Inter Mirifica

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Hati hiyo ilitolewa na Mtaguso wa pili wa Vatikano mapema (4 Desemba 1963) ili kukabili jambo ambalo siku hizi ni zito sana kwa jinsi linavyochangia maisha na utamaduni wa watu duniani kote, yaani vyombo vya upashanaji habari vilivyoendelea hasa katika karne ya 20 na kuwafikia karibu watu wote vikieneza habari, mawazo, maadili n.k.

Hati hiyo maalumu, iliyopata kura 1960 dhidi ya 164 kati ya washiriki wa mtaguso huo, inaitwa kwa Kilatini "Inter Mirifica" (maana yake, "Kati ya Maajabu").

Kwa njia yake Kanisa Katoliki limetamka kuwa linavipokea kwa shukrani kwa Mungu aliyempa binadamu akili ya kuvumbua na kubuni njia hizo zinazoweza kumuinua hata kidini.

Lakini kwa ubaya wa moyo wake anaweza pia kuzitumia kwa uharibifu wake na wa wengine wengi, hasa watoto na vijana wasio na kinga.

Kwa hiyo Kanisa linapaswa kushughulika ili vyombo hivyo vyote vitumike vema kwa kueneza habari njema, maadili na taarifa za kweli ili watu wakabili maisha vizuri na kuokoka.

Pia liwaelimishe wote kuhusu namna ya kuchuja na kutumia vilivyo magazeti, vitabu, filamu, redio, televisheni n.k., wakielewa urahisi wa kudanganywa na kupotoshwa na vyombo hivyo.

Hiyo ni kazi ya wachungaji, wazazi na walezi, lakini serikali pia isaidie kutunza mazingira safi.

Mtaguso umeagiza shughuli hizo ziratibiwe kijimbo, kitaifa hata kimataifa.

Kwa kuwa shughuli hizo zina gharama kubwa, Wakristo wanahimizwa kujitolea kwa ukarimu hasa Jumapili maalumu moja kwa mwaka.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]