Akwilina Akwilini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Akwilina Akwilini
Picha ya Akwilina Akwilini enzi ya uhai wake.
AmezaliwaAkwilina Akwilini Bafta[1]
(1996-04-01)1 Aprili 1996
Amekufa16 Februari 2018 (umri 21)
Kinondoni, Dar es Salaam, Tanzania
Sababu ya kifoRisasi ya kichwa kutoka kwa jeshi la polisi waliokuwa wanazuia maandamano ya CHADEMA
Majina mengineAquilina, Akwilina
Kazi yakeMwanafunzi wa chuo cha usafirishaji Dar (NIT)
Anajulikana kwa ajili yaMhanga wa maandamano ya kisiaa ya CHADEMA

Akwilina Akwilini Bafta (1 Aprili 1996 - 16 Februari 2018) alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha usafirishaji Dar es Salaam (NIT) ambaye alifariki baada ya kupigwa risasi ya kichwa kimakosa na afisa wa polisi aliyekuwa anajaribu kutuliza ghasia za waandamanaji wa kisiasa wa CHADEMA tarehe 16 Februari Ijumaa, 2018 huko Kinondoni. Tukio hili la kusikitisha limeamsha hisia kali sana katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania. Wengi wamelaani kitendo cha askari kutumia risasi za moto kutuliza ghasia za kisiasa. Tena kwa watu ambao hawana silaha yoyote na wanafanya maandamano ya amani bila fujo.

Baada ya tukio, kumekuwa na maswali mengi inawezekana vipi risasi iliyopigwa juu, impige mtu upande wa kushoto ubavuni itokee kulia. Baada ya tukio, polisi sita wahojiwa kuhusiana na tukio hilo la kusikitisha.[2] Siku mbili tangu tukio kutokea, Rais wa Tanzania John Joseph Pombe Magufuli amelaani vikali tukio hilo lisilo la kibinadamu dhidi ya mwanafunzi huyo, na kuwataka wale wote waliohusika wafikishwe katika vyombo vya sheria.[3]

Baada ya hili kutokea, ukaanza msako wa kumtafuta mchawi aliyesababisha tukio hili, na hatimaye wakaungukia katika upande wa kisiasa. Hasa akina Mbowe na kikosi chake cha CDM kilichoshutumiwa kwa kufanya maandamano haramu yasiyo na kibali.[4] Hata hivyo, viongozi wa juu wa CDM waliripoti polisi, na hatimaye kuachiwa kwa dhamana huku kukiwa na taarifa ya kwamba uchunguzi haujakamilika na wataitwa tena mara tu uchunguzi dhidi yao utakapokuwa tayari.[5]

Wasifu

Maisha na elimu

Akwilina alizaliwa tarehe 1 Aprili, 1996, katika Kijiji cha Marangu Kitowo, Kata ya Olele, wilayani Rombo, Kilimanjaro. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule Kitongoria na kuhitimu 2009. Halafu baadaye sekondari alisomea mkoani Iringa na kuhitimu 2014. Baadaye, alichaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Embauwai, iliyoko Ngorongoro, Arusha. Kutokana na afya yake kumletea shida akiwa mkoani Arusha, ililazimika kuhama mkoa na kwenda kumalizia elimu ya sekondari kidato cha tano na sita tena mkoani Iringa na kumaliza mwaka 2016. Kuanzia Oktoba 2017, alianza masomo yake katika chuo kikuu cha usafirishaji (NIT) hadi umauti unamfika 16 Februaria, 2018. Hapo NIT alikuwa anachukua shahada ya kwanza ugavi na ununuzi.

