Mungu ibariki Afrika
Mungu Ibariki Afrika ni wimbo wa taifa wa Tanzania. Jina linatokana na maneno yake ya kwanza.
Asili yake ni wimbo Nkosi Sikelel' iAfrika wa Afrika Kusini. Enoch Sontonga ndiye mtunzi wake mwaka 1897.
Sehemu ya wimbo huu inatumika pia katika nyimbo za taifa za Afrika Kusini na Zambia. Huko nyuma ulitumiwa kama wimbo wa taifa wa Zimbabwe.
Mungu ibariki Afrika
- Mungu ibariki Afrika
- Wabariki viongozi wake
- Hekima, Umoja na Amani
- Hizi ni ngao zetu
- Afrika na watu wake
KIITIKIO:
- Ibariki Afrika
- Ibariki Afrika
- Tubariki watoto wa Afrika
- Mungu ibariki Tanzania
- Dumisha Uhuru na Umoja
- Wake kwa Waume na Watoto
- Mungu ibariki Tanzania na watu wake
KIITIKIO:
- Ibariki Tanzania
- Ibariki Tanzania
- Tubariki watoto wa Tanzania
Historia yake kwa urefu
[hariri | hariri chanzo]Wimbo "Nkosi Sikelel' iAfrika", yaani "God Bless Africa", ulitungwa na Enoch Sontonga, Mxhosa, raia wa Afrika Kusini, na baadaye kutafsiriwa na kanali Moses Nnauye kwenda Kiswahili kuwa "Mungu ibariki Afrika".
Ulikuwa wimbo wa African National Congress (ANC) walipokuwa wanapambana na ukandamizaji wa Makaburu.
Pamoja na kutumika katika Afrika Kusini, umeimbwa pia katika nchi nyingine, kwa mfano Zimbabwe na Namibia, na labda hata Botswana, Eswatini, Lesotho na Malawi kwa miaka mingi.
Hata kabla ya TANU (Tanganyika African National Union) kuanzishwa mwaka wa 1954, wimbo huo, Nkosi Sikelel' iAfrika, ulikuwa unaimbwa Afrika Kusini, kama vile chama cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC), kilivyoanzishwa miaka mingi kabla ya chama cha TANU.
Kwenye mkutano wa kwanza uliofanyika Bloemfontein ili kuanzisha chama hicho mwaka wa 1912, waliimba Nkosi Sikelel' iAfrika. Julius Nyerere alikuwa bado hajazaliwa. Chama kilichoanzishwa kiliitwa South African Native Congress chini ya uongozi wa John Dube, Mzulu, na Pixley ka I. Seme pia kutoka Natal kama Dube. Kikabadilishwa jina baadaye na kuitwa African National Congress (ANC).
Kuanzia mwaka wa 1925, wana ANC waliuchagua wimbo huo, Nkosi Sikelel' iAfrika, kama wimbo wao wa taifa na bado unaimbwa leo.
Katika nyimbo za mataifa yetu ya Kiafrika, hakuna wimbo mwingine unaojulikana kama wimbo huo. Hata katika nchi za Afrika Magharibi, watu wengi wanajua Nkosi Sikelel' iAfrika ni wimbo gani na unamaanisha nini. Hata Kenya wanaimba wimbo huo. Unaimbwa na unafahamika katika nchi nyingi hata kaskazini mwa bara hili. Ukienda Misri, Algeria na nchi nyingine huko, utawakuta watu wengi wanaojua kuhusu Nkosi Sikelel' iAfrika.
Enoch Sontonga alitoka Eastern Cape Province, jimbo la Waxhosa, ambako pia ni nyumbani kwa Nelson Mandela. Alitunga wimbo huo kama wimbo wa Kanisa katika lugha yake ya Kixhosa kama wimbo wa bara lote. Ndiyo maana alisema Nkosi Sikelel' iAfrika, God Bless Africa, si God Bless South Africa.
Alipotunga wimbo huo mwaka wa 1897, haukuimbwa hadharani mpaka mwaka wa 1899. Uliimbwa kanisani kwa mara ya kwanza mwaka huo. Halafu, baada ya miaka kumi na tatu, uliimbwa kwenye mkutano wa kwanza wa South African Native Congress mwaka wa 1912 uliofanyika Bloemfontein kuanzisha chama hicho kugombea haki za Wafrika.
Hata Watanganyika wengi waliokwenda kufanya kazi migodini Afrika Kusini miaka ya 1940 na 1950 waliujua wimbo huo. Walikuwa wanaimba Nkosi Sikelel' iAfrika pamoja na watu wa Afrika Kusini walipokuwa huko na waliporudi Tanganyika.
Watanganyika wengi, mara baada ya kupata uhuru, walikuwa au waliona music sheets za wimbo huo nchini Tanganyika ikiwa na jina la Enoch Sontonga kama ndiye mtunzi wa wimbo huo. Ilikuwa katika lugha mbili, Kiswahili na Kiingereza, na kichwa chake kilikuwa Mungu Ibariki Afrika, God Bless Africa, yaani Nkosi Sikelel' iAfrika.
Sikiliza wimbo huo katika Youtube ambao mmoja wa waimbaji wake katika video ni Miriam Makeba. Ukiusikiliza muziki wake, hauna tofauti hata kidogo na ule wa wimbo wa taifa, Mungi Ibariki Afrika, au wa wimbo wa taifa wa Zambia.
Nyimbo nyingi za Enoch Sontonga zilikuwa nyimbo za huzuni kuhusu maisha magumu ya Wafrika chini ya utawala wa Wazungu waliokuwa wanawakandamiza Wafrika katika bara lote. Wimbo wake, Nkosi Sikelel' iAfrika, ulitokana na maumivu hayo ya Wafrika ingawa pia ulikuwa wimbo wa kuwapa tumaini kwamba hawako peke yao. Mungu yuko nao, au yuko nasi, ingawa tunaumia na tunateswa na wanaotutawala kwa mabavu.
Wimbo huo, Nkosi Sikelel' iAfrika, uliwekwa kwenye sahani ya santuri kwa mara ya kwanza huko London, mwaka wa 1923. Uliimbwa na Solomon Plaatje, mwimbaji maarufu wa Afrika Kusini ambaye pia alikuwa mmoja wa Wafrika walioanzisha chama cha South African Native Congress, Bloemfontein, mwaka wa 1912.
Ni wimbo wa Watanzania pia kwa sababu Afrika ni moja. Kwa hiyo hawakuiba wala kuazima wimbo huo kwa kuufanya wimbo wa taifa. Ni wa watu wa Afrika Kusini na wa nchi nyingine zote za Afrika vilevile.
Utumizi wa wimbo huo unaonyesha umoja na undugu wa Waafrika. Ndiyo maana kulikuwa hata vyama vilivyopigania uhuru ambavyo majina yao yalifanana au yalikuwa karibu sana. Kwa mfano, African National Congress (ANC) iliyoundwa Tanganyika na kuongozwa na Zuberi Mtemvu na katibu wake mkuu John Chipaka ilikuwa na jina sawa na la chama cha Afrika Kusini cha akina Mandela.
Pia chama cha kwanza kupigania uhuru Northern Rhodesia kilichoongozwa na Harry Nkumbula kilikuwa kinaitwa African National Congress, na kiliendelea kuitwa hivyo hata baada ya wanachama wengine kuondoka na kuunda chama kingine, United National Independence Party (UNIP), chini ya uongozi wa Kenneth Kaunda.
Kenya kulikuwa na Kenya African Union (KAU) kabla ya Tanganyika African National Union. Baadaye KAU ikabadili jina kidogo na kuitwa KANU. Na ndugu zetu Zimbabwe waliunda chama kinachoitwa ZANU baada ya baadhi yao, pamoja na Robert Mugabe, kuondoka na kuachana na ZAPU.
Majina hayo, katika nchi mbalimbali, yanafanana kwa sababu Waafrika wanajiona na kweli ni ndugu, bila kujali kabila, rangi, dini, au asili. Pia inaonyesha ushirikiano wao. Hata Uganda, jeshi lao ni Uganda People's Defence Forces (UPDF), jina linalotokana na jina la Tanzania People's Defence Forces (TPDF).
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- [1] Archived 13 Oktoba 2011 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mambo ya muziki bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mungu ibariki Afrika kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |