Beirut

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kitovu cha Beirut kutoka hewani: Bandari, Ras Beirut, Uwanja wa ndege

Beirut (pia: Beyrouth; kwa Kiarabu: بيروت) ni mji mkuu wa Lebanon, pia mji mkubwa na bandari kuu ya nchi hiyo. Iko mwambaoni pa Bahari ya Kati.

Imekadiriwa kuwa idadi ya wakazi ni kati ya milioni moja na mbili.

Mahali pa mji ni kanda kati ya bahari na milima inayofuatana sambamba na mwendo wa pwani.

Kitovu cha kihistoria kiko kando ya rasi inayoitwa Ras Beirut penye kitovu cha mji wa kisasa kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ya Lebanon kati ya miaka 1975 na 1990.

Kanisa na msikiti kandokando mjini Beirut.

Kipindi kirefu cha vita hivyo vya ndani kilibadilisha uso wa mji katika mengi. Mji ulitenganishwa katika maeneo ya Wakristo na Waislamu hasa. Mitaa mipya ilianzishwa mbali na mstari wa mapigano, ujenzi ukaongezeka sana hasa upande wa kaskazini na kuelekea milimani.

Tangu amani ya mwaka 1990 mji ulijengwa upya. Lakini mashambulizi ya ndege za vita za Israel mnamo Julai 2006 yaliharibu tena sehemu za mji.

Nyumba zilizofyatuliwa risasi wakati wa vita 1975-1990.

Kabla ya vita Beirut ilikuwa tangu muda mrefu kitovu cha kiuchumi na kielimu cha Mashariki ya Kati. Chuo Kikuu cha Kimarekani (American University of Beirut) pamoja na vyuo vikuu vya serikali na Kanisa Katoliki vimeendelea kufundisha hata wakati wa vita. Nafasi ya kinara cha kielimu imerudishwa kwa sababu ya uhuru kwa ajili ya magazeti na wachapishaji vitabu, lakini uongozi wa kiuchumi umehamia nchi za ghuba ya Uajemi kama vile Kuwait, Qatar na Falme za Kiarabu.

Makala hii kuhusu maeneo ya Asia bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Beirut kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.