Nenda kwa yaliyomo

Ziwa la chumvi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ziwa la magadi)
Jangwa la chumvi Bonneville katika Utah lilikuwa ziwa na kila majira ya mvua linafunikwa na maji yenye kimo cha sentimita 30.
Jangwa la chumvi Bonneville katika Utah wakati wa joto.

Ziwa la chumvi (kwa Kiingereza: salt lake) ni aina ya ziwa ambalo maji yake huwa na kiwango kikubwa cha chumvi ndani yake. Kwa kawaida karibu kila mahali maji yanayopatikana duniani huwa na kiwango fulani cha chumvi ndani yake. Binadamu, wanyama na mimea mingi huhitaji maji matamu ambayo kiwango cha chumvi kipo chini ya asilimia 0.1 au gramu moja ya chumvi katika kila lita ya maji.

Uainishaji wa maziwa ya chumvi[hariri | hariri chanzo]

Kwa kawaida "ziwa la chumvi" hufafanuliwa kuwa na asilimia 0.5 au zaidi ya chumvi, yaani gramu 5 za chumvi katika lita moja ya maji. Viwango vya uchumvi hutofautishwa hivi:[1]

  • Uchumvi mdogo (subsaline) ‰ 0.5–3
  • Uchumvi juu (hyposaline) ‰ 3–20
  • Uchumvi kuu (mesosaline) ‰ 20–50
  • Uchumvi kabisa (hypersaline) juu ya ‰ 50


Chumvi katika maziwa haya kwa kawaida ni mchanganyiko wa chumvi tofautitofauti zinazotegemea tabia za kikemia za ardhi ambako usimbishaji wa mvua na mito inapita; mara nyingi ni hasa chumvi ya kloridi ya natiri (NaCl). Pale ambapo kiwango cha kabonati ni cha juu, thamani pH huongezeka katika maji: hapo maziwa yanaweza kuitwa "maziwa ya magadi".

Kuna pia maziwa ambapo kiwango cha fosfeti kinaweza kuwa juu.

Tabia[hariri | hariri chanzo]

Maziwa ya chumvi hutokea kama kama maji yenye kiwango cha chumvi yanaingia ziwani lakini hakuna njia ya kutoka. Ziwa hupotea maji kwa njia ya uvukizaji, chumvi hubaki na polepole kiasi cha chumvi ndani ya ziwa huongezeka.

Kuongezeka kwa ukali wa maji ya chumvi kunaleta mabadiliko katika wanyama na mimea ziwani; wasioweza kuvumilia chumvi nyingi hupotea, wakibaki wale wanaostawi katika mazingira ya chumvi; inawezekana kuna spishi chache sana zinazobaki katika mazingira ya ziwa la chumvi.

Kama kiasi cha maji yanayoingia ziwani ni kidogo kuliko kiasi kinachovukiza ziwa litapungua hadi kupotea kabisa na kuonekana tu kama tambarare ya chumvi. Katika mazingira ya joto mara nyingi ziwa la chumvi lenye kimo kidogo linakauka katika majira ya joto kuwa jangwa la chumvi lakini hufunikwa tena maji wakati wa mvua.

Mtalii katika Bahari ya Chumvi anaelea juu ya maji akisoma gazeti lake

Katika maziwa yenye uchumvi mkuu maji yake huwa na densiti kubwa inayosababisha binadamu kuelea juu ya maji bila kuzama; mfano mashuhuri ni Bahari ya Chumvi huko Israeli - Palestina - Yordani.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Hammer, U. T. (1986). Saline Lake Ecosystems of the World. Springer. p. 15. ISBN 90-6193-535-0