maonyesho haya vilimsumbua akili mpaka alipofariki, kwani muda mchache kabla ya Festac, wakati huo serikali ikiwa imeshamtaarifu kuwa ndiye atakuwa mwakilishi wa Tanzania, vyombo vyake vyote vilihalibika katika ajali ya gari. Serikali ilikuwa imenunua vyombo vipya kwa ajili ya bendi yake ya Wizara ya Utamaduni wakati huo, ambavyo siku zote Balisdya alisema aliambiwa ni vyake baada ya maonyesho. Aliporudi kutoka Nigeria Kiongozi mwingine wa serikali aliamuliwa arudishe hivyo vyombo virudishwe serikalini na kwa kitendo kile kutangaza kifo cha Afro70.

Vyombo hivyo vilitumika kuanzisha bendi ya Asilia Jazz ambayo ilikuwa Bendi ya Wizara ya Utamaduni na Vijana. Balisdya alitumia muda mwingi kujaribu kudai haki yake hiyo ambayo ilimkwepa mpaka mwisho wa maisha. Mwaka 1979, Balisidya alikwenda Sweden na kushirikiana na kikundi cha Archimedes akatoa album nzuri sana iliyoitwa Bado Kidogo.

Kuna wakati Patrick alijiunga na Orchestre Safari Sound, (Masantula) na kupiga piano katika ule wimbo maarufu, ‘Unambie Siri’, Patrick pia alikuwa mpigaji mahiri wa kinanda. Kwa kweli nyimbo za Patrick zilizokuwa juu katika chati ni nyingi. Harusi, Dirishani, Weekend, Tausi, Pesa, Nakupenda Kama Lulu, Ni Mashaka na Mahangaiko, Afrika. Patrick alifariki tarehe 7, Agosti 2004 na kuzikwa 12 Agosti katika makaburi ya Buguruni Malapa.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Patrick Balisidya kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.