Kifo

Siku ya Ijumaa mnamo tarehe 16 Februari 2018 CHADEMA na kikosi chake walikuwa wanafanya maandamano ya amani ya kushinikiza kupewa fomu za viapo. Wakati wa maandamano haya, inasemekana polisi walitokea kwa mbele na kutoa onyo za mdomo na kuwataka waandamanaji kusitisha maandamano ambayo hayajapewa kibali. Onyo hizo ziliambatana na maneno makali yaliyokuwa yakisemwa iwapo waposimama hatua kali zitachukuliwa dhidi ya waandamanaji. Punde si punde, makabiliano kati ya jeshi la polisi na wafuasi wa chama cha Chadema, yakaanza na kwa maelezo ya jeshi la polisi wanasema walipiga risasi juu ili kutawanyisha waandamanaji na kwa bahati mbaya sana risasi imerudi chini na kumpiga upande wa kushoto Akwilina Akwilini. Mwanafunzi huyo wa chuo cha usafirishaji Tanzania NIT ambaye baada ya tukio jina lake na picha vilisambazwa katika mitando ya kijamii alipigwa risasi akiwa ndani ya basi au maarufu kama daladala jijini Dar es salaam siku ya Ijumaa majira ya jioni, ikiwa siku moja kabla ya uchaguzi mdogo wa eneo ubunge la kinondoni kufanyika. [6]

Kulingana na mashuhudia, wanasema kuwa maafisa wa polisi walitumia vitoa machozi na risasi katika harakati za kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama cha Chadema waliokuwa wakiandamana hadi afisi za tume ya uchaguzi. Katika mbilinge hilo, baadhi ya wanachama wa CDM walikamatwa.

Baada ya taarifa kuenea, shirika la habari la BBC walienda kuzungumza na mkuu wa chuo cha NIT Prof. Zacharia Mganilwa alithibitisha kuwa mwanafunzi wao wa shahada ya Manunuzi na Ugavi Akwilina Akwilini alifariki dunia siku ya Ijumaa. Mganilwa alisema kuwa mwili wa msichana huyo ulikuwa na jeraha la risasi kichwani.

Maziko na gharama zake

Baada ya masiku kupita na ndugu wa familia kutaka kujua chanzo cha umauti wa binti yao, ripoti ikaja amepigwa na ncha kali. Majibu ambayo wengi hawakuyapenda. Baada ya joto kuwa kubwa mtandaoni wakihoji uhalali wa majibu mepesi kwa maswali mazito, ndipo jibu lilipotoka ya kwamba chanzo ni risasi iliyopigwa hewani na kupoteza mwelekeo.[7] Taarifa za awali zilikuwa zinasema ya kwamba suala la uchunguzi litachukua takribani siku 14, ndipo walipoazimia kuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya maandalizi ya maziko huku wakisubiri ripoti ya mwisho. Baada ya majadiliano ya ndani ya familia, walikuja na bajeti ya shilingi za Kitanzania milioni themanini lakhi moja na elfu hamsini (80,150,000). Bajeti hii ilizua taharuki kubwa mno mtandaoni. Wengine waliona kama usanii, wengine kufa kufaana, na wengine waliona kama vile kufanya mtaji suala la kuzika.[8] Mchanganuo wa bajeti wa bajeti hiyo ya familia unaonesha kuwa jeneza ni Sh milioni 1.5, malipo hospitali Sh 200,000, gari ya kusafirisha mwili Sh milioni 3, magari ya kusafirisha wafiwa makubwa matano Sh milioni 20, chakula njiani Sh milioni 3, chakula kwenye msiba Mbezi kwa siku tatu Sh milioni 10, viti 200 Sh 400,000. Turubai kwa siku tatu ni Sh 600,000, mwongoza shughuli Sh 400,000, picha Sh milioni 1 na maji ya kutumia nyumbani Sh 50,000. Kwa pande wa Rombo, Kilimanjaro, chakula kwa siku tano ni Sh milioni 30, muziki na mwongoza shughuli Sh 200,000, turubai Sh milioni 1, viti Sh 400,000, kinywaji cha mabora Sh 100,000, kaburi la kisasa Sh milioni 3, maua na mataji Sh milioni 1, mapambo Sh 500,000 na dharura na tahadhari Sh milioni 2. Awali, ilionekana kama kuna mgomo baridi kutoka serikalini kuhusu kugharamia mazishi hayo kwa bajeti iliyotajwa, lakini baada ya muda kadhaa serikali iliridhia lakini kwa masharti ya kugharamia yenyewe mazishi na si kutoa fedha taslimu.[9][10] Baada ya mivutano mingi, hatimaye hatua ya maziko ya Akwilina yalianza Dar es Salaam katika viwanja vya chuo NIT tarehe 22 Februari 2018 kumuaga kwa watu wa DAR, halafu tarehe 23 Februari safari ya kwenda Rombo kwa maziko.[11]

Marejeo