Walimwengu
"Walimwengu" | ||
---|---|---|
Kiwambo cha video ya Walimwengu | ||
Wimbo wa Nuru the Light | ||
Umetolewa | 2007 | |
Umerekodiwa | 2006 | |
Aina ya wimbo | Bongo Flava, afro-pop | |
Lugha | Kiswahili | |
Urefu | 3:09 | |
Studio | SoulHouse Studio | |
Mtunzi | Nuru the Light |
Walimwengu ni jina la wimbo uliotoka 2007 kutoka kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka nchini Tanzania, Nuru the Light. Katika wimbo, Nuru ameangalia sana tabia za kibinadamu ambazo rahisi kutokea. Namna watu wanavyokupenda ukiwa na kitu halafu kukubadilikia ukiwa huna kitu. Hali ambayo inatokea kila siku katika jamii yetu. Hii ni kazi ya SoulHouse Studio, huku video ikiwa kazi ya Adam Juma kupitia Visual Lab.
Historia ya wimbo
[hariri | hariri chanzo]Kikazi, huu ndio wimbo wa kwanza wa Nuru kuimba Kiswahili. Wazo la kuandika wimbo lilimjia akiwa anasafisha ukumbini kwake na punde akawaza sana maisha ya nyumbani Tanzania na namna watu wanavyomchukulia amekulia Ulaya. Wakati huo kabla ya wimbo, alikuwa akija Tanzania anakuja na rundo la mabegi yaliyojawa mazawadi ya kila aina. Kwa tabia hiyo, akagundua kama anapendewa kitu na si utu wake. Tangu hapo akaona sasa isiwe shida heri tu aachane na ubebaji wa mabegi ya zawadi. Fikra hizi za kuwa wewe wa Ulaya au Amerika ukija una mazawadi imetawaliwa na watu wengi sana. Sehemu kubwa ya wanadamu huamini ya kwamba mtu kutoka nchi za nje lazima we na kila cha kumsaidia aliye katika bara la Afrika. Mawazo ambayo Nuru aliyaona si sawa. Wimbo uko binafsi sana namna ambavyo unaimbwa. Kaimba katika sauti ya huzuni yenye kulalamikia miyenendo mibaya ya raia wenza wenye tabia kama hizi za kudhani waliopo nje ya nchi wakija TZ basi mijihela na mizawadi tu na si kingine. Hali halisi ya wimbo inagusa wengi na imewatokea hasa ukiachia Nuru yeye binafsi kuonelea kutunga wimbo huu. Ndani ya wimbo hakuzungumzia mapenzi bali hali halisi ya maisha ya kitegemezi kwa Waswahili.
Maudhui
[hariri | hariri chanzo]Wimbo unaanza na kiitikio kinasema;
“Walimwengu ni wazuri, ukiwa na mali” “Walimwengu ni wazuri, ukiwa na mali” “Mali ikiisha, watu wote, huwaoni” “Mali ikiisha, watu wote, huwaoni”
Ubeti wa kwanza
[hariri | hariri chanzo]Baada ya upepo wa pesa kwenda kusi, ndugu na jamaa wamepotea. Marafiki nao ndio usiseme kabisa. Chambi kwisha kila mtu kaingia mitini. Nuru kabaki peke yake. Kachanganyikiwa kiasi hata hajui kama anaota au la. Maisha kizungumkuti unaowajua wamesepa. Baada ya kilio anarudia tena kiitikio.
Ubeti wa pili
[hariri | hariri chanzo]Akirudi katika ubeti wa pili, anajiuliza na maisha yake afanyeje. Njaa kali na maisha msoto. Ngoma ngumu hadi mpenzi wake nae kabwaga manyanga. Walimwengu wazito sana. Pamoja na yote hayo, bado hajakata tamaa anaamini Mungu bado yupo naye. Ya dunia yakupita na si ya kuganda. Wakati mwingine upitie magumu ili heri ije.
Video ya muziki
[hariri | hariri chanzo]Video ilifanywa huko mjini Zanzibar. Siku ya kupiga video kulikuwa na bonge la mvua. Hali ambayo ilipelekea kushindikana kufanya video hiyo nje na ilikuwa siku hiyo-hiyo tu kwani siku inayofuata Nuru alikuwa anarudi Sweden. Video ilitengenezwa kwa muda wa masaa yasiyozidi matatu. Vipande vya nje vimepigwa kwa dakika zisizozidi hamsini tu baada ya mvua kukata. Na ilitakiwao ubunifu wa hali ya juu ili kutosha wakati huo na ndio maana katika video ameonekana na mavazi mawili tu na sio zaidi ya hayo na punde baada ya kumaliza imlimbidi awahi boti la kurudi mjini Dar es Salaam.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Walimwengu katika YouTube