Nenda kwa yaliyomo

Kukausha kwa moshi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Hemu na soseji katika chumba cha moshi baridi.

Kukausha kwa moshi ni mbinu ya kutunza vyakula ili visiharibike haraka. Kwa njia hiyo chakula hupokea pia ladha maalumu.

Hutumiwa hasa kwa nyama na samaki, mara chache pia kwa mboga ya majani lakini hapo zaidi ni shauri la ladha.

Kama hatua ya kwanza nyama au samaki hutiwa chumvi. Chumvi huondoa sehemu ya maji ndani yake na kuzuia bakteria wengi ambao wanaweza kusababisha uharibifu.

Katika hatua ya pili nyama iliyoandaliwa vile huweka juu ya moshi wa moto. Hapo kiwango cha maji hupungua zaidi. Kemikali katika moshi wa moto wa mbao huzuia tena bakteria. Uso wa kile kinachotiwa moshi hukauka zaidi na kuwa mgumu kiasi na hivyo kuna kizuizi cha ziada dhidi ya kuingia kwa bakteria na wadudu[1].

Moshi wa moto[hariri | hariri chanzo]

Samaki huwekwa kwenye moshi wa moto.

Hapo nyama mbichi na pia samaki mbichi huwekwa juu ya moto ambapo vinapikwa polepole na kukaushwa kiasi kwa halijoto duni za sentigredi 50-90. Vyakula vya aina hiyo haviwezi kudumu siku nyingi isipokuwa kama zimetiwa chumvi nyingi.

Siku hizi kazi inatekelezwa katika oveni ya pekee ambamo jotoridi inaweza kutawaliwa kikamilifu. Joto linapatikana kwa umeme au gesi. Moshi unapatikana ama kwa kumwaga ubao uliosagwa ndani ya oveni au kwa kupuliza kutoka nje moshi ndani ya oveni.

Soseji maalum huwekwa kwenye moshi wenye jotoridi ndogo ya nyuzi 25-40 pekee, kwa kupata ladha inayotafutwa.

Moshi baridi[hariri | hariri chanzo]

Hemu kwenye moshi kiwandani.

Asili ya kukausha kwa moshi baridi ni nyumba za zamani za wakulima katika nchi za baridi. Hapo moshi wa jikoni ulienea kote nyumbani na kupaa juu. Hivyo vipande vya nyama vilivyotiwa chumvi kama hemu (ham) na soseji zilitunzwa chini ya dari nje ya upeo wa panya na paka na hivyo vilikaa katika moshi baridi uliyopaa hadi kule. Hivyo vilipokea ladha yake na kukauka polepole sana ilhali zikiiva pia na kubadilika ladha[2].

Vyakula vilivyoandaliwa kwa njia hiyo vinaweza kudumu miezi bila kuoza.

Siku hizi moshi baridi hutiwa katika vyumba au makabati ya pekee kwenye jotoridi ya nyuzi za 15-25. Moshi kutokana na ubao maalumu unaoteuliwa kulingana na ladha inayolengwa hupulizwa ndani ya vyumba hivyo. Vyakula vinavyokaushwa kwenye moshi baridi ni soseji kama salami na hemu (ham).

Moshi bandia[hariri | hariri chanzo]

Katika uzalishaji wa kitasnia wa soseji na hemu matumizi ya moshi bandia hutumiwa. Hapo hawatumii moshi halisi bali kemikali zinazounda ladha ya moshi zinakorogwa katika maji na kumwagwa juu ya nyama wakati wa kuikausha.

Tahadhari ya kiafya[hariri | hariri chanzo]

Ulaji wa mara kwa mara wa nyama na samaki iliyokaushwa katika moshi unaweza kuongeza hatari ya kupata kansa[3][4] na magonjwa ya moyo.[5]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. [https://hotsmoked.co.uk/cold-smoking-recipes-and-tips Cold Smoking - A quick Introduction - What is Curing? - Drying - Creating Cold Smoke - RECIPES - Bacon - Pancetta - Beetroot Cured Salmon], tovuti ya hotsmoked.co.uk, iliangaliwa Machi 2021
  2. Briefing: Smoked food, gazeti la The Herald, 19.02. 2002, kupitia archive.org
  3. Leyshon, Laura. "I enjoy eating smoked salmon. How healthy is it?", The Globe and mail, 2018-05-11. 
  4. Rapaport, Lisa. "Barbecued and smoked meat tied to risk of death from breast cancer", U.S., 2017-01-19. (en-US) 
  5. Harvey-Berino, Jean. "What Are the Dangers of Eating Smoked Meat?", 2017-06-30. Retrieved on 2021-03-18. (en) Archived from the original on 2021-07-05. 

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje na kujisomea[hariri | hariri chanzo]

  • Curing and Smoking Meats for Home Food Preservation Archived 6 Mei 2022 at the Wayback Machine., tovuti ya National Center for Home Food Preservation , Marekani
  • McGee, Harold (2004). "Wood Smoke and Charred Wood". On Food and Cooking (toleo la Revised). Scribner. ku. 448–450. ISBN 978-0-684-80001-1.
Makala hii kuhusu mambo ya teknolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hiyo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.