Ahmed Kipande
Ahmed Kipande | |
---|---|
Taarifa za awali | |
Jina la kuzaliwa | Ahmed Mohamed Kipande |
Amezaliwa | 1937 Kilwa Kivinje, Tanzania |
Amekufa | 23 Aprili, 1987 Tandika Maguruwe, Dar es Salaam, Tanzania |
Kazi yake | Mwimbaji, mtunzi, mpiga gitaa |
Miaka ya kazi | 1950-1987 |
Ahmed Mohamed Kipande (1937 - 27 Aprili 1987) alikuwa mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi kutoka nchini Tanzania. Anafahamika zaidi kwa kuwa mwanzilishi wa bendi ya muziki wa dansi maarufu kama "Kilwa Jazz Band".[1]
Historia
[hariri | hariri chanzo]Maisha na muziki
[hariri | hariri chanzo]Ahmed Mohamed Kipande ni kati ya wanamuziki ambao wameacha jina kubwa kutokana na mchango wake katika maendeleo ya muziki wa Tanzania. Kipande alizaliwa Kilwa Kivinje mwaka 1937, alianza shule 1946 huko huko Kilwa Kivinje na baada ya darasa la nne akahamia Dar es Salaam ambako aliendelea shule ambayo baadae iliitwa Uhuru Boys mpaka alipomaliza darasa la nane. Alipoanza kazi alianzisha kundi la muziki lililokuwa likitumia vyombo vya asili , baadaye akaanzisha bendi rasmi ya muziki aliyoiita Home Boys. Ujuzi wa muziki wa Kipande ulianza kujulikana rasmi 1955 wakati alipoweza kushika nafasi ya pili katika mashindano ya kupiga gitaa yaliyofanyika mtaa wa Kichwele, mbele ya viongozi wa Kikoloni. Kipande alipata zawadi ya shilingi 15 kwa kuwa wa pili. Mwaka 1958 aliachana na bendi ya Home Boys na kuanzisha Kilwa Jazz Band akiwa na wanamuziki watano tu.
Kipande alikuwa hodari kwa gitaa la solo na hata kumudu vizuri gitaa la Hawaian na pia alikuwa mpuliza saksafoni mahili sana. Alikaa miaka mingi Kilwa na kupiga nyimbo ambazo hadi leo bado watu wanazipenda. Napenda Nipate Lau Nafasi, Nachekacheka Kilwa leo, Play your Part na nyingi nyingine.
Baadaye kutokuelewana fulani kukamfanya ahame na kuanzisha African Quellado, bendi nzuri ambayo haikudumu muda mrefu, alijaribu kufufua tena Kilwa Jazz iliyokuwa imekufa lakini haikudumu muda mrefu.
Hakurudi tena kwenye muziki mpaka mauti yalipomkuta.
Kifo cha Kipande
[hariri | hariri chanzo]Kipande alifariki 23 Aprili 1987 nyumbani kwake Tandika Maguruwe na kuzikwa hukohuko, baada ya kuugua kwa muda wa miaka 10 akiwa amepooza upande wa kulia wa mwili wake.
Urithi
[hariri | hariri chanzo]Shahiri zuri sana lilitungwa na mtunzi Saidi M Nyoka (Udogo si hoja) katika kumuelezea Ahmad Kipande. Tazama mashairi yenyewe:
- Amezikwa Jumanne,jeneza tukalibeba,
- Aprili mbili nne, mwaka themanini na saba,
- Ikabidi tujazane, kinamama kinababa,
- Kwa Maguruwe sa nane,tutele kwenye msiba,
- Machozi tele matone, simanzi imetukaba,
- Kiasi tusijuane, uzishini kwa nasaba,
- Kalale pema panene, Kipande kwaheri baba
- Alikuwa maarufu, Kipande na bendi yake
- Nchi hii kaisifu,katika utunzi wake,
- Leo tena katawafu,Yarabi pema muweke,
- Muweke paangalifu, kila jaza imfike,
- Anukishie harufu, njema kaburini pake,
- Umsamehe machafu,Yarabi kando uyaweke,
- Yaweke mema matufu, Kipande afaridhike,
- Faraja ya ukunjufu, Roho yake ifufuke,
- Mjaze mema Latifu, humo kaburini mwake.
- Alikuwa mwimbaji, mzuri wan chi hi,
- Kadhalika mtungaji, hodari wa wasanii,
- Kisha mpulizji, wa zumari kwa bidii,
- Bidii ya mwanambuji, sasa hatumsikii,
- Bwana Mungu mfariji,Pepo njema ya utu,
- Aishi katika mji,wa amani na jamii,
- Jamii ya watendaji, mazuri ya utwalii,
- Nasi nyuma wafataji, njia ndo hii hii,
- Kimezimika kipaji, kupotea jii jii
- Alikuwa kiongozi, wa bendi mwenye akili,
- Kaongoza Kilwa jazi,kwa nyimbo za maadili,
- Kwa amri ya Mwenyezi, kaufisha wake mwili,
- Mwili wake hatuwezi, kuuona kwa dalili,
- Mawazo yake azizi, hayafutiki kwa kweli,
- Molla umpe makazi,mazuri penye kivuli,
- Kivuli chenye mbawazi,kisichopenya miali,
- Mwondoshee mabazazi,na adui wakatili,
- Afate maelekezi, ua wewe Bwana Jalali.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- http://wanamuzikiwatanzania.blogspot.com/2011/08/ahmed-mohamed-kipande-wa-kilwa-jazz.html Archived 13 Agosti 2016 at the Wayback Machine. katika blogu ya Anko John Kitime
- http://www.tanzaniaheritageproject.org/ahmed-kipande-of-kilwa-jazz-band/ Archived 18 Februari 2017 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Ahmed Kipande kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Ahmed Kipande alivyong'ara na Kilwa Jazz". Mwananchi (kwa Kiingereza). 2021-03-13. Iliwekwa mnamo 2024-01-13.