Carl Linnaeus

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Carl Linnaeus 1775

Carl Linnaeus (tamka: Karl Lineus; pia kwa umbo la Kilatini Carolus Linnaeus na baadaye Carl von Linné; 23 Mei 170710 Januari 1778) alikuwa mwanasayansi nchini Uswidi aliyeweka misingi ya biolojia ya kisasa kwa kuunda utaratibu wa taksonomia au uainishaji wa mimea na wanyama katika vikundi mbalimbali na kuvipa majina ya kisayansi.

[hariri] Familia na elimu yake

Linnaeus alizaliwa kama mtoto wa mchungaji wa Kiluteri katika Uswidi ya kusini. Akasoma tiba, botania na zuolojia kwenye chuo kikuu cha Uppsala akaendelea kufundisha botania kuanzia 1730. 1732 alifanya safari katika Uswidi ya kaskazini alipokusanya mimea mingi na kuipanga katika vikundi. Katika kazi hizi alitambua kasoro za uainishaji jinsi ilivyokuwa kawaida wakati ule akaanzisha mpangilio mpya. 1935-1738 alikaa Uholanzi alipochukua shahada ya daktari. Alifanya pia safari za Uingereza na Ufaransa alipofanya utafiti wa mimea kutoka pande zote za dunia alizoona kwa wafanyabiashara waliokuwa na bustani ya sampuli kutoka koloni za nchi hizi. Wakati huu alitoa toleo la kwanza la kitabu chake juu ya "systema naturae" au muundo wa utaratibu wa viumbe alimopanga aina za mimea, wanyama na mawe.

[hariri] Profesa wa botania

Baada ya kurudi Uswidi alipata nafasi ya profesa ya botania kwenye chuo kikuu cha Uppsala alipoendelea kufundisha na kuandika. Aliendelea kuboresha kitabu cha "systema naturae" akatoa kitabu cha pili kilichokuwa muhimu kwa wanafuzi wake "Species Plantarum" (aina za mimea).

1757 Linnaeus alipewa cheo cha mkabaila na mfalme wa Uswidi akajiita Carl von Linné. Akaendelea kufundisha hadi alipogonjeka mnamo 1774 na kiharusi. Aliaga dunia 10 Januari 1778 mjini Uppsala akazikwa katika kanisa kuu ya mji huu.

[hariri] Umuhimu wake

Utaratibu wa uainishaji wa Linnaeus unaendelea hadi leo na kila mmea au mnyama una jina la kisayansi yenye sehemu mbili; sehemu ya kwanza inataja jenasi na sehemu ya pili spishi. Kwa kawaida inafuatwa na herufi ya kwanza ya jina la mtaalamu aliyeeleza spishi hii mara ya kwanza katika maandiko ya kisayansi.

Hadi leo aina za mimea au wanyama zilizoainishwa na Linnaeus inatajwa kwa herufi "L." baada ya jina la kisayansi, kwa mfano mpunga ni mmea wa jenasi inayotajwa kwa jina la kisayansi kama Oryza (L.) na "L." katika mabano inaonyesha jenasi hii ilielezwa mara ya kwanza na Linnaeus. Jina la kisayansi ya simba Panthera leo L. kwa sababu pia mnyama huyu aliwekwa na Linnaeus katika utaratibu wa uainishaji wa kisayansi.

Pesa ya Uswidi inaonyesha picha yake kwenye benknoti ya krona 100.