Mkutano wa Kupambana na Utumwa wa Brussels 1889-90

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mkutano wa Kupambana na Utumwa wa Brussels 1889-90 (kwa Kiingereza: Brussels Anti-Slavery Conference) ulifanyika huko Brussels, Ubelgiji, kati ya 18 Novemba 1889 - 2 Julai 1890.[1]

Uliitishwa na Mfalme Leopold II wa Ubelgiji aliyefuata ombi la Uingereza, iliyotaka kuonyesha jibu la kisiasa kwa harakati dhidi ya utumwa iliyoendeshwa siku zile na Kanisa Katoliki na hasa Kadinali Charles Lavigerie. Shirika ya Kukomesha Utumwa ya Uingereza na Ng'ambo (British and Foreign Anti-Slavery Society) iliwasilisha ripoti kwa mkutano huo.

Mkutano wa Brussels ulileta mkataba wa kukandamiza biashara ya watumwa katika Afrika wa mwaka 1890, ambao ulianza kutumika mnamo 1892.

Mkataba huo ulikuwa na udhaifu wake, jinsi alivyoeleza mtaalamu wa Historia ya Afrika Suzanne Miers:

"Haukuwa na utaratibu wa utekelezaji, na haukutaja mbinu zilizotumiwa na serikali za kikoloni kwa kunyonya kazi ya Waafrika, kama vile kazi ya kulazimishwa. Walakini, ulisaidia masilahi ya watawala wa kikoloni kukandamiza vita za kukamata watumwa, biashara ya watumwa wengi, na usafirishaji wa watumwa nje ya nchi. Hayo yote yalikwisha wakati tawala za wakoloni zilipoanzishwa. Utumwa wenyewe, ambao haukutajwa katika mkataba wa Brussels, ulivumiliwa kwa miaka mingi. Biashara ya watumwa wachache, pamoja na kuwapeleka wachache nje, iliendelea katika maeneo mengine hadi mwisho wa utawala wa kikoloni.

Mkutano wa Brussels ulifunua maovu ya biashara ya watumwa mbele ya macho ya jamii za watu wa Ulaya na hivyo serikali zililazimishwa kuchukua hatua dhidi yake.

Watetezi wa haki za binadamu katika Ulaya waliona mkataba kuwa ushindi mkubwa. Katika sheria ya kimataifa mkataba ulikuwa hatua ya kukubali kanuni ya udhamini, yaani kutekeleza mamlaka kwa maslahi ya waliotawaliwa. Kanuni hizo zimeingia katika utaratibu wa Shirikisho la Mataifa na mwishowe wa Umoja wa Mataifa. " [2]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Le Ghait, Alfred (1892). "The Anti Slavery Conference". The North American Review 154 (424): 287–296. JSTOR . 25102339 . 
  2. Miers, Suzanne. "Brussels Conference and Act, 1890". www.worldhistory.biz.