Anwani
Anwani (kutoka neno la Kiarabu) ni maelezo jinsi ya kumkuta mtu au mahali.
Anwani ya posta
Anwani ya posta ni maelezo yanayoandikwa juu ya bahasha au kifurushi yanayotaja mahali mtu anapoishi au anapofanyia kazi na ambapo barua zinaweza kutumwa. Katika nchi nyingi kama Tanzania au Kenya anwani ya posta inataja jina la mpokeaji pamoja na namba ya sanduku la posta na mahali pa ofisi ya posta.
Katika nchi nyingine barua zinapelekwa pia nyumbani kwa hiyo bahasha hutaja jina la mpokeaji, mtaa wenye nyumba yake, namba ya nyumba pamoja na mji au mahali anapoishi, pamoja na msimbo wa posta (postikodi) ya eneo hilo.
Anwani za nyumbani huandikwa pia ukituma kifurushi kwa njia ya kampuni ya binafsi, mara nyingi pamoja na namba ya simu.
Anwani ya baruapepe
Anwani ya baruapepe (kwa Kiingereza: email adress) ni mpangilio wa habari zinazomwezesha mwandishi wa baruapepe kufikisha ujumbe kwa mlengwa. Kwa kawaida huwa na sehemu mbili:
- jina la mpokeaji linaloandikishwa kwenye kampuni ya huduma za baruapepe (email provider) ; inaweza kuwa tofauti na jina halisi la mtu
- jina la kampuni linalotoa huduma au jina la kikoa (domain) kinachobeba anwani.
- sehemu hizo hutenganishwa na alama ya @
Mifano:
- bahati147@gmail.com
- horseycrazy@yahoo.com
- larry.smith@msn.com
- mfano50150@domain.co.tz
Anwani ya mtandao (URL)
Anwani ya mtandao au URL ni namna ya kutaja mahali pa tovuti kwenye intaneti.
Mfano:
- https://sw.wikipedia.org/wiki/Anwani ni URL ya makala hii
- https://nation.africa ni URL ya tovuti la gazeti "The Nation" kutoka Nairobi
Anwani ya kijiografia (majiranukta)
Anwani ya kijiografia au majiranukta inataja mahali duniani au hata kwenye anga kwa kurejea fomati ya latitudo na longitudo.
Mfano: majiranukta ya 6°10′S 35°44′E (digrii 6 na dakika 10 Kusini, digrii 35 na dakika 44 Mashariki) yanataja nafasi ya Dodoma kwenye uso wa ardhi. Yanaweza kuandikwa pia hivyo kwa njia ya desimali : -6.166667, 35.733333.
Viungo vya Nje
- Frank's compulsive guide to postal addresses
- Universal Postal Union Archived 2009-07-24 at the Portuguese Web Archive Postal addressing systems by country
- ISO TC 154 ISO Technical Committee 154 on Processes, data elements and documents in commerce, industry and administration
- United States Postal Service Address Guidelines