Shirikisho la Amerika ya Kati

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ramani ya Shirikisho la Amerika ya Kati

Shirikisho la Amerika ya Kati (kwa Kihispania: Confederación de Centroamérica), pia: Muungano wa majimbo ya Amerika ya Kati (Provincias Unidas del Centro de América) lilikuwa muungano wa maeneo ya Amerika ya Kati tangu mwaka 1823 hadi 1838. Lilijumlisha nchi tano za Guatemala (pamoja na Belize), El Salvador, Honduras, Nikaragua na Kosta Rika.

Kabla ya mwaka 1821 nchi hizo zote zilikuwa makoloni ya Hispania na sehemu za Jimbo Kuu la Guatemala chini ya ufalme mdogo wa Hispania Mpya. Wakati wa kuasi kwa makoloni ya Hispania katika Amerika jimbo kuu la Guatemala lilijiunga na nchi mpya ya Meksiko kwa muda mfupi. Baada ya kupinduliwa kwa mtawala wa kwanza wa Meksiko Agustin de Iturbide jimbo kuu la Guatemala likaamua kuwa nchi ya pekee.

Shirikisho la Amerika ya Kati likaanzishwa mwaka 1823 na mji mkuu ulikuwa Guatemala City. Nchi mpya ilikuwa na matatizo mengi. Mawasiliano yalikuwa magumu kutokana na ukosefu wa barabara. Viongozi wa kila sehemu walitafuta mambo yao bila kujali hali ya shirikisho. Hofu ya kipaumbele cha Guatemala ilisababisha uhamisho wa mji mkuu kwenda El Salvador mwaka 1831.

Jamhuri ikaporomoka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 1838. Nikaragua ikajiondoa katika shirikisho tarehe 30 Aprili 1838, Honduras ikafuata tarehe 26 Oktoba na Kosta Rika tarehe 14 Novemba 1838. Guatemala ikaondoka mwaka 1839 na El Salvador ikabaki pekee yake hadi kufuta jina la shirikisho mwaka 1841.

Majaribio yote ya kuunganisha tena nchi za Amerika ya Kati yalishindikana.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Shirikisho la Amerika ya Kati kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.