Nenda kwa yaliyomo

Mbawakawa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mende-kibyongo)
Mbawakawa
Bungo huko Mauritania (Pimelia angulata)
Bungo huko Mauritania
(Pimelia angulata)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Coleoptera (Wadudu wenye mabawa magumu)
Ngazi za chini

Nusuoda 4:

Mbawakawa (pia mbawakavu, mbawakau) ni jina la kawaida la wadudu walio wadogo hadi wakubwa wa oda Coleoptera. Majina mengine yanayotumika ni mende na kombamwiko, lakini kwa kuwa majina hayo hutumika pia kwa wadudu wa oda Blattodea, ni bora kutumia mende-kibyongo na kombamwiko-kibyongo.

Kwa kawaida kiunzi nje cha wadudu hao ni kigumu sana. Hata mabawa ya mbele yamekuwa kama magamba magumu na pengine magamba hayo yameunganika kuwa moja. Kiunzi kigumu hicho kinazuia mbuai wadogo wasiwale mbawakawa. Sehemu za kinywa ni sahili lakini spishi mbuai zina mandibuli kubwa na kali mara nyingi. Macho yao yameundwa kwa sehemu nyingi kama wadudu wote lakini macho ni madogo kwa kulinganisha na kichwa kuliko wadudu wengine wengi. Pingili ya kwanza ya toraksi (kidari) huitwa protoraksi (ile ya mbele). Upande wake wa juu ni pronoto na inaonekana zaidi. Pingili ya pili na ya tatu zimeungana kwa kawaida na pamoja huitwa pterotoraksi (ile yenye mabawa). Kiungo kati ya protoraksi na pterotoraski hupindika kwa rahisi na kwa hivyo mbawakawa wanaweza kusogeza kichwa chao katika pande zote kwa rahisi zaidi kuliko wadudu wengine, isipokuwa vivunjajungu.

Oda ya Coleoptera ni kubwa kuliko zote za wanyama na ina zaidi ya spishi 400,000. Spishi nyingi bado hazijafafanuliwa na wataalamu wanakisia kwamba jumla ya spishi itazidi milioni moja na kwamba 25% ya spishi zote za wanyama ni Coleoptera. Kwa sasa karibu 40% ya spishi za wanyama zilizofafanuliwa ni Coleoptera. Lakini hivi karibuni wanasayansi wameanza kumaizi kwamba oda hii si monofiletiki, yaani haina mhenga mmoja tu. Nusuoda ya Adephaga inaweza kuwa oda na labda makundi mengine ya Coleoptera yatapewa oda zao.

Kuna majina mbalimbali kwa makundi ya mbawakawa, kama vile: bungo, dundu, fukusi, kidungadunga, kimetameta/kimulimuli, kipukusa, kisaga, mdudu-kibibi, sururu na tuta.

Makala hii kuhusu mdudu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mbawakawa kama uainishaji wake wa kibiolojia, maisha au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.