Kanku Kelly

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kanku Kelly
Kanku Kelly upande wa kulia na kushoto (kati) Waziri Ally (Kissinger) wakati wa mazoezi ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania mnamo 2011.
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaNkashama Luis Polycarp
Amezaliwa20 Januari 1958 (1958-01-20) (umri 66)
Kananga, Mkoa wa Kasai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Kazi yakeMpiga trampeti
Ameshirikiana naMarquis du Zaire

Nkashama Kanku Kelly (20 Januari, 1958) ni mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- Tanzania. Anafahamika zaidi kwa kuwa miongoni wapigaji mashuhuri wa trampeti mwenye historia ya ndefu katika muziki - hasa kwa kushirikiana na Maquis du Zaire na kuwa mwanzilishi wa Kilimanjaro Connection Band. Vilevile amebahatika kushikana mikono na viongozi wakubwa wanaoheshimika duniani kote, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Nelson Mandela.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Wasifu[hariri | hariri chanzo]

Kanku ambaye alifukuzwa shule kwa ajili ya muziki, jina lake halisi ni Nkashama Luis Polycarp, alizaliwa Januari 20, 1958, katika mji wa Kananga Mkoa wa Kasai, Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kanku ambaye aliingia nchini Tanzania akiwa kinda kabisa (chini ya miaka ishirini) alikuwa kivutio kikubwa kwenye safu ya wapulizaji wa trumpet katika bendi iliyokuwa tishio miaka ya 1970 hadi 1990 ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa White House, Ubungo jijini Dar es Salaam. Baba yake mzee Chasuma Leonard alikuwa Daktari wa binadamu na mama yake Chibwabwa Kayipu, alikuwa mfanyabiashara katika mji huo wa Kananga. Kelly alipata elimu ya msingi katika shule ya Kamilabi ambayo miongoni mwa masomo yaliyokuwa yakifundishwa somo la muziki lilikuwemo. Baadaye aliendelea na masomo ya juu katika shule ya Sekondari ya Lyceede Kelekele, ambako aliishia kidato cha tano kwa kufukuzwa shule baada ya kufumwa na mwalimu akiandika wimbo wa Nyboma Mwandido darasani mwaka 1973.

Akiwa shule ya msingi walifundishwa somo la muziki na yeye alikuwa akifanya vizuri sana na kuwa mmoja kati ya wanafunzi bora wa somo hilo. Akifafanaua juu ya kufukuzwa shule, Kelly anasema “Nilikuwa anapenda muziki kupita kiasi, nikiwa darasani mwalimu alinikuta nikiandika wimbo wa ‘Amba’ uliotungwa na Nyboma Mwandido ndipo nikafukuzwa shule”. Kanku anasema baada ya kufukuzwa shule mwaka 1974, alihitajika kujiunga na jeshi la nchi hiyo katika kitengo cha muziki wa Brass band, lakini akakataa akiwa na dhamira kubwa kuwa mwanamuziki mashuhuri. Anaeleza kuwa jamaa zake aliokuwa nao darasani asilimia tisini walipelekwa jeshini kupiga muziki wa Brass band.

Harakati za maisha na muziki[hariri | hariri chanzo]

Kushoto; Kanku Kelly na wa upande wa kulia ni Tshimanga Assosa wakiwa katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam wakati wa mazishi ya Mzee Kassim Mapili, Februari, 2016.

Katika kujitafutia maisha mwaka 1975 Nkashama Kelly aliamua kwenda mji wa Katanga uliopo jimbo la Shaba, huko alijiunga katika bendi ya Safari Nkoi iliyokuwa na wanamuziki mahiri akina Ndala Kasheba na Baziano Bwetii. Nyota yake ilianza kutoa nuru njema, kwani mwezi Febrauri 1977 baadhi ya wanamuziki Kongo walifuatwa na Chibangu Katai ‘mzee Paul’ kuja Tanzania kujiunga na bendi ya Maquis du Zaire. Anamtaja Kikumbi Mwanza Mpango maarufu kama "King Kikii", Mutombo Sozzy (drumz), Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’ (besi gita) Ngalula Chandanda (steji shoo) pamoja na yeye Kanku ndiyo kwa pamoja walichukuliwa kuja Tanzania waka huo. Alipofika Maquis du Zaire jijini Dar es Salaam, aliungana na wapulizaji wa trumpet wengine akina Mwema Mudjanga ‘mzee Chekecha’, Mino wa Mwamba ‘mzee Tito, Mpoyo Kalenga, Kaumba Kalemba na Ngenda Kalonga.

Safu hiyo ilikuwa burudani tosha katika ukumbi wa White House wakati huo kwa jinsi walivyokuwa wakimudu kulimiliki jukwaa kwa uchezaji wao. Kanku Kelly anatamka kwamba mwaka 1978 ilikuwa kama ‘bahati ya mtende kuotea Jangwani’ anasema hatakuja kuisahau siku ile aliyopelekwa kukutana na Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam. Anakumbuka alishikana mikono na rais wa Tanzania wakati huo, Mwalimu Nyerere na alimuuliza “unatoka Kongo ya Lumumba”? Akiwa na hofu isiyokuwa na sababu, Kelly alijibu "ndiyo". Maisha ni kutafuta. Ndivyo alivyosema Kanku kwamba mwanzoni wa mwaka 1981 alichomoka na kwenda kujiunga na bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS). Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara maarufu Hugo Kisima. Katika kipindi cha mwaka mmoja wa 1981 aliondoka Orchestra Safari Sound(OSS) kwenda kujiunga katika bendi ya mzee Makassy ambako huko nako hakudumu kipindi kirefu na alirudi tena OSS.

Mwaka 1982 Kanku alichumpa hadi Nairobi nchini Kenya, na akajiunga na bendi ya Orchestra Virunga iliyokuwa ikiongozwa na mwanamuziki mkongwe Samba Mapangala, ambako alidumu na bendi hiyo kwa takriban miaka miwili. Akiwa huko Kenya mwaka 1984 Nkashama Kanku Kelly akiwa na wanamuziki wenzake, waliamua kuanzisha bendi yao ya Orchestra Vundumuna ikiwa na wanamuziki nguli akina Sammy Kasule (kuimba), Nsilu wa Bansilu ‘Manicho’(gita), Tabu Ngongo(sax), na Tabu Fratal (gita/drums). Wengine walikuwa akina Munamba Jean (keyboard) na Botanga Mofrank Bijing, ambaye alikuwa kiongozi wa bendi na mpiga keyboard. Anamtaja Mofank kuwa ndiye aliyekuwa chanzo cha bendi hiyo kupata mikataba wa kupiga muziki nchini Japan kwa kupitia nafasi yake ya kuoa mwanamke wa nchi hiyo.

Orchestra Vundumuna wakiwa nchini Japan na kufa kwa bendi[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kuachiwa huru mzee Nelson Mandela toka gerezani, mwaka 1990 alifanya ziara ya kuizunguka dunia. Katika ziara yake hiyo alifika nchini Japan ambako bendi yao ya Vundumuna ilialikwa kutoa burudani katika sherehe za mapokezi ya shujaa huyo kwenye uwanja uliokuwa umefurika kumpokea. Anasema mzee Mandela alivutiwa na wanamuziki wa Vundumuna ambao ni weusi. Mandela alipanda kwenye jukwaa lao kuja kuwashika mikono huku akiwauliza wanatoka nchi gani. Alipomfika yeye, akamuuliza swali lilelile kama aliloulizwa na Mwalimu Nyerere kuwa natoka Zaire ya Lumumba? “ Sitoshau maishani mwangu siku hiyo” anasema Kanku. Vundumuna ilifanya safari zaidi ya mara kumi kati ya miaka ya 1987 na 1991 kisha wakatengenezewa vikwazo vya hati yakufanya kazi hapo Japan (working permit), na walirudi nyumbani na ndiyo ikawa mwisho wa bendi hiyo.

Kuanzisha bendi yake binafsi "The Kilimanjaro Connection"[hariri | hariri chanzo]

Kanku Kelly akiwa bado kijana kwa wakati huo alikuwa ni mwenye ujasiri usiyetaka kushindwa kitu. Mei 15, 1992 aliingiwa na ujasiri wa kusimama kama yeye na kuazisha bendi yake ya The Kilimanjaro Connection. Alifanikiwa kuwapata wanamziki mahiri na makini akina Asia Darwesh ‘super mama’ aliyekuwa mbonyezaji wa kinanda, Mafumu Bilali ‘Bombenga’ kwenye Saxophone, Andy Swebe kwa upande wa gita zito la besi, Burahan Muba, aliyekuwa mpiga gita la solo na Shomari Abdalah akizicharaza drumz. The Kilimanajaro Connection Band imekuwa ikipata mikataba ya kupiga muziki katika nchi mbalimbali za Singapore, Malaysia, Thailand na Oman. Ni usimamizi makini wa Kanku Kelly umeifikisha bendi hiyo kupata mafanikio makubwa pia bendi hiyo imekubalika sana nchini Malaysia.

Maisha binafsi[hariri | hariri chanzo]

Kanku Kelly ni raia halali wa Tanzania aliyefanikiwa kupata uraia mapema Aprili 27, 2011. Matarajio yake ya baadaye ni kuwa mtayarishaji mkubwa aiyekamilika kwa vyombo vya kufanyia kazi hiyo. Ametoa shukrani nyingi za dhati kwa watanzania wote waliomlea toka alipokuja hapa nchini, akiwa bado kinda wa miaka 19 hadi leo ana zaidi ya nusu karne. Kanku Kelly ni Baba wa familia. Alifunga ndoa ya kiserikali mwaka 1987 na Bi. Mwajuma Kibwana ambaye ni Mtanzania, katika jiji la Nairobi huko Kenya. Katika maisha yao ya ndoa wamefanikiwa kupata mabinti wawili Agnes Chichi Kelly (26), anayesoma katika Chuo Kikuu nchini Malaysia na mdogo wake Lucy Kelly (20) ambaye anamuelezea kwamba amefuata nyayo zake katika muziki.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kanku Kelly kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.