Kanu, kala au karasa ni wanyama mbua wadogo wa jenasiGenetta katika familiaViverridae. Kanu mlasamaki aliainishwa katika jenasi Osbornictis lakini wataalamu wameonyesha kama spishi hii ina mnasaba wa karibu na kanu wa jenasi Genetta. Wanyama hawa ni warefu na wembamba wenye mkia mrefu, kichwa kidogo na masikio makubwa. Rangi yao ni nyeupe hadi njano na wana madoa meusi na mkia wenye miviringo. Mkia wao ni mrefu sana: 1-1.5 mara urefu wa mwili. Hiyo inawapa taraju wakisombea miti na kuchupa matawi. Wanatokea Afrika tu isipokuwa kanu madoa-madogo ambaye anatokea Rasi ya Iberia na Mashariki ya Kati pia. Kanu wana tezi kando ya mkundu zinazotoa aina ya zabadi ambayo inanuka sana. Hula wanyama wadogo, mijusi, ndege wadogo, amfibia, wadudu na hata matunda